Ticker

10/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YAIPIGA TAFU HOSPITALI YA MJI WA MBULU

Na Woinde Shizza, Globu ya Jamii.

Hospitali ya mji wa Mbulu Mkoani Manyara inayokabiliwa na uchakavu wa miundombinu ikiwemo majengo,samani na upungufu wa vifaaa kutokana na hospitali hiyo kujengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita hivyo kusababisha usumbufu kwa wagonjwa wanaotumia hospitali hiyo.

Licha ya serikali kuanza uboreshaji wa miundombinu kwa kukarabati majengo ya hospitali  hiyo baadhi ya wadau wameanza kujitokeza kuunga mkono jitihada hizo kuhakikisha ukarabati huo  unaenda sambamba na uwekaji wa vifaa ikiwemo vitanda na magodoro, ambapo benki ya CRDB kupitia tawi la Mbulu katika kurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii imetoa msaada wa vitanda vitano na magodoro vya wagonjwa kwa ajili ya hospitali hiyo na mabati sitini kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi.

Akikabidhi msaada huo kwa mkuu wa wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga, katika hafla iliyofanyika kwenye hospitali ya mji wa Mbulu, Meneja wa benki ya CRDB kanda ya kaskazini, Chiku Issa amesema benki hiyo inatambua kuwa vitanda ni nyenzo muhimu sana katika utoaji wa huduma za afya lakini pia mabati katika kuboresha miundombinu ya utoaji huduma nchini kote.
Alisema aliposikia kuwa halmashauri ya mji wa Mbulu ina uhitaji wa vitanda na mabati ili kuboresha huduma za afya  hawakusita kama benki kuunga mkono ombi hilo kuwezesha katika kufanikisha jitihada hizo.

“Benki ya CRDB ni muumini mkubwa wa falsafa ya kusaidia jamii ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma juhudi za maendeleo yaani kurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii hivyo imepelekea benki kujiwekea sera maalum ya kusaidia jamii yenye kuagiza na kuelekeza kutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka ili ziende katika shughuli za kusaidia jamii katika Nyanja mbalimbali”alisema Chiku.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mbulu Chelestino Mofuga aliishukuru benki ya CRDB kwa msaada huo ambao amesema umekuja kwa wakati na utasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa vitanda na magadoro iliyokuwa ikiwakabili hospitalini hapo ambapo wakati mwingine kulazimu wagonjwa wanapozidi kulala zaidi ya mtu mmoja lakini pia msaada wa mabati utasaidia kuboresha sekta ya elimu.

“Hili ni tukio muhimu sana kwa maana msaada huu  unatimiza falsafa yenu ya ulipo tupo huu ndio utekelezaji wa kusogea kwa wale wadau wenu muhimu na kuweza kuwachangia kile kitu cha ziada kinachotokana na biashara yenu”alisema Mofuga

Awali Kaimu mganga mfawidhi hospital ya mji wa Mbulu daktari Charles Shija alisema msaada huo utawapunguzia kazi wao kama watumishi kwa kuwa walikuwa wakabiliwa na upungufu wa vitanda ishirini na mbili hivyo kusababisha wagonjwa wanapofurika kuwalazimu kulala Zaidi ya mmoja jambo ambalo amesema si salama kwa afya za wagonjwa.  

Alisema Hospitali hiyo bado inakabiliwa na upungufu wa vitanda na magodoro 17 ambapo endapo vitapatikana vitasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa haswa kina mama wanapokuja kujifungua ambao wakati mwingine wanalazimika kulala watatu kwenye kitanda kimoja pamoja na watoto wao.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2Yle7UB
via

Post a Comment

0 Comments