Ticker

10/recent/ticker-posts

SERIKALI YAAGIZA HOSPITALI ZOTE NCHINI KUANZISHA MFUKO WA FEDHA ZA DAWA.

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- MWANZA

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeagiza Waganga Wakuu wa Vituo vya Afya na Hospitali zote nchini kuanzisha mfuko wa fedha za Dawa kupitia makusanyo ya fedha za ndani, ili kuweza kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa dawa nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu katika kikao cha uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza.

"Kuanzia Vituo vya Afya, Hospitali zote za Halmashauri, za Mikoa , kuanzisha mfuko wa fedha za dawa, na vyanzo vikuu vya mifuko hii ni mapato yatokanayo na mauzo ya dawa, huduma za Maabara, huduma za mionzi" alisema Waziri @umwalimu.

Amesema, Bodi hiyo ya ushauri lengo lake kubwa ni kuhakikisha inaboresha huduma za kinga na tiba katika Hospitali, huku ikihakikisha huduma hizo zinaifikia wananchi kwa ubora na gharama nafua.

Aliendelea kusema, Sera ya Afya nchini inawataka Wananchi kuchangia huduma kwa gharama nafuu isipokuwa kwa makundi yote ya msamaha, wakiwemo Wazee, Watoto walio chini ya miaka mitano na mama wajawazito, hivyo kuwataka kuweka mifumo mizuri ili kurahisisha utoaji huduma.

Mbali na hayo, Waziri Ummy ameiagiza Bodi hiyo kuhakikisha inaboresha huduma za dharura na ajali, ili kuokoa vifo vitokanavyo weza kuepukika kupitia huduma za dharura, keisha kuwashauri kujenga jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) ili kuboresha huduma kwa wananchi.

"Watu wengi wanakufa wakiwa getini Mwa Hospitali, wakati utaalamu upo, kwamba mkiboresha huduma za dharura na ajari, tunaweza kuokoa maisha ya watu wengi " alisema Waziri @umwalimu.

Aidha, Waziri Ummy ameeleza majukumu ya Bodi hiyo ni kushauri, kutengeneza, kusimamia na kupitisha miongozo, malengo na mipango mikakati ya Hospitali kulingana na Sera na miongozo ya Serikali.

Nae Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou-Toure Dkt. Dkt. Graham Mtui ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya katika Hospitali hiyo kwa kuleta mashine ya uchunguzi wa figo na ini, mashine ya kusafisha figo ambazo zinatarajia kuanza kutoa huduma Januari 2020.

Kwa upande mwingine amesema, Hospitali inatarajia kupokea mashine sita ikiwemo CT Scan, X- ray yakidigitali, vifaa vya mifupa na mashine zinazosaidia kupumulia kutoka MSD.

Hata hivyo, amesema kuwa, idadi ya Wagonjwa wanaofika kupata huduma, kutoka wastani wa wagonjwa 350 kwa siku kwa mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa kati ya 500 mpaka 700 kwa Mwaka huu 2019, huku akiweka wazi kupunguza Rufaa za kwenda Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Bugando kwa asilimia 50.

"Kutokana na mafanikio hayo, idadi ya wagonjwa wanaopata huduma katika Hospitali imeongezeka, kutoka wastani wa wagonjwa 350 kwa siku ambayo ilikuwa mwaka 2015, na kufikia wastani wa wagonjwa kati ya 500 hadi 700 kwa mwaka huu 2019", alisema Dkt. Graham Mtui.

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akikata  utepe ikiwa kama ishara ya uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure, Kulia kwake ni Mwenyekiti mpya wa Bodi Prof. Abel Makubi, kushoto kwake ni Kaimu RMO Mkoa Mwanza Dkt. Silas Wambura.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akiteta  jambo na Mwenyekiti mpya wa Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure  Prof. Abel Makubi wakati wa kikao cha kuzindua Bodi hiyo.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akieleza jambo wakati wa kikao cha kuzindua Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure
 Baadhi ya Watumishi wa Hospitali  ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure na Wajumbe wa Bodi ya zamani  ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure, waliofika kushuhudia uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali hiyo, uliofanywa na Waziri wa Afya Mhe.@umwalimu katika ukumbi wa RMO Mkoa wa Mwanza.
 Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu , akiwa na wajumbe wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu na Mwenyekiti mpya wa Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure wakiwa wamebeba kitabu cha mwongozo wa Bodi ya ushauri,  wakati wa kikao cha kuzindua Bodi hiyo.
 Baadhi ya Watumishi wa Hospitali  ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure waliofika kushuhudia uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali hiyo, uliofanywa na Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu katika ukumbi wa RMO Mkoa wa Mwanza.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akimkabidhi mwongozo mmoja kati  ya wajumbe wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure, katikati ni Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Silas Wambura.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2sgJ4x4
via

Post a Comment

0 Comments