ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami mkoani Katavi waleta unafuu wa maisha kwa wananchi

  Masama Blog      
Na Muhidin Amri, Mpanda

WAKALA wa Barabara (Tanroad) mkoa wa Katavi, umefanikiwa kujenga jumla ya kilometa 140.23 kati ya km 1,192.07 za Barabara kwa kiwango cha lami katika kipindi cha miaka minne tangu Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani.

Meneja wa Tanroad mkoani Katavi Mhandisi Martin Mwakabende alisema,  km 115.83 ni za Barabara Kuu na km24.4 ni za mkoa  ambapo Serikali kupitia vyanzo mbalimbali  vya mapato imetenga fedha kwa ajili ya kuendelea  kujenga Barabara zenye urefu wa km 235.4 kwa kiwango cha lami.

Kwa mujibu wake, kwa sasa kuna miradi mitano ya ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami inaendelea kutekelezwa katika mkoa huo na ziko katika hatua mbalimbali  ambapo mara zikapokamilika utarahisisha mawasiliano na kuunganisha  mkoa huo na mikoa jirani ya Tabora na Kigoma.

Alitaja miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa katika mkoa huo ni Bara bara ya Mpanda-Inyonga-Sikonge-Tabora km 359 kwa kiwango cha lami ambayo imepata ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika(ADB) ambayo imegawanywa sehemu tatu,Usesula-Komanga km 108,Barabara ya kuunga Mji wa Sikonge(Sikonge Spur) km2.21 na Barabara inayoingia Sikonge mjini yenye urefu wa km 7.36 ambayo ipo mkoani Tabora.

Kwa mujibu wa Mwakabende,sehemu  ya pili ni Komanga-Kisinde km 108  pamoja na Barabara inayoingia Inyonga mjini km 4.14 ambayo sehemu kubwa ya Bara bara hiyo ipo mkoani Katavi ambapo gharama ya ujenzi wake ni shilingi Ml140,025.50 na gharama ya usimamizi ni Ml 7 na sehemu ya tatu ni Kasinde-Mpanda km 108 inayojengwa kwa shilingi Ml 133.8.

Aidha alisema, ujenzi wa Barabara ya Sitalike-Kibaoni yenye km 71 kati ya hizo km 44 inapita kwenye Hifadhi ya Taifa ya Katavi haujaanza ambapo Ofisi ya Wakala wa Bara bara Tanroad imeandaa ripoti ya awali itakayosaidia usanifu.

Wakizungumzia ujenzi huo baadhi ya wananchi  wamepongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali  katika ujenzi wa Barabara inayounganisha mkoa huo na mikoa jirani.

Jackson Kaliba na Amani Bondo wakazi wa Kijiji cha  Hurwila walisema, ujenzi wa Barabara hiyo  umeanza kuleta nafuu ya maisha  ikiwemo kupungua kwa nauli kutoka shilingi elfu tatu hadi kufikia  shilingi elfu moja na mia tano,kupungua kwa muda waliokuwa wanautumia hadi makao makuu ya wilaya  Mpanda mjini kufuata huduma za kijamii.

Walisema, hapo awali walitumia  masaa matatu lakini baada ya kujengwa kwa Bara bara hiyo inayokwenda mkoa jirani wa Tabora  kwa sasa wanatumia muda wa Dk 30 hadi Mpanda mjini ambapo wameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kujenga Bara bara hiyo ambayo ilikuwa changamoto kubwa.

Aman Bondo mbali na kuipongeza Serikali alisema, wameanza kuitumia barabara hiyo kuzalisha kwa wingi na kusafirisha maazao yao kutoka kijijini kufikisha sokoni jambo litakalo chochea maendeleo na uchumi wao.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/33GdMNe
via
logoblog

Thanks for reading ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami mkoani Katavi waleta unafuu wa maisha kwa wananchi

Previous
« Prev Post