Bluefins yashinda ubingwa kuogelea Morogoro

  Masama Blog      
Klabu ya Bluefins ya Upanga jijini Dar es Salaam imeshinda ubingwa wa mashindano ya kuogelea ya Morogoro baada ya kukusanya pointi  2,621 na kuzipiku klabu nyingine zilizoshiriki.

Mashindano hayo yalifanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Morogoro (MIS) yalishirikisha jumla ya waogeleaji 190 kutoka klabu nne nchini.

Bluefins ambayo inaundwa na wachezaji  chipukizi, iliweza kuzipiku klabu tatu, Taliss-IST, Dar Swim Club na wenyeji, Mis Piranhas.

Mashindano hayo yalikuwa magumu na waogeleaji wa kike wa klabu hiyo waliweza kukusanya jumla ya pointi 1,224  wakati wavulana walikusanya pointi 1,397 na kuibuka kidedea.

Muasisi na kocha mkuu wa timu hiyo, Rahim Alidina alisema kuwa ushindi huo umetokana na ushirikiano baina yao na makocha, wazazi, wadau na juhudi za waogeleaji kuiletea sifa klabu yao.

Alisema kuwa walikuwa wanasaka mafanikio hayo tokea mwaka 2018 baada ya kushinda nafasi ya pili na mwaka jana walishinda pia nafasi ya pili.

“Haikuwa kazi rahisi kutwaa ubingwa huu, mashindano yalikuwa magumu sana, nawapongeza wote waliofanikisha ushindi huu na kuanza mwaka 2020 vizuri,” alisema Alidina.

Waogeleaji wa kike walioleta sifa katika klabu hiyo ni Aliyana Kachra, Zainab Moosajee, Maryam Ipilinga, Alexis Misabo, Aminaz Kachra, Lina Goyayi, Muskan Gaikwad, Filbertha Demello, Niharika Mahapatra, Yumna Hassan na Natalia Ladha.

Waogeleaji wa kiume walioleta sifa ni pamoja na  Mohammadhussein Imran, Kaysan Kachra, Sahal Harunani, Moiz Kaderbhai, Jay Govindji,Raihan Abdullatif, Hassan Harunani, Idris Zavery, Isaac Mukani, Kabeer Lakhani, Salman Yasser, Gervas Sayi na  Delbert Ipilinga.

Pia wamo, Zac Okumu, Adam Patwa, Qais Kanji, Kahil Walli, Christian Fernandes, Avinav Mahapatra, Aaron Akwenda, Shuneal Bharwani, Enrico Barretto, Burhanuddin Gulamhussein na Rayyan Khan.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na klabu ya Taliss-IST iliyopata pointi  2,583 wakati  Mis Piranhas walimaliza katika nafasi ya tatu kwa kupata pointi 1,914 na Dar Swim Club (DSC) ilipata jumla ya pointi  1907 na kumaliza katika nafasi ya nne.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/3699gb9
via
logoblog

Thanks for reading Bluefins yashinda ubingwa kuogelea Morogoro

Previous
« Prev Post