Ticker

10/recent/ticker-posts

WATAFITI WATAKA USAWA WA KIJINSIA KWENYE UTAFITI


WASAYANSI watafiti wanaoshiriki mkutano wa mwaka wa Baraza la Sayansi Kanda ya Afrika wamezitaka nchi zao, kuhakikisha zinakuwa na Sheria na Sera ambazo zitawezesha wanawake watalaam kushiriki katika utafiti ili kuwepo usawa wa kijinsia.

Hayo yamsemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Profesa Muhammed Sheikh wakati akitoa taarifa ya mkutano huo ambao umeshamalizika.

Prof. Sheikh alisema takwimu zinaonesha uwiano kati ya wanaume na wanawake kwenye kufanya utafiti haulingani hivyo Serikali za Afrika zinapaswa kuweka mfumo ambao utarahisha usawa kisheria na kisera.

"Tumejadiliana na asilimia kubwa hoja ya ushiriki wa wanawake katika utafiti imechukua nafasi kubwa kwani takwimu zinaonesha karibu nchi zote ushiriki upo chini hivyo njia rahisi ni kuwepo mifumo ya kisheria na kisera ambayo itapendelea kundi la wanawake.

 Ili kufikia huko ni muhimu taasisi za utafiti zinakuwa na ushirikiano kikazi kwa kuwawezesha wanawake wanasayansi kufanya utafiti kama walivyo wanaume," alisema.Sheikh alisema wasayansi hao wanaamini iwapo kundi hilo litapewa msukumo dhana ya usawa wa kijinsi itaonekana na kuondoa malalamiko.

Aidha, alisema wanataaluma hao wamejadili namna ya kuwawezesha watafiti wanaoibukia fedha za kufanyia utafiti ili iwe rahisi kuwaingiza kwenye mfumo kitafiti ulio bora.

Alisema Tanzania kupitia COSTECH na nchi ya Sweden imekuwa ikiwezesha watafiti wanaochipukia kuanzia mwaka 2015 programu ambayo imeonesha matokeo chanya.

"Karibu Euro 900,000 zimeweza kutumika kuwezesha watafiti wapya hivyo ni jukumu la wenzetu kuchukua mfumo huu na kuupeleka kwao,” alisema.
Aidham alisema kupitia mkutano wamekutana na Baraza la Utafiti la Norway na kubadilishana uzoefu katika shughuli za utafiti.

Mtafiti kutoka Taasisi ya Taifa ya Sayansi nchini Marekani, Makyba Charles alisema nchini kwao wamekuwa wakizingatia jinsia kwenye utafiti kwa kuwepo vipengele vya sheria na sera.Charles alisema nchini Marekani sheria na sera zinaelekeza taasisi za utafiti kuzingatia usawa wa kijinsi hivyo ameshauri nchi za Afrika kuzingatia hilo.

Alisema nchini Marekani iwapo kutatokea unyanyasaji wa kijinsia sheria zinaelekeza tukio hilo liripotiwe ndani ya siku 10 ili hatua zichukuliwe.

Mtafiti Mwandamizi wa COSTECH, Hildegalda Mushi alisema washiriki wamependekeza changamoto zote ambazo zinarudisha nyuma watafiti wanawake zipatiwe ufumbuzi."Muda mwingi ulitumika kujadili namna ya kuwezesha kundi letu la wanawake kuhakikisha linaambukizwa chachu ya kufanya utafiti kama walivyo wanaume," alisema.

Alisema washiriki walisema ili kundi hilo liweze kuwa shindani linahitaji kujengewa uwezo kuanzia elimu ya msingi hadi vyuoni ambapo takwimu zinaonesha ushiriki wao umeshuka.Mushi alisema pia wamekubaliana kila nchi shiriki kukusanya takwimu za ushiriki wanawake kwenye utafiti ili kuwa na taarifa sahihi.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia, Sera na Ubunifu Afrika (ATPS), Nicholas Ozor alisema pamoja na uwezeshwaji wanawake na watafiti wanaochipukia juhudi kubwa zinapaswa kuelekezwa kwenye utafiti ulio wazi.

Ozor alisema ulimwengu wa leo unahitaji  ushirikiano katika kila jambo hivyo iwapo mfumo wa utafiti wa kisayansi uliowazi ukipata nafasi kutakuwa na matokeo chanya."Sisi ATPS tunaamini katika utafiti uliowazi kama njia ya kuendeleza jinsia na watafiti wanaochipukia tunachopigania ni uwepo wa miundombinu rafiki katika kitekeleza adhma hiyo," alisema.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/33YR2sQ
via

Post a Comment

0 Comments