Ticker

10/recent/ticker-posts

WANANCHI WAIOMBA SERIKALI KUHARAKISHA MCHAKATO WA UJENZI WA BARABARA YA KIBAONI - STALIKE, KATAVI

BAADHI ya  watumiaji wa Barabara ya Kibaoni-Stalike wilaya ya Mlele mkoani Katavi, wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa ujenzi wake ili kuwaondolea kero wanayokutana nayo hasa msimu huu wa masika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Ripota Wetu walisema, barabara hiyo yenye urefu wa km 71 inayopita katika ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi  kwa sasa imekuwa kero kubwa kutokana na utelezi  na mashimo,jambo linalo sababisha magari kukwama na kupoteza muda mwingi  wa kufanya shughuli za maendeleo wakiwa njiani.

Athanas John na Miriam Daniel wameiomba Serikali kupitia wakala wa Barabara (Tanroad) mkoa wa Katavi kutafuta fedha ili kuijenga barabara hiyo ambayo  inachangia kurudisha nyuma uchumi wa mkoa wa Katavi na mikoa mingine  ya Rukwa, Kigoma na Tabora.

Athanas alisema, kama barabara hiyo ingejengwa kwa kiwango cha lami basi  kungekuwa na fursa kubwa ya usafiri na usafirishaj bidhaa za mashambani  hivyo kutoa nafasi kwa wananchi kuwahi katika majukumu yao ya  kimaendeleo tofauti na sasa ambapo wanalazimika kutumia masaa mawili hadi matatu.
Baadhi ya  magari yakiwa yamekwama katika Barabara ya Mpanda -Sumbawanga mkoani Katavi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika mikoa ya Nyanda za juu na hivyo kusababisha magari kukwama na kupelekea kero kubwa kwa wasafiri.

Mmoja wa Dereva anayefanya safari zake kati ya mkoa wa Katavi na mkoa  wa Rukwa ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema, barabara imekuwa chanzo cha kuharibika magari yao na hivyo kuwaongezea hasara kubwa.

Alisema, wakati umefika kwa Serikali  kuiangalia barabara hiyo ambayo ni kiungo kikubwa kwa uchumi wa mkoa,  kupitisha mazao na hata kurahisisha shughuli za utalii katika hifadhi  maarufu ya Katavi.

Kwa upande wake Meneja wa Tanroad mkoa wa Katavi Martin Mwakabende alisema, ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa km 71 na kati ya hizo km 44 inapita kwenye hifadhi ya Katavi haujaanza,hata hivyo Ofisi ya Wakala wa Barabara Tanroad imeandaa ripoti ya awali itakayosaidia usanifu wake.

Alisema, Rais Dkt John Magufuri akiwa katika ziara ya siku tatu mkoani Katavi Mwezi Novemba mwaka huu  aliahidi kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Aidha alitaja barabara ya Kizi Lyambamfipa hadi Sitalike yenye urefu wa km86.5 kati ya hizo km 50 zipo kwenye hifadhi ya Katavi bado haujaanza ambapo zoezi la upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulikamilika tangu mwaka 2009 na Serikali inafanya jitihada kutafuta fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2s49f9W
via

Post a Comment

0 Comments