Ticker

10/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AZINDUA WIKI YA AZAKI, AWATAKA KUENDELEA KUHUDUMIA WANANCHI

Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imesema inathamini kazi kubwa inayofanywa na Asasi za Kiraia nchini (Azaki) hasa katika kuwahudumia wananchi kwenye sekta mbalimbali katika kuwaletea maendeleo.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa wakati akizindua wiki ya Azaki ambayo inashirikisha zaidi ya Asasi za kiraia zipatazo 500 na Taasisi 100 kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Mhe Waziri Mkuu amesema ni ukweli usiopingika kuwa Asasi za Kiraia zimekua na ushirikiano mkubwa na Serikali ya awamu ya tano katika kuwahudumia wananchi na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo ambao umekua na tija na manufaa kwa jamii.

Amesema Asasi za Kiraia zimekua mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali kwenye vita dhidi ya ukatili wa kijinsia, mila potofu ikiwemo kupigania upatikanaji wa elimu kwa watoto wa kike 

" Serikali yetu chini ya Rais Dk John Magufuli kwa hakika itaendeleza ushirikiano na Azaki katika kuwatumikia wananchi wetu, tunafahamu namna ambavyo mmekua mstari wa mbele katika kuwahudumia wananchi wetu.

Tunafahamu mmekua mkitoa elimu kwa viongozi wetu hasa katika eneo la utawala bora lakini pia mmekua mkiwahudumia wananchi wetu kwenye sekta ya elimu, afya na hata kiuchumi kwa kuanzisha mikopo ambayo imekua na manufaa makubwa katika kukuza vipato vyao," Amesema Mhe Waziri Mkuu.

Amezitaka Azaki kuendelea kuiunga mkono Serikali katika vita dhidi ya rushwa, ubadhirifu kwenye mali za umma na nidhamu katika utendaji na kuwaasa kutumia fedha wanazopata kwa wahisani kufanya miradi ambayo ina taji kwa jamii.

Amesema ili kuendana na kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema "Ubia kwa maendeleo, ushirikiano kama nguzo ya maendeleo nchini" ni muhimu Azaki kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo yote hasa wale wa kijijini.

Pia Mhe Waziri Mkuu amezitaka Azaki kuhamasisha wananchi kuchagua viongozi bora wenye uzalendo ambao watashirikiana na Asasi hizo katika kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.

Kwa wa upande wake Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo amesema kuwa ushirikiano baina ya serikali na Azaki utaendelea kwaajili ya kuleta maendeleo ya Tanzania.

“Asasi zimesaidia kutoa elimu kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa hivyo wao wanabaki kuwa ni watu muhimu katika Taifa hili,” Amesema.

Naye Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee na Watoto, Mhe Ummy Mwalimu amesema kuwa wapo tayari kama Wizara kukaa pamoja na kutatua changamoto wanazokumbana nazo Azaki.

Rais wa Foundation Civil for Society (FCS), Stigmata Tenga alisema kuwa kuna changamoto mbalimbali wanazo kumbana nazo ikiwemo kuwepo kwa ugumu kwa taasisi na mamlaka za serikali kutaka kuonyesha vibali hali inayosababisha miradi kuchelewa au kutofanyika kabisa.

“ Pia bado kuna changamoto ya kuaminiana kwani ili dhana iwe kweli ni lazima kuaminiana,kwani asasi zinafanya kazi kwa maendeleo ya taifa hivyo wanaomba waaminiwe ili kazi zilete tija zaidi,”Amesema Tenga.
Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria kufungua rasmi wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) jijini Dodoma leo. Kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe Ummy Mwalimu na kulia ni Francis Kiwanga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa FCS. 
Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa akizungumza na wadau wa maendeleo na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika ufunguzi wa wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo. 
 Wananchi jijini Dodoma waliojitokeza katika wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) wakimsikiliza mgeni rasmi, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa jijini Dodoma leo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe Ummy Mwalimu akizungumza katika ufunguzi wa wiki ya Azaki uliofanyika leo jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi akiongoza wadau mbalimbali na washiriki wa Azaki katika matembezi ya amani kutoka katika viwanja vya Nyerere kwenda uwanja wa Jamhuri ikiwa ni kuashiria kuanza kwa wiki ya Azaki jijini Dodoma leo.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/33g1njr
via

Post a Comment

0 Comments