TAKUKURU MKOA WA SINGIDA YAMSHIKILIA HAKIMU WA MAHAKAMA YA MWANZO MTINKO KWA TUHUMA ZA KUPOKEA RUSHWA YA 250,000/=

  Masama Blog      
Na Jumbe Ismailly - SINGIDA 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida inamshikilia Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mtinko,katika Halmashauri ya wilaya ya Singida kwa tuhuma za kupokea rushwa ya shilingi 250,000/=kutoka kwa mtoa taarifa ili aweze kutoa upendeleo kwenye kesi ya madai inayomkabili katika Mahakama hiyo.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida,Adili Elinipenda alimtaja Hakimu huyo wa Mahakama ya mwanzo kuwa ni Benard Modest Kasanda na kwamba alitenda kosa hilo dec,16,mwaka huu kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

“Mtuhumiwa Hakimu Kasanda alikamatwa na TAKUKURU Mkoa wa Singida baada ya kupokea kiasi cha shilingi 250,000/= kutoka kwa mtoa taarifa ili aweze kutoa upendeleo kwenye kesi ya madai namba 137/2019”alisisitiza mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Singida.

Aidha Elinipenda alifafanua kwamba mtuhumiwa huyo baada kupokea fedha hizo ndipo alizificha kwenye kasha la dawa ya meno aina ya Wgitedent.

Mkuu huyo wa TAKUKURU hata hivyo aliweka bayana kwamba baada ya kumpekua zaidi mtuhumiwa walifanikiwa kumkuta na kiasi kingine cha fedha cha shilingi 489,100/= pamoja na visu vitano,huku kimoja kikiwa kwenye soksi,vingine vikiwa kwenye droo ya meza yake na kwenye mkoba wake.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa taasisi baada ya tukio hilo,vile vile wananchi wengine wawili waliodai wana mashauri yao mbele ya mtuhumiwa Hakimu Kasanda walijitokeza kwa Takukuru na kusema nao pia walimpatia mtuhumiwa fedha,huku mmoja akidai kutoa shilingi 50,000/= na mwingine shilingi 200,000/=

Hata hivyo Elinipenda alibainisha kuwa Takukuru inaendelea kuchunguza mashauri haya yote na umma utajulishwa baada ya kukamilika,hivyo basi taasisi hiyo inaendelea kuwakumbusha wananchi wote wa Mkoa wa Singida kutoa taarifa za vitendo vya rushwa mara moja ili hatua za kisheria ziweze kuchukulia kwa wakati.
Ni visu alivyokutwanavyo Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Mtinko huku vikiwa ameviweka kwenye soksi za viatu,kwenye droo ya meza na kwenye mkoba wake..(Picha zote Na Jumbe Ismailly)Ni Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Mtinko,Singida vijijini,Benard Modest Kassanda anayeshikiliwa na TAKUKURU Mkoa wa Singida kwa tuhuma za kupokea rushwa ya shsilingi 250,000/= kutoka kwa mtoa taarifa ili aweze kutoa upendeleo kwenye kesi ya madai Na.137/2019.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida,ADILI ELINIPENDA akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu kumkamata Hakimu huyo anayetuhumiwa kwa rushwa ya shilingi 250,000/=


baadhi ya watumishsi wa TAKUKURU Mkoa wa Singida waliohudhuria kikao cha Waandishi wa Habari walipokuwa wakipataiwa taarifa ya kukamatwa kwa Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Mtinko.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/35vVEHC
via
logoblog

Thanks for reading TAKUKURU MKOA WA SINGIDA YAMSHIKILIA HAKIMU WA MAHAKAMA YA MWANZO MTINKO KWA TUHUMA ZA KUPOKEA RUSHWA YA 250,000/=

Previous
« Prev Post