WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA CHUO CHA MAFUNZO YA UFUNDI CHA MKOA WA KAGERA

  Masama Blog      
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezindua ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera na kusema kuwa ujenzi wa chuo hicho ni muendelezo wa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kunakuwa na Vyuo vya ufundi stadi vya Mikoa na Wilaya.

Akizindua ujenzi wa chuo hicho mkoani Kagera Waziri Ndalichako amesema  chuo hicho  kinajengwa  na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kutokana na uhusiano mzuri wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na Nchi hiyo na kwamba ujenzi utakapokamilika vijana wengi wa kitanzania watapata fursa ya kusoma katika chuo hicho na kupata ujuzi katika fani mbalimbali zitakazo fundishwa.

"Kama nilivyosema Tanzania na China ni marafiki na rafiki yako anaangalia mahitaji yako, waswahili husema akufaaye kwa dhiki ndio rafiki wa kweli. China imeona Tanzania inajenga uchumi wa Viwanda ikiwa ni azma ya serikali ya awamu ya Tano  nao wakaamua watuunge mkono katika ujenzi wa Chuo cha Ufundi stadi ili kuandaa vijana wenye ujuzi watakaofanya kazi katika viwanda.

Nikuombe Balozi  tufikishie shukrani zetu za dhati kwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa msaada huu mkubwa na wa kihistoria ," Amesema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema ujio wa mradi huo utaongeza ajira kwa vijana wa kitanzania kwa kuwa wazawa 400 wataajiriwa katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kupata  ujuzi  kulingana na kazi watakazokuwa wakizitekeleza.

"Vijana watakaofanya kazi eneo la mradi pamoja na kufanya kazi  watapata na mafunzo, kwa hiyo ujuzi wao wa kiufundi utaimarishwa kupitia kazi ambazo watakuwa wakifanya katika mradi," Amesema waziri Ndalichako.

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameitaka Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA kupitia upya fani zilizopangwa kutolewa katika chuo hicho ili ziendane na Mazingira halisi ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.

"Nimepitia fani ambazo zimeanishwa kutolewa katika chuo hiki pindi kitakapokamilika, nikiangalia eneo ambalo chuo kinajengwa ni eneo la ziwa na watu wa Kagera au wazazi wa hapa ni wavuvi lakini sijaona kozi ya uvuvi sasa tunawaletea mambo ya uchomeleaji, ufundi bomba, useremala, upakaji rangi kwenye bahari, nilitegemea kuwe na fani ya uvuvi pia
 tuweke fani zinazoendana na mazingira," Amesema Waziri Ndalichako

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania Balozi WANG Ke amesema Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania amezingatia maboresho ya sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuwaongoza watanzania kuelekea dira ya  maendeleo 2025 hivyo China iko tayari kuchangia maendeleo katika sekta ya elimu ili kufikia malengo ya elimu ambayo serikali ya tanzania imejiwekea. 

Nae Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco Gaguti  amewataka wanakagera hasa vijana kushiriki vizuri katika kazi za ujenzi zitakazofanyika katika mradi huo  ili kupata ujuzi wa ufundi ambao utawasaidia kushirikia katika kazi za ujenzi zitakazojitokeza katika Mkoa wa Kagera mara baada ya mradi kukamilika. 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi   VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema Chuo hicho kinajengwa katika eneo lililotolewa na wananchi wa kijiji cha Burugo wilayani Bukoba na lina ukubwa wa hekta 40. 5 sawa na hekari 100.

Dkt. Bujulu amesema Chuo hicho pindi kitakapokamilika kitatoa fani za useremala, uchomeleaji, upakaji rangi, ufundi bomba na kitachukua wanafunzi 800 wa kozi ndefu na 2000 wa kozi fupi

Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Mkoa wa Kagera kinajengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China  kwa gharama za fedha za kitanzania sh bilioni 19.4  ambapo ujenzi wake utachukua miezi 18

Gharama hizo zinajumuisha usanifu, upembuzi yakinifu na ujenzi mpaka ukamilike.
Waziri wa Elimu, Sayansi  na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizindua kuanza kwa ujenzi wa Chuo cha  Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha mkoa wa Kagera, mkoani Kagera.

 Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo cha ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi waliohudhuria uzinduzi wa ujenzi wa chuo cha VETA  cha Mkoa wa Kagera wakifuatilia hotuba ya waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.
 Balozi wa China nchini Tanzania WANG Ke akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi  Stadi na Huduma Cha Mkoa wa Kagera.
 Waziri wa Elimu, Sayansi  na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ujenzi wa Chuo cha mafunzo ya Ufundi Stadi na  Huduma  cha Mkoa wa Kagera.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2q1JeHP
via
logoblog

Thanks for reading WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA CHUO CHA MAFUNZO YA UFUNDI CHA MKOA WA KAGERA

Previous
« Prev Post