Ticker

10/recent/ticker-posts

MINADA YA FORODHA SASA KUFANYIKA KWA NJIA YA MTANDAO

 Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza kusitisha rasmi minada ya hadhara ya forodha iliyokuwa ikifanyika hapo awali na badala yake minada hiyo itakuwa ikifanyika kwa njia ya mtandao kupitia Tovuti ya TRA ambayo ni www.tra.go.tz na tarehe 2 Januari, 2020 kutakuwa na mnada huo utaofanyika kwa njia ya mtandao. 

Na Veronica Kazimoto
Dar es Salaam

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imetangaza kusitisha minada ya hadhara ya forodha iliyokuwa ikifanyika hapo awali na badala yake minada hiyo itakuwa ikifanyika kwa njia ya mtandao kupitia Tovuti ya TRA ambayo ni www.tra.go.tz

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Edwin Mhede amesema kwa mara ya kwanza, mnada kwa njia ya mtandao utafanyika tarehe 2 Januari, 2020 ambapo kutakuwa na ushindani wa haki na taarifa zote za washindi zitaonekana kwa uwazi kwenye tovuti hiyo ya TRA. 

“Napenda kuwataarifu rasmi kuwa, kuanzia sasa mamlaka itafanya minada yote kwa njia ya mtandao na kwa kuanzia tutakuwa na mnada mnamo tarehe 2 Januari, 2020. 

“Hivyo, nachukua fursa hii kuwaalika wananchi wote walioko ndani na nje ya nchi kushiriki mnada huo na ninawakumbusha kuwa, bado wana haki ya kukagua bidhaa kabla ya kununua kwa wale watakaoweza kufika kwenye maeneo bidhaa zilipo”, alisema Dkt. Mhede.

Dkt. Mhede ameyataja mafanikio ambayo TRA inayatarajia kutokana na mfumo huu mpya ambapo amesema ni pamoja na bidhaa nyingi zinatarajiwa kuuzwa kwa wingi na hatimaye makusanyo ya kodi yataongezeka. 

Pia, watanzania wengi wenye nia watapata fursa ya kununua bidhaa bila kuongeza gharama kwa kutumia madalali na wanunuzi watakuwa na muda wa kutosha wa kununua bidhaa hizo huku kukukiwa na ushindani wa haki.

Mafanikio mengine ni kupungua kwa gharama zinazotumiwa na mamlaka kuendesha minada kulinganisha na utaratibu uliokuwepo hapo awali na hivyo kazi hii itafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Kamishna Mkuu Mhede alieleza jinsi ya kushiriki mnada kwa njia ya mtandao ambapo alisema kuwa ni lazima mshiriki awe na kifaa chochote chenye mtandao popote alipo kama vile simu ya mkononi, kompyuta au kompyuta mpakato. 

Vilevile, ni lazima mshiriki awe amejisajili kwenye mfumo na kwa wale wasiokuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) watatakiwa kujisajili kwa kuwasilisha taarifa zao kwenye mfumo ili kupata TIN kwanza.

Baada ya kuingia kwenye tovuti, mshiriki atachagua bidhaa mbalimbali na kuanza kushindana na washiriki wengine kwa kuweka bei na atakuwa na uwezo wa kuongeza bei kadri ushindani utakavyokuwa ukiendelea. 

Aidha, mshiriki atakayekuwa ameshinda atataarifiwa kwenye mfumo na anaweza kupata ankara kwa ajili ya kufanya malipo na hatimaye mshindi atapata hati ya kuruhusu mzigo kutolewa maeneo ya forodha kwa njia hiyo hiyo ya mtandao.

Awali, Kamishna Mkuu huyo Dkt. Edwin Mhede alizitaja changamoto za mnada wa hadhara uliokuwa ukifanyika zamani kwamba, ulikuwa ukifanyika mara moja kwa wiki na hivyo kusababisha bidhaa kutokuuzwa kwa wakati na kupelekea serikali kutokukomboa kodi yake kwa wakati.

Pia, washiriki wa mnada walikuwa ni walewale na wengi wao walikuwa siyo wanunuzi huku wakiingilia minada na kufanya wanunuzi wenye nia kushindwa kununua bidhaa. 

Changamoto nyingine ilikuwa ni ulipaji wa malipo ya awali ya asilimia 25 kwa washindi ulikuwa ukihitaji washindi hao kwenda eneo la mnada na fedha taslimu na kwa wale wanaolipa kwenye akaunti zao iliwalazimu wawe na akaunti ya benki iliyopo kwenye eneo la mnada wakati kwa sasa mshindi hulipia mzigo kupitia kwenye akauti yake kwa kutumia ankara na halazimiki kwenda TRA isipokuwa wakati wa kuchukua mzigo wake tu.

Mamlaka ya Mapato Tanzania imeamua kubadilisha mfumo wa kufanya mnada wa hadhara wa forodha ikiwa ni sehemu ya kuondokana na changamoto zilizokuwepo kabla ya kuanza kwa mfumo wa kielektroniki, kutekeleza Mpango Mkakati wa Tano wa TRA na Mpango Kabambe wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuwa na Serikali Mtandao ambapo Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Serikali zinatakiwa kuendesha shughuli zake hasa za ukusanyaji wa Mapato kwa kutumia mifumo ya kielektroniki.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2ZkX1Gy
via

Post a Comment

0 Comments