Ticker

10/recent/ticker-posts

HASUNGA AZINDUA MASHINE YA KUKOBOA MPUNGA KIJIJINI MKINDO WILAYA YA MVOMERO

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) akikagua mashine kukoboa mpunga katika kijiji cha Mkindo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Jana Tarehe 2 Disemba 2019. 
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizindua mashine ya kukoboa Mpunga katika kijiji cha Mkindo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambayo ni moja ya mashine kubwa nne zilizonunuliwa na kusimikwa kupitia mradi huo, Jana Tarehe 2 Disemba 2019. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro

Serikali imelipongeza Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa-FAO, Serikali ya Venezuela, Halmashauri za Wilaya za Kilosa, Mvomero na Kilombero kwa utekelezaji wa mradi wa ubia wa maendeleo ya mifumo ya uzalishaji endelevu wa mpunga Afrika chini ya jangwa la Sahara.

Pamoja na majukumu mengine mradi huo ulikuwa na majukumu ya kuwafundisha vijana kilimo shadidi cha mpunga ambacho kinatumia mbegu kidogo zenye ubora na maji kidogo huku kikiwahakikishia wakulima mavuno zaidi.

Mradi huo pia ulitoa na kuwafundisha vijana kutumia zana za kilimo zenye kujali masuala ya jinsia, kurahisisha kazi na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) ametoa pongezi kwa taasisi hizo jana tarehe 2 Disemba 2019 wakati akizindua mashine ya kukoboa Mpunga katika kijiji cha Mkindo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambayo ni moja ya mashine kubwa nne zilizonunuliwa na kusimikwa kupitia mradi huo.

Amesema kuwa lengo la serikali kwa kushirikiana na taasisi hizo ni kuhakikisha kuwa wakulima katika eneo hilo wanatunza ubora wa mazao yao na kupunguza upotevu wa mazao yao baada ya mavuno ikiwa pia ni kuyaongezea thamani ili kupata faida zaidi. 

Amesema kuwa Sanjali na jitihada hizo, Wizara ya Kilimo imeanzisha kitengo cha masoko ya mazao ya kilimo ambacho kinahusika na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi kwa mazao mbali mbali yanayozalishwa hapa nchini ili mbegu zitakazozalishwa na kuwa na mafanikio makubwa katika kilimo uweze kuimarisha kipato cha wananchi.

Takwimu zinaonesha kwamba wastani wa kitaifa wa matumizi ya zana bora za kilimo umeongezeka hadi kufikia asilimia 20 kwa matrekta na asilimia 27 kwa wanyama kazi ikilinganishwa na asilimia 14 ya matrekta na asilimia 24 ya wanyama kazi mwaka 2013. 

Amesema kuwa Kutokana na ongezeko hilo, matumizi ya jembe la mkono yamepungua na kufikia asilimia 53 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 62 kwa mwaka 2013. Aidha, kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) Wizara imeendelea kutoa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo. 

Waziri Hasunga amesema kuwa mradi huo umekuwa ukitekeleza kwa vitendo Mkakati wa Kitaifa wa Kuwahusisha Vijana katika Kilimo wa mwaka 2016 pamoja na Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP-II), Sera na Miongozo mbalimbali ya kilimo hapa nchini. 

Alisema kuwa kupitia miongozo hiyo mbalimbali, Wizara ya Kilimo imeendelea kuratibu utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya kilimo hapa nchini kwa kuimarisha huduma za utafiti, upatikanaji na utumiaji wa pembejeo na zana za kilimo, udhibiti wa visumbufu vya mazao, huduma za ugani, uongezaji wa thamani na upatikanaji wa masoko. 

“Nafarijika kutambua kuwa vijana walionufaika na mradi huu pia walipata mafunzo ya kuongeza thamani kwa mavuno yao, ufikiaji na upatikanaji wa masoko ili kuweza kuuza mazao yao kwa faida” Alikaririwa Mhe Hasunga 

Alisisitiza kuwa zao la mpunga ni la pili kwa umuhimu hapa nchini linapokuja suala la chakula likifuatia kwa mahindi ambayo ndio zao kuu la chakula kwa Watanzania wengi. “Kama ilivyo kwa mazao mengine, Serikali imeweka mikakati kadhaa ya kuhakikisha uzalishaji wake unaongezeka. Kwa sasa nchi yetu inazalisha karibu asilimia mia moja ya mahitaji yetu ya mchele kwa mwaka tukiwa ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa mpunga Afrika baada ya Madagascar” Alisema 

Alisema kuwa kukosekana kwa miundombinu dhabiti ya umwagiliaji, zana na teknolojia duni, athari mabadiliko ya tabia nchi pamoja na mbegu zenye ubora hafifu ni miongoni mwa sababu zinazotuzuia tusizalishe zaidi na kwa tija, hivyo serikali imeweka msisitizo madhubuti katika kukabiliana nazo.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/35Ye03O
via

Post a Comment

0 Comments