WACHIMBAJI TANZANITE WAFANYA MISA YA KUMSHUKURU MUNGU

  Masama Blog      

WACHIMBAJI wa madini ya Tanzanite wa kampuni ya California Camp eneo la Kitalu B (Opec) Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamefanya misa ya kumshukuru Mungu kwenye mgodi huo kwa kumaliza mwaka salama bila kupata ajali wala misukosuko katika shughuli zao.  

Mkurugenzi wa mgodi huo wa California camp, Deogratius Minja alisema wamefanya misa hiyo ya shukrani katika mgodi huo ili kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka salama na kufanya kazi zao bila matatizo. 

Minja alisema kazi za uchimbaji madini ya Tanzanite ni ngumu na wanamshukuru Mungu kupitia misa hiyo ya shukrani kwa kuwaepusha na ajali kwenye mgodi wao. 

"Shughuli za uchimbaji madini ya Tanzanite ni ngumu na zinahitaji gharama kubwa lakini tunamshukuru Mungu kwa mema yote aliyotujalia na kumaliza mwaka 2019 na kukaribisha mwaka mpya wa 2021," alisema. 

Paroko wa parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozali Takatifu wa Kanisa katoliki Mirerani, Padri Vincent Ole Tendeu aliyasema hayo jana kwenye misa ya shukrani katika mgodi wa madini ya Tanzanite Africa California camp. 

Padri Ole Tendeu alisema mara nyingi watu wana tafsiri potofu kwamba wachimbaji wa madini ya Tanzanite hawapo karibu na Mungu jambo ambalo siyo sahihi. 

Alisema tukio la misa ya shukrani katika mgodi wa kampuni ya California camp imedhihirisha kuwa wachimbaji madini ya Tanzanite wana imani kubwa kwa Mungu na wanamtangukiza mbele katika shughuli zao za uchimbaji madini.  

"Misa hii ya shukrani iliyofanyika kwenye mgodi wa ndugu yetu Deogratius Minja kupitia California camp imetuonyesha imani kubwa kwa Mungu walionao wachimbaji madini ya Tanzanite," alisema padri Ole Tendeu. 

Katekista wa kigango cha Mtakatifu Malaika mkuu Gabriel, Martin Mbuya alisema Mungu ni mwema kwani wamefanikiwa kuwa na eneo la kufanya ibada katika machimbo hayo. 

Mbuya alisema wanamshukuru ofisa madini mkazi wa Mirerani Daudi Ntalima kwa kuwapa fursa ya kupata eneo la kufanya ibada katika machimbo ya madini ya Tanzanite. 

Alisema hivi sasa hakuna ushirikina kwenye madini hayo na wachimbaji wamemtambua Mungu na wanatarajia Tanzanite itapatikana kwa wingi kutokana na imani waliyonayo kwa Mungu. 
Mkurugenzi wa mgodi wa kampuni ya California Camp, Deo Minja akiongoza njia wakati Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozali Takatifu, Padri Vincent Ole Tendeu (kulia) akinyunyiza maji ya baraka kwenye eneo la mgodi.from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2ERXir4
via
logoblog

Thanks for reading WACHIMBAJI TANZANITE WAFANYA MISA YA KUMSHUKURU MUNGU

Previous
« Prev Post