Ticker

10/recent/ticker-posts

TRENI YA ZIADA ILIVYOBEBA ABIRIA ZAIDI YA 1000 KWENDA MOSHI,WAZIRI KAMWELWE APEPERUSHA BENDERA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe amepeperusha bendera kuruhusu treni maalumu iliyoandaliwa kutokana na idadi kubwa ya abiria wanaoelekea Moshi kuongezeka katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

Safari hiyo imeanza rasmi katika stesheni ya Kamata jijini Dar es Salaam ambapo imeondoka na jumla ya abiria 950, Desemba 21, 2019.

Waziri Kamwelwe alitumia fursa hiyo kusikiliza maoni na pongezi kutoka kwa abiria waliokuwa ndani ya treni hiyo ya Deluxe ambapo abiria hao  walipata nafasi ya kuishukuru Serikali kupitia Shirika la Reli nchini kwa kurejesha usafiri wa treni ambao kwa takribani miaka 25 iliyopita ilikuwa imesimama kutoa huduma kwa kanda ya kaskazini.

Hata hivyo abiria hao walitoa maoni yao pamoja na kueleza changamoto wanazopata wakati wa safari hasa wakati wa msimu wa sikukuu ambapo uhitaji wa usafiri huongezeka.

Akizungumza na abiria Waziri amewatoa hofu abiria hao kwa kuwaeleza jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha wanatatua swala la upungufu wa mabehewa ya abria “kutokana na ongezeko la abiria, tayari Serikali imeagiza mabehewa 45 mapya kwa ajili ya kutatua changamoro ya msongamano wa abiria wanaotumia reli ya kati” Waziri Kamwelwe alisema.

Kwa upande mwingine Waziri alipongeza Shirika kwa huduma nzuri na za ufanisi ambazo wanaendelea kuzitoa kwa watanzania kupitia usafiri wa treni ambapo watanzania wengi wamevutiwa na kufurahia huduma ambapo imepelekea ndani ya mwezi mmoja tangu izinduliwe mapema mwezi Disemba kusafirisha  jumla ya abiria 6,500 kutoka Dar es Salaam kuelekea Moshi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amemshukuru Waziri Kamwele kwa kuja  kuzindua  tukio hilo la safari ya treni maalumu, lakini pia Ndugu Kadogosa alifafanua juu ya kuwepo taarifa zisizo rasmi kuhusu mgawanyo wa mabehewa ki mkoa

Mkurugenzi Mkuu TRC aliongeza kuwa "sisi kama Shirika la Reli tunahudumia watanzania wote bila kujali hawa ni Moshi, Kigoma ama Mwanza sisi kazi yetu ni kuhudumia watanzania wote bila ubaguzi lakini pia kwa treni za Kigoma iko vilevile tulipunguza safari kwa sababu maalumu ya ukarabati wa njia badala ya mara nne tunaenda safari mara tatu ili kuwapa muda wakandarasi wamalize uboreshaji wa njia kwa wakati,  hivi karibuni tutawatangazia ratiba mpya ya safari na kurejea kama ilivyokuwa zamani mara nne kwa wiki”.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/392dP9Y
via

Post a Comment

0 Comments