Ticker

10/recent/ticker-posts

RC Wangabo asisitiza umoja Kanisa la KKKT Rukwa.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesisitiza umoja na mshikamano kwa waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)ambao kwa majuma kadhaa wamekuwa na mikwaruzano hali iliyofanya waumini hao kuswali kwa mafungu jambo ambalo halileti maendeleo ndani ya kanisa pamoja na mkoa.

Amesema kuwa wakati alipoteuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kuweza kuwasili katika mkoa miongoni mwa viongozi wa dini waliomuombea alikuwa ni Baba Askofu Ambele Mwaipopo ambaye anatambuliwa na serikali na kutahadharisha kuwa endapo serikali inamtambua kuwa ndio kiongozi wa kanisa hilo iweje wanaushirika wasimtambue.

“Mimi niko ndani ya Kanisa, nalitambua Kanisa, namtambua Muasham Baba Askofu, Kanisa hili limesajiliwa, Kanisa la Mungu, Muasham Baba Askofu wakati nilipofika tu hapa Mkoa wa Rukwa, Sumbawanga. Pamoja na viongozi wengine waliofika ofisini wakaniombea, Baba Askofu huyu alikuja akaniombea pia, wewe ni nani usiyemtambua? Mimi niwatake na kuwaomba, wanausharika wote ambao wako nje ya Kanisa warudi ndani ya Kanisa,” Alisema.

Na kuongeza kuwa endapo waumini wakishikana Mungu huwa pamoja na waumini hao na kamwe Mungu hawezi kumfuata mtu asiyependa umoja na kuwahahakikishia kuwa wale wote ambao wapo nje ya Kanisa kuwa Baba Askofu amekwisha wasamehe hivyo wasiwe na sababu ya kuendelea kubaki nje ya Kanisa.

Aidha alisisitiza kuwa umoja kati ya waumini wa madhehebu mbalimbali ndani ya mkoa unachangia kwa kiasi kikubwa umoja wa wanarukwa na hivyo kusababisha mkoa wa Rukwa kusonga mbele kimaendeleo.

Ameyasema hayo katika salamu zake za Krismasi leo 25.12.2019 kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa alizozitoa wakati aliposhiriki ibada ya ya Krismasi katika kanisa la KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika Mkoani Rukwa.

Kwa upande wake Baba Askofu Ambele Mwaipopo alimshukuru Mkuu wa Mkoa huyo kwa kutoa ujumbe mzuri wa mshikamano hasa katika siku ya kusheherekea kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristo na kuwaomba waumini waliohusdhuria ibada hiyo kuzungumza na wale wote waliopo nje ya kanisa hilo ili kuweza kuurudisha umoja na kuweza kupanga mambo ya kimaendeleo.

“Tukumbuke tuna mkakati mzuri kabisa wa kuandikwa wa dayosisi yetu ambayo tulikuwa tunayafanya, tumeweka kipaumbele lakini baada ya mgogoro huu kwakeli kulikuwa na kusimama mahala Fulani lakini Mungu ni mwema hajatuacha ndiomaana shughuli hizi hapa Kanisani zinaendelea na tunashukuru sana kwa kututia moyo Mkuu wa Mkoa kwaajili ya Ujenzi wa Kanisa hili,” Alisema

Aliongeza kuwa pamoja na kuwa Mkuu wa mkoa ni Muumini wa Kanisa la Roma lakini kwa upendo wake na kuguswa na jambo hilo ameona asali pamoja na washirika wa kanisa la KKKT. 
 Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa toleo wakati aliposhiriki Ibada ya Krismas katika Kanisa la KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika Mkoani Rukwa.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akisalimiana na Baba Askofu Ambele Mwaipopo wa KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika Mkoa wa Rukwa muda mfupi baada ya kutoa salamu zake.
 Baba Askofu Ambele Mwaipopo wa KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika Mkoa wa Rukwa 
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (katikati) akishiriki ibada ya Krismas pamoja na Mkewe Mama Veronica Joachim Wangabo (kulia) na Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mkoa wa Rukwa Sadrick Malila.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo pamoja na Baba Askofu Ambele Mwaipopo wa KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika Mkoa wa Rukwa  katika picha ya pamoja na watoto waliohudhuria ibada ya Krismasi.
 


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/35VJ4Bu
via

Post a Comment

0 Comments