MAKAO MAKUU YA UMOJA WA POSTA AFRIKA KUJENGWA JIJINI ARUSHA

  Masama Blog      

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

BAADA ya kudumu kwa takribani miaka 40 sasa tangu baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atangaze na kutoa eneo la kujenga makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika, Pan African Postal Union (PAPU) hatimaye leo Desemba 23 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Umoja wa Posta Afrika pamoja na kampuni ya ujenzi ya Beijing Construction Company Limited kutoka nchini China wameweka saini makubaliano ya ujenzi wa jengo hilo ambalo litajengwa Jijini Arusha Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo utagharimu zaidi ya shilingi bilioni Shilingi 33 bilioni na litajengwa kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Umoja wa Posta Afrika(PAPU).

Amesema kutokana na umuhimu wa jengo hilo, Serikali ipo chini ya mradi huo na itatoa ushirikiano wa hali ya juu katika kuhakikisha jengo hilo linajengwa kwa ubunifu wa kiwango cha juu na kwa kuanzia Serikali imetangaza kutoa msamaha wa kodi kwa vifaa vya ujenzi kwa mujibu wa Sheria na mkataba.

“Ni mradi wenye hadhi kubwa kwa Taifa na Kimataifa, serikali itasimamia kuhakikisha ujenzi huu unakuwa na ubora na ufanisi mkubwa na unapaswa ukamilike chini ya muda uliopangwa wa miezi thelathini na kwa gharama hiyo iliyopangwa" amesema.

Amesema kuwa atatumia Kofi yake ya uhandisi katika kuhakikisha hakuna ucheleweshwaji kwa aina yoyote na kuiagiza Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kusimamia kazi hiyo kwa kuangaalia maslahi ya nchi na mazingira bora ya kufanyia kazi.

Amebainisha kuwa kwakuwa serikali ipo nyuma ya mradi huo uangalizi utakuwa mkubwa kwakuwa awali ulishindwa kutekelezeka baada ya kuwapo kwa ukwamishaji kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) Mhandisi James Kilaba amesema, mradi huo ulisainiwa tangu Septemba 2016 lakini kulikuwa na vikwazo kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama hali iliyopelekea ucheleweshwaji wa kiutekelezaji.

“Ujenzi wa mradi huu ulikuwa na zengwe nyingi hadi kufikia hatua ya kusaini maana yake tumeweza kushinda vikwazo hivyo vya kisiasa ambavyo tuliwekewa na baadhi ya nchi,” amesema Mhandisi Kilaba.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema kuwa usalama umeimarishwa jijini humo na kwa mwaka 2020 kuanzia Januari 17 hadi 19 maadhimisho ya miaka 40 ya umoja wa Posta Afrika yatafanyika jijini humo na yataambatana na uwekwaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa jengo hilo.

Hafla hiyo ya utiaji wa saini umefanywa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, Mkuu wa Operesheni naTeknolojia wa PAPU, Nathan Mkandawile na mkandarasi kutoka China wa kampuni ya Beijing Contruction Company Limited.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (aliyesimama watatu kulia) akishuhudia utiaji saini wa makubaliano wa Ujenzi wa jengo la makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika litakalojengwa jijini Arusha Tanzania waliosaini mkataba huo ni walioketi; Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) Mhandisi James Kilaba (katikati) Mkuu wa Operesheni naTeknolojia wa PAPU Nathan Mkandawire (Kushoto) na Mkandarasi kutoka kampuni ya Beijing Construction Company Limited (kushoto) leo jijini, Dar es Salaam. 


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/39cCAQI
via
logoblog

Thanks for reading MAKAO MAKUU YA UMOJA WA POSTA AFRIKA KUJENGWA JIJINI ARUSHA

Previous
« Prev Post