WANAYOJIVUNIA WANANCHI WA WILAYA YA NYASA KATIKA MIAKA MINNE YA RAIS DK.JOHN MAGUFULI

  Masama Blog      
Na Said Mwishehe-Michuzi TV-Nyasa

WANANCHI wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma katika miaka minne ya Rais Dk.John Magufuli wanajivunia mambo makubwa matatu likiwemo la kwanza la kutengenezwa kwa meli tatu ndani ya Ziwa Nyasa na la pili ni uenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 67 kutoka Mbinga hadi Mbambabay.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi , Mkuu wa wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba amesema katika miaka minne ya uongozi Rais Magufuli kuna mengi ya kujivunia kwao kayika nyanja mbalimbali za usafiri, afya, elimu, miundombinu pamoja na uboreshwaji wa huduma za kijamii.

"Tunachojivunia wananchi wa Nyasa katika miaka minne ya Rais Magufuli , kwanza kabisa niseme ni meli tatu ambazo zimetengenezwa katika Ziwa Nyasa kwani hatutakuwa na changamoto ya usafiri wa majini kama ilivyo sasa.

"Jambo la pili la kujivunia miaka minne ya Rais wetu mpendwa ni ujenzi wa barabara ya lami ya kilometa 67 ya Mbinga hadi Mbambabay. Wananchi wameisubiri hii barabara kwa muda mrefu na ilifika mahali hadi mkandarasi anaweka bango na anaanza ujenzi wananchi wanasema hakuna kitu.

"Sisi Nyasa tupewe barabara haiwezekani, hata wakiambiwa kazi ndio imeaaza hawaamini lakini leo hii sote ni mashahidi lami inaendelea kutandikwa na Septemba mwaka 2020 itakuwa imekamilika yote,"amesema Chilumba wakati anaelezea maendeleo ambayo yamefanyika katika Wilaya yao.

Pia amesema katika sekta ya elimu nako kuna mambo makubwa ya yamefanyika ambayo wanajivunia nayo ambapo amezungumzia majengo ya shule ambayo yamejengwa katika Sekndari ya Mbambabay.

"Kuna shule ya sekondari Mbambabay ambayo mwaka 2016 ilikuwa imeanza kidato cha tano na sita, shule hii imejengwa kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu na kisasa.Pia kumekuwa na uboreshaji wa miundombinu katika shule za msingi na sekondari ndani ya wilaya ya Nyasa,"amesema na kuongeza hata ghala kubwa la chakula kushinda yote mkoani Ruvuma liko Mbambabay.

Katika sekta ya afya,Chilumba amesema wamejenga hospitali ya wilaya ya Nyasa na wiki iliyopita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Seleman Jafo amefanya ziara katika wilaya hiyo na kutoa pongezi nyingi kutokana na maendeleo yaliyopo.

"Mbali ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya , kuna vituo vya afya viwili ambavyo tayari vimekamilika na vinaweza kutumika , kimoja tumepata fedha juzi.Mengi yamefanyika chini ya uongozi wa Rais Magufuli.

"Huwa najionea maajabu, kwanini, mimi ni mtumishi wa siku nyingi katika Serikali ya mitaa , nimeanzia ngazi za chini kabisa hadi kuwa Mkuu wa Wilaya , katika utumishi wangu huko nyuma sikuwahi kuona tumejenga hospitali 67.Tuzoea kuoa hospitali ni zile zile zaidi ni kuongeza watumishi .Leo hii Serikal imejenga hospitali 67 haya ni maajabu,"amesema.

Ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Rais Magufuli kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Nyasa ambao wamejawa na matumaini na uongozi wake thabiti na wenye kujali wanyonge huku wakisisitiza kazi ya ujenzi wa barabara ya lami na uboreshwaji wa miundombinu ya usafiri wa meli unakwenda kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kasi kubwa.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/356sHkB
via
logoblog

Thanks for reading WANAYOJIVUNIA WANANCHI WA WILAYA YA NYASA KATIKA MIAKA MINNE YA RAIS DK.JOHN MAGUFULI

Previous
« Prev Post