Ticker

10/recent/ticker-posts

UMEME UMEBADILI MAISHA YA WANA-RUVUMA – RC MNDEME

Veronica Simba – Ruvuma

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ameipongeza Serikali kwa kuunganisha umeme wa gridi ya Taifa mkoani humo, ambao umebadili hali ya maisha ya wananchi husika kutoka kwenye uduni na kuwa bora zaidi.

Alikuwa akieleza hali ya upatikanaji umeme mkoani Ruvuma kwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, ambaye alimtembelea ofisini kwake akiwa katika ziara ya kazi, Desemba 12, 2019.

“Tunamshukuru sana Rais John Pombe Magufuli kwa kutuletea umeme. Sisi tangu nchi inapata Uhuru, tulikuwa hatujawahi kupata umeme wa gridi; Sasa hivi tunafurahia umeme kila uchao.”

Akifafanua mabadiliko chanya yaliyoletwa na umeme kwa wananchi wa Ruvuma, Mkuu huyo wa Mkoa alisema yamejikita hasa katika shughuli za kimaendeleo.

Alisema, mashine za kusaga mahindi zilizokuwa zinatumia mafuta ya dizeli na ambazo zilikuwa nyingi, kwa kiasi kikubwa hazipo tena badala yake mashine nyingi sasa zinatumia umeme.

Alieleza zaidi kuwa, uwepo wa mashine zinazotumia umeme kusaga nafaka, kumepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kusaga nafaka hizo kwa wananchi ambao hutumia unga wa mahindi kupikia ugali, ambacho ni chakula chao kikuu.

Vilevile, alieleza kuwa vijiji vingi sasa vimekuwa na mwanga wa umeme hasa nyakati za usiku, tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo vijijini kulikuwa na giza totoro.

Kufuatia suala hilo, aliipongeza serikali kwa kupitisha na kutekeleza azimio la kutobagua aina ya nyumba wakati wa kuunganisha umeme na kusema kuwa wananchi wengi wa maisha ya chini wanafurahia umeme kama wengine wenye kipato cha juu pasipo kujiona wametengwa.

Aidha, alishukuru kwa kazi inayoendelea ya kujenga miundombinu ya umeme ili kupeleka gridi ya Taifa wilayani Tunduru huku akibainisha kuwa ndiyo wilaya pekee mkoani humo ambayo haijafikiwa na umeme wa gridi ya Taifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati alimweleza Mkuu huyo wa Mkoa kwamba kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kupeleka umeme wa gridi Tunduru imekamilika na kwamba katika ziara yake amejiridhisha na hilo.

“Wataalamu wamefanya kazi nzuri sana na kwa sasa wanakamilisha kazi ndogo ndogo tu. Tunatarajia siku yoyote kuanzia hivi sasa, tutazima mitambo ya mafuta Tunduru na kuunganisha umeme wa gridi ya Taifa.”

Katika hatua nyingine, Waziri aliahidi kuwashawishi wawekezaji waende mkoani humo kufanya tathmini kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza nguzo.

Alitoa ahadi hiyo kufuatia maombi ya Mkuu wa Mkoa ambaye alimweleza kuwa mkoa huo pia umejaaliwa kuwa na miti mingi hivyo ingefaa kukawa na kiwanda hicho ili kuunga mkono juhudi za serikali kutumia vifaa vya kuunganishia umeme ambavyo vinatengenezwa ndani ya nchi.


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme (kushoto), akizungumza na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, kuhusu hali ya upatikanaji umeme mkoani humo. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi, Desemba 12, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme (Meza Kuu-katikati), akizungumza na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, kuhusu hali ya upatikanaji umeme mkoani humo. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi, Desemba 12, 2019.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/34fJYay
via

Post a Comment

0 Comments