Ticker

10/recent/ticker-posts

MENEJIMENT YA TMA YAJIPANGA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Picha pamoja.
 Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mwenyekiti wa kikao hicho, Dkt. Agnes Kijazi akizungumza mbele ya wageni waalikwa mbalimbali kwenye kikao hicho



 Menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imefanya kikao kazi kwa siku mbili ili kupitia kwa pamoja na kupata uelewa wa namna bora ya utekelezaji wa sheria Na. 2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na mwenyekiti wa kikao, Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wakurugenzi na mameneja kujenga utamaduni wa utendaji kazi wenye lengo la uboreshaji huduma ilikufikia malengo ya Mamlaka katika utekelezaji wa sheria iliyopo. 

Aidha, aliwapongeza na kuwashukuru washiriki wa kikao kazi hicho kwa jinsi walivyojitoa kuifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa kwa zaidi ya saa kumi na mbili za kazi kila siku pasipo mtu yoyote kuondoka.

‘Nataka baada ya kikao hiki viongozi wote muwe mstari wa mbele katika kuhakikisha watumishi mnaowasimamia wana fahamu sheria, taratibu na kanuni kwenye utekelezaji wa majukumu yao kwa maslahi ya Mamlaka na Taifa kwa ujumla. Alizungumza Dkt. Kijazi.

Awali, akifungua kikao kazi hicho Dkt. Kijazi aliwapongeza wafanyakazi wote wa TMA kwa utendaji mzuri wa kazi uliopelekea kufanikiwa kukishikilia cheti cha ubora cha ISO 9001:2015 baada ya ukaguzi uliofanyika kati ya tarehe 16 na 20 Disemba, 2019 ambapo TMA ilikaguliwa na Mkaguzi wanje kutoka Canada.

Kikao kazi hicho kiliwakutanisha Mkurugenzi Mkuu, wakurugenzi, Mkurugenzi Ofisi ya Zanzibar, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa- Kigoma, mameneja kutoka makao makuu, mameneja wa Kanda na wanasheria wa TMA. 

Awali, wajumbe walipitia vifungu vyote vya sheria na kujadili kwa kina ili kuhakikisha viongozi wote wa Mamlaka wanakuwa na uelewa wa pamoja wa sheria hiyo ili kurahisisha utekelezaji wake katika maeneo yao ya kazi na hivyo kuchangia katika ustawi wa maendeleo ya nchi kupitia sayansi ya hali ya hewa.

Aidha, wajumbe hao waliainisha maeneo ya uboreshaji katika kanuni hususan kwenye udhibiti wa huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukusanyaji mapato, utoaji huduma za hali ya hewa kwa usahihi na kwa wakati pamoja na kutoa elimu kwa umma na wadau kuhusu sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/37jOdn7
via

Post a Comment

0 Comments