SHIRIKA LA ‘ESTL’ MKOANI SINGIDA LATOA WITO KWA JAMII KUUNGANA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA, UKEKETAJI KWA MTOTO WA KIKE.

  Masama Blog      

 Mratibu wa Mradi maarufu ‘Kick FGM out of Singida kutoka Shirika lisilo la kiserikali la ESTL, Rosemary Mfui akitoa mada mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ya Kata ya Mwankoko, Singida MC jana kuhusu athari za ukatili wa kijinsia na masuala ya ukeketaji.
 Mthamini Mradi wa ‘Kick FGM out of Singida kutoka Shirika lisilo la kiserikali la ESTL, Philbert Swai akiwaeleza wajumbe wa Kamati ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ya Kata ya Mwankoko, Singida MC jana, juu ya hatua mbalimbali za awali za kuchukua endapo mtoto wa kike amebakwa.
 Afisa Mendeleo ya Jamii, Singida MC, akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa kamati ya kata ya kupinga vitendo vya ukatili kata ya Mwankoko, Singida MC jana (hawapo pichani) kuhusiana na matakwa ya Mwongozo uliopo wa Uratibu wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA)
 Wajumbe wa  Kamati ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ya Kata ya Mwankoko, Singida MC wakifuatilia mada mbalimbali zinazowasiliswa na wataalamu wa ESTL (hawapo pichani) kuhusu athari za ukatili wa kijinsia na ukeketaji ndani ya jamii.
 Wajumbe wa  Kamati ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ya Kata ya Mwankoko, Singida MC wakisikiliza mada mbalimbali zinazowasiliswa na wataalamu wa ESTL (hawapo pichani) kuhusu athari za ukatili wa kijinsia na ukeketaji ndani ya jamii.
Picha ya pamoja ya baadhi ya wajumbe wa MTAKUWWA kata ya Mwankoko, Singida MC, na wataalamu wa ESTL, mda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano uliojadili na kuweka mikakati ya namna bora ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike.

Na Dotto Mwaibale,  Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL), limetoa wito kwa watanzania kuungana pamoja katika kukabiliana na vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia kwa mwanamke na mtoto wa kike ikiwemo ukeketaji, ambavyo bado hufanyika kwa siri sana kwa baadhi ya maeneo.
Ifahamike ukeketaji ni aina yoyote ya kutoa kidogo au kutoa kabisa viungo vya nje vya uzazi vya mwanamke au mtoto wa kike bila sababu za kimatibabu. Ukatili wa aina hiyo hupelekea madhara makubwa kwa ustawi wa ukuaji wa mtoto wa kike kiafya, kimwili, kiuchumi na kiakili
Awali, mtindo wa ukeketaji uliokuwa ukitumika ni kumuwahi mtoto tangu akiwa mchanga, lakini kupitia juhudi kubwa za ukaguzi wanaofanyiwa watoto mara kwa mara wanapoletwa zahanati zimewashtua wahalifu wa vitendo hivyo. Sasa mbinu inayotumika kutekeleza uhalifu huo ni kushughulika na wale wenye umri wa kuanzia miaka 5 na kuendelea ambao hawapelekwi tena zahanati.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Kutokomeza Ukatili wa kijinsia, hususan dhidi ya Wanawake na Watoto Kata ya Mwankoko, Singida MC, mkoani hapa jana, Mratibu wa mradi wa Kupinga Ukeketaji na Ukatili wa kijinsia kupitia ESTL maarufu 'Kick FGM Out of Singida,’ chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society, Rosemary Mfui, alisema ukatili huo unachangiwa zaidi na mambo ya kiimani anayoaminishwa mtu, sambamba na mila na desturi zilizopitwa na wakati
"Tatizo la ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji ni changamoto kubwa ndani ya mkoa wa Singida, baadhi ya watu bado wanafanya kwa siri, kitaifa tatizo linaonyesha kupungua lakini kwa mkoa wa Singida tatizo linaongezeka. Nichukue nafasi hii kuwasihi sana viongozi wa kimila, wazazi, viongozi wa dini, Jeshi la Polisi na jamii kwa ujumla tushikamane ili kwa pamoja tuweze kutokomeza vitendo vya ukeketaji kwa watoto wetu hawa wa kike," alisema Mfui
Alisema kinachosikitisha zaidi ukatili huo hufanyika kwa siri sana kwa wahusika kuogopa mkondo wa sheria, hali inayopelekea ugumu wa kubaini vitendo hivyo kutokana na watu walio wa karibu ya mwathirika wa tukio hilo kutoonyesha ushirikiano ipasavyo, na kuendelea kukumbatia na kuzipa hadhi mila potofu na kandamizi ndani ya baadhi ya jamii kwa kuzigeuza kuwa kama ndio sheria halali za kimila
Mfui alibainisha kwamba madhara ya ukeketaji ni mengi, ikiwemo kuweza kusababisha vifo kutokana na mwathirika wa tukio hilo kutokwa na damu nyingi, maambukizo ya magonjwa na hasa UKIMWI kutokana na vifaa vinavyotumika kwa ukeketaji kutokuwa safi na salama, maumivu makali wakati wa kujamiiana na kujifungua, ongezeko la mimba za utotoni na madhara ya kimwili na kisaikolojia
Aidha, akizungumzia kuhusu ukatili wa kijinsia, alisema ni kitendo anachofanyiwa mtu yeyote mwanamke au mwanaume kwa lengo la kumdhuru au kumuumiza kisaikolojia, kimwili, kiafya, kingono au kiuchumi, kitendo kinachohusisha kutishia usalama na uhuru katika maisha ya mtu binafsi au jamii, huku wahanga wakubwa wa ukatili huo wakiwa ni wanawake na watoto wa kike
Kwa upande wake, Afisa Mthamini wa Mradi huo kutoka ESTL, Philbert Swai, pamoja na mambo mengine, alitoa mwongozo wa hatua za kuchukua pindi mwanamke au mtoto wa kike amebakwa au kulatiwa kuwa ni kwanza kuhakikisha anakimbilia sehemu salama.
Swai alisema baada ya hapo mhanga anapaswa kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola na ahakikishe anapewa fomu ya Polisi namba 3, kisha afike zahanati au kituo cha afya ndani ya masaa 72 kwa lengo la kupewa dawa za kuzuia maradhi na mimba.
Aidha, alitahadharisha kuwa kamwe mwathirika baada ya kufanyiwa tukio la ukatili asikubali kuwekwa chini na kufanyiwa vikao vya usuluhishi kutoka kwa yeyote, na aliyebakwa au kulatiwa akumbuke mda wote kuchukua ushahidi
“Usifue nguo, usioge, usichane wala kuosha nywele, na usibadilishe nguo baada ya kitendo cha ubakaji, endapo utabanwa na haja ndogo fanya hivyo kwenye chombo,” alisisitiza Swai
Alisema azma iliyopo kwa ESTL ni kuhakikisha wanatokomeza kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukeketaji ndani ya maeneo yote ya mkoa huo, na hivi karibuni kwa kushirikiana na serikali kupitia Manispaa ya wilaya ya Singida wanatarajia kuendelea kutoa elimu hiyo ya ukatili wa kijinsia na masuala ya ukeketaji kwa makundi tofauti ndani ya jamii
Swai alisema kwa mujibu wa takwimu za kitafiti, mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa mitano kitaifa ambayo masuala hayo ya ukeketaji yameonyesha kushamiri. Takwimu zinaonyesha asilimia 31 ya wanawake wa mkoa huo wamekumbwa na kadhia hiyo, jambo ambalo alisisitiza kuwa jamii inapaswa kukataa hali hiyo na kubadilika
Awali, akifafanua mwongozo wa uratibu wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto 2017/2018-2021/22 (MTAKUWWA), Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Tumaini Sabbi Christopher, alisema lengo la mpango huo ni kukabiliana na changamoto za ulinzi wa wanawake na watoto nchini
Christopher kupitia mwongozo wa mpango huo, alibainisha kwa mujibu wa takwimu za kitafiti zinaonyesha kwamba mwanamke 1 kati ya 5 ametoa taarifa ya kufanyiwa ukatili wa kingono katika maisha yake, msichana 1 kati ya 3 na mvulana 1 kati ya 7 walifanyiwa ukatili wa kingono kabla ya umri wa miaka 18
Katika kutekeleza mpango huo kwa ufanisi, serikali imeandaa mwongozo wa uratibu, usimamizi, na ufuatiliaji. Aidha, mwongozo huo unatoa maelekezo kuhusu uundwaji wa kamati mbalimbali, mfumo wa mawasiliano na uwasilishaji wa taarifa kutoka ngazi ya taifa mpaka kijiji
“Hata hivyo pamoja na uhaba wa rasilimali fedha za kuhudumia kamati zote za mtakuwwa nchi nzima, serikali kwa kushirikiana na wadau mpaka sasa tayari imeandaa sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia (2000), na sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008), kupitishwa kwa Sheria ya Mtoto Na. 21 na kanuni zake,” alisema
Christopher aliongeza kuwa, juhudi nyingine zilizofikiwa ni pamoja na kuanzishwa Dawati la Jinsia kwenye wizara zote, kuanzishwa kwa mifumo ya ulinzi wa mtoto katika halmashauri 63 nchini, kuanzishwa kwa Dawati la Jinsia na Watoto kwenye vituo vya Polisi 417, sambamba na kuanzishwa kwa mahakama za kusimamia kesi za watoto katika halmashauri 131.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/34TCwmj
via
logoblog

Thanks for reading SHIRIKA LA ‘ESTL’ MKOANI SINGIDA LATOA WITO KWA JAMII KUUNGANA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA, UKEKETAJI KWA MTOTO WA KIKE.

Previous
« Prev Post