Ticker

10/recent/ticker-posts

BENKI KUU YA TANZANIA YABAINI UWEPO WA MATAPELI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA FEDHA, VICOBA FOUNDATION YAHUSISHWA


Na Said Mwishehe,Michuzi Globu

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT)imesema imebaini uwepo wa kampuni za kitapeli zinazodai kutoa mikopo kwa wananchi ndani ya muda mfupi baada ya kujiunga kwa kuweka amana kwa njia ya mtandao.

Taarifa ya BoT kwa vyombo vya habari ambayo imetolewa leo Januari 9, 2020 imesema kuwa kampuni hizo ni pamoja na ile inayojiita VICOBA Foundation, ambayo imekuwa ikijinasibu kutoa mikopo ya kuanzia Sh. 2,000,000.00 hadi Sh.10,000,000.00 baada ya mteja kulipia ada ya kujiunga ya kati ya Shilingi za Kitanzania 200,000.00 hadi 500,000.00.

Aidha, ili kuvutia wananchi, Kampuni hiyo imekuwa ikiudanganya Umma kwamba ni Taasisi ya Serikali, jambo ambalo halina ukweli wowote.

Kwa mujibu wa BoT ni kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba Kampuni hii haina hata ofisi ya kudumu. Vile vile, Kampuni hii imekuwa ikitumia majina ya viongozi wakuu wa nchi na watu mashuhuri katika kufanikisha utapeli wao yakiwemo majina ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hasan na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.

"Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuufahamisha Umma kwamba mmiliki wa VICOBA Foundation kwa sasa anashikiliwa na Vyombo vya Dola ambavyo vinaendelea na uchunguzi ili kuchukua hatua stahiki. Benki Kuu ya Tanzania kama Msimamizi wa Sekta ya Fedha, vikiwemo VICOBA, inapenda kuutahadharisha Umma kutojihusisha na huduma zozote zinazotolewa na Kampuni za namna hii ili kuzuia upotevu wa

fedha zao,"imesema taarifa hiyo.

Aidha, Benki Kuu ya Tanzania inatoa onyo kwa mtu, kikundi au taasisi yoyote inayojihusisha na biashara ya upokeaji amana na/au utoaji wa mikopo bila kuwa na leseni kuacha mara moja.

Pia BoT imesema  inaukumbusha Umma kwamba

Kifungu cha 6 (1) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, kinakataza mtu yeyote kufanya biashara ya benki au kupokea amana kutoka kwa Umma bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya 2018, kinakataza mtu binafsi, kampuni au kikundi kilichoanza

biashara kuanzia tarehe 1 Novemba 2019 kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila kuwa na leseni halali inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania.


 Watu binafsi, makampuni na vikundi vilivyokuwa vinatoa huduma ya kupokea amana na/au kutoa mikopo kabla ya tarehe 1 Novemba 2019, vinapaswa kuomba leseni ya biashara kutoka Benki Kuu ya Tanzania kabla ya tarehe 31 Oktoba 2020 bila kukosa. Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu binafsi, kampuni au kikundi chochote kitakachofanya biashara ya kupokea amana na/au

kutoa mikopo bila kuwa na leseni stahiki kwa mujibu wa Sheria.


"Wananchi wanaombwa kutoa taarifa Benki Kuu ya Tanzania, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pale wanapopata taarifa za uwepo wa watu binafsi, kampuni au vikundi vinavyotoa huduma za fedha bila kuwa na leseni ya Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, wananchi wenye dukuduku au taarifa tajwa, wanahamasishwa kuwasiliana na Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania-

Makao Makuu, Ghorofa ya 6 Mnara wa Kaskazini, S.L.P. 2939, Mtaa wa

2 Mirambo, 11884 Dar es Salaam au namba za simu +255-22-223-5483;

+255-22-223-5584; au +255-22-223-5557 au barua pepe kwa

vctarimu@bot.go.tz; nfmongateko@bot.go.tz; na dasasya@bot.go.tz.

BENKI KUU YA TANZANIA

botcommunications@bot.go.tz,"imeeleza taarifa hiyo ya BoT.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2uuNscR
via

Post a Comment

0 Comments