WAWILI WARUHUSIWA KATI YA 55 WALIOKULA CHAKULA CHENYE 'SUMU'

  Masama Blog      
Charles James, Michuzi TV

WAGONJWA waliofikishwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ilifikia 55 ambapo wawili kati yao wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya hali zao kutengamaa.

Idadi hiyo ya watu walifikishwa hospitalini hapo baada ya kupata ugonjwa wa kuhara na kutapika kwa kile kinachosadikiwa kula chakula chenye sumu kwenye msiba wa jirani yao eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Akizungumza hospitalini hapo alipoenda kuwajulia hali wagonjwa hao, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe DkBinilith Mahenge amewapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali hiyo kwa namna walivyowahudumia wananchi hao kwa haraka na kujitahidi kumaliza tatizo hilo.

Amesema idadi ya waliyofika hospitalini hapo walikua ni 45 lakini baadaye Serikali iliamua kupeleka gari mbili za wagonjwa ambapo wengine 10 walijitokeza na kuchukuliwa baada ya kufanyiwa vipimo.

" Tunawashukuru sana matabibu wetu hakika wamefanya kazi nzuri sana, nimepita wodi zote kukagua hali za wagonjwa ambao wote wamehudumiwa bure wanaendelea vizuri.

Niwaombe wananchi wetu wawe wasafi hasa katika mikusanyiko ya watu, lakini pia niwatake wawe watulivu wakati huu ambao Serikali inafanya uchunguzi wake kubaini nini chanzo cha tatizo hilo, " Amesema Dk Mahenge.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Best Magoma amesema utafiti unaendelea kujua chanzo cha ugonjwa huo huku akisema mpaka kufikia jioni idadi kubwa ya wagonjwa watakua wameruhusiwa kurudi majumbani mwao.

" Hali za wagonjwa ni nzuri na wengi wao tutawaruhusu leo kurejea majumbani mwao, jana tulifika kwenye eneo la tukio tukachukua sampo ya  Chakula, Maji na Damu kwa ajili ya kufanyia uchunguzi, " Amesema Dk Magoma.
 Wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ambao walipata ugonjwa wa kuhara na kutapika baada ya kula kinachodaiwa kuwa na sumu.
 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge akizungumza na wandishi wa habari alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo baada ya kudaiwa kula Chakula chenye sumu
 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Best Magoma Akitolea ufafanuzi kuhusiana na hali ya wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo baada ya kula Chakula kinachodaiwa kuwa na sumu.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2S77eoP
via
logoblog

Thanks for reading WAWILI WARUHUSIWA KATI YA 55 WALIOKULA CHAKULA CHENYE 'SUMU'

Previous
« Prev Post