Ticker

10/recent/ticker-posts

AGIZO LA WAZIRI KALEMANI KUPELEKA UMEME KABUKOME LAAMSHA NDEREMO

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akikabidhi vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wa kijiji cha Kabukome, wilayani Biharamulo, Mkoa wa Kagera, alipokuwa katika ziara ya kazi, Desemba 5, 2019.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kabukome, wilayani Biharamulo, Mkoa wa Kagera, akiwa katika ziara ya kazi, Desemba 5, 2019.
Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambao waliambatana na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), katika ziara yake kijijini Kabukome, Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera, Desemba 5, 2019 wakiwa wamesimama mbele ya wananchi kwa ajili ya utambulisho.

Veronica Simba – Biharamulo

Wananchi wa kijiji cha Kabukome, Kata ya Nyalubungo, wilayani Biharamulo, Mkoa wa Kagera, wameruka kwa nderemo na vifijo, wakifurahia maagizo aliyoyatoa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani Desemba 5, 2019, kuwa kijiji hicho kiwe kimewashiwa umeme ifikapo Januari 30 mwakani.

Waziri alitoa maagizo hayo mbele ya umati wa wananchi wa kijiji hicho, kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme vijijini wilayani Biharamulo.

“Leo ni tarehe 5 Desemba; Nataka kuona ikifika tarehe 20 mwezi huu, nguzo ziwe zimeshaanza kusimikwa hapa Kabukome, na tarehe 2 Januari, zianze kupelekwa kijiji cha Lusabya,” aliagiza Waziri.

Akieleza kuhusu mpango wa upelekaji umeme katika vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo, Dkt Kalemani alisema, vijiji hivyo viwili ambavyo ndivyo pekee havijapata umeme kati ya sita vya kata husika; havikuwa kwenye mpango wa awamu ya kwanza ya uunganishaji umeme vijijini na kwamba viko katika awamu ya pili inayotarajiwa kuanza Aprili, 2020.

“Lakini kwa kutambua shauku kubwa ya umeme mliyonayo wananchi wa Kabukome na Lusabya,  serikali imeamua kuwawahishia huduma hiyo muhimu, ili nanyi mnufaike kama wananchi wengine walio na umeme.”

Vilevile, Waziri aliwataka TANESCO kuanzisha ofisi ndogo eneo hilo mahsusi kwa wananchi kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ili kuwaepusha na usumbufu wa kusafiri mwendo mrefu kufuata huduma hiyo.

Aidha, aliwahamasisha wananchi kuanza mara moja maandalizi ya kuunganishiwa umeme kwa kusuka mfumo wa nyaya (wiring) katika makazi yao pamoja na majengo mbalimbali ya taasisi za umma zikiwemo shule, nyumba za ibada na vituo vya afya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi mbalimbali wa kijiji hicho, akiwemo mwenyekiti wake, Kisabo Dominic, walipongeza kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya tano, chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli, kuhakikisha wananchi wanyonge wanafikiwa na huduma mbalimbali za kimaendeleo hususan nishati ya umeme.

Pia, walimpongeza Waziri Kalemani pamoja na watendaji wengine wote wa wizara kwa uchapakazi wake na ushirikiano ambao wamekuwa wakitoa kwa wananchi.

Takwimu zinaonesha kuwa, hadi sasa vijiji 51 kati ya 74 vya Wilaya ya Biharamulo vimekwishaunganishiwa umeme.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2qq7Lqd
via

Post a Comment

0 Comments