Ticker

10/recent/ticker-posts

WATAALAM FIZIOTHERAPIA WAKUTANA MLOGANZILA

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Sara Maongezi akifungua kongamano la kitaifa la wafiziotherapia nchini.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi (Kulia) akizungumza katika kongamano la wafiziotherapia linalofanyika katika Hospitali ya Mloganzila, kushoto ni Dkt. Sara Maongezi.
Rais wa Chama cha Kitaaluma cha Wafiziotherapia Tanzania (APTA), Bi. Remla Shirima akisoma risala wakati wa Kongamano la Wafiziotherapia linalolenga kuangalia maendeleo ya taaluma hiyo nchini.
Wataalam wa Fiziotherapia wakisikiliza hotuba mbalimbali zilizotolewa katika mkutano huo.
Dkt. Sara Maongezi na Dkt. Julieth Magandi wakiwa katika picha ya pamoja na wafiziotherapia mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa mwaka wa wataalam hao.

…………………..

Wataalam wa Fiziotherapia wamekutana katika kongamano la kitaifa la taaluma ya tiba kwa vitendo lengo likiwa ni kuangalia maendeleo ya taaluma hiyo nchini.

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo uliofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Sara Maongezi amesema kuwa Wizara ya Afya inazitambua kisheria huduma zinazotolewa na wafiziotherapia nchini.

“Huduma ya tiba kwa vitendo na wanataalauma wake wanatambuliwa rasmi na sheria ya kusimamia huduma na watoa huduma wa taaluma katika sheria mpya ya madaktari, madakari wa meno na huduma shirikishi ya 2017 (Medical, Dental and Allied Health Professionals Act 2017),” Amesema Dkt. Maongezi.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mloganzila Dkt. Julieth Magandi ametaja kuwa hospitali ina jumla ya vitanda 608 ambapo kwa siku inahudumia wagonjwa wa nje 400 hadi 450, na wagonjwa wa ndani takribani 300 ikiwa ni pamoja na kufanya upasuaji kwa wagonjwa 200 hadi 300 kwa mwezi.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Kitaaluma cha Wafiziotherapia Tanzania, Bi. Remla Shirima ametaja moja kati ya changamoto ambayo taaluma hiyo inapata ni kukosekana kwa vyuo vinavyotoa shahada ya taaluma ya tiba kwa njia ya vitendo ambapo hadi sasa vyuo vingi hapa nchini vinatoa elimu hiyo kwa ngazi ya stashahada tu.

“Tunaiomba Serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ianzishe vyuo vinavyotoa shahada ya tiba kwa njia ya vitendo kutokana na idadi ya wataalam hawa kuwa wachache, ambapo hadi sasa wapo takribani wataalam 400 nchini na kati ya hao 182 tu ndio wanaofanyakazi kwenye taasisi za Serikali kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mapema mwaka huu,” Amesema Shirima.

Kongamano limejumuisha washiriki wanaotoka sehemu mbalimbali nchini ikiwamo wataalam kutoka MNH, Chuo cha Fiziotherapia KCMC, Benki ya NMB, Wawakilishi kutoka Chuo cha Fiziotherapia SOMT nchini Netherlands, Bodi ya Usajili wa Hospitali Binafsi za Afya nchini (PHAB), Taasisi za Hospitali Binafsi (APHTA), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Wawakilishi wa vyama mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, Kamati tendaji ya Chama cha Kitaaluma cha Wafiziotherapia Tanzania (APTA), Dawati la utengamao-Wizara ya Afya na Baraza la Habari Tanzania (MCT).



from MICHUZI BLOG https://ift.tt/37lqwvF
via

Post a Comment

0 Comments