Ticker

10/recent/ticker-posts

WANAFUNZI KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE WAKUMBUSHWA KUZINGATIA MASOMO, NIDHAMU


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MKUU wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Profesa. Shadrack Mwakalila amewataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo 2019/20  kuhakikisha wanazingatia kile kilichowapeleka chuoni hapo kuwa ni kusoma na kufanya vizuri katika mitihani yao na si vinginevyo.

Prof. Mwakalila ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanafunzi wanaosomea cheti, dipoloma na wale wa digrii ambapo kwa ujumla amewataka wanafunzi hao  kujiepusha  na vitendo vyote vinavyoashiria ubaguzi, masuala ya kisasa, kuhakikisha wanakuwa na nidhamu pamoja na kuwa na matumizi mazuri ya muda ili kufikia malengo wanayokusudia.

Taarifa ya Kitengo Cha Habari na Mawasiliano cha  Chuo Cha KumbuKumbu ya Mwalimu Nyerere imesema Prof. Mwakalila amesema lengo la kuzungumza na wanafunzi hao kwanza kuwapongeza kwa kuchaguliwa katika Chuo hicho kikongwe Cha Mwalimu Nyerere chenye  historia kubwa na kilichobeba jina  Muasisi wa Taifa letu.

"Hivyo hakikisheni kile kilichowaleta hapa kitaaluma mnakifanikisha ikiwa ni pamoja na kusoma kwa bidii na maarifa na kumtanguliza Mungu mbele, mambo ambayo hayana msingi achaneni nayo,"amesema Prof. Mwakalila.

"Msipoteze malengo ambayo yamewaleta hapa, mmekuja kusoma zingatieni hilo na wala msijiingize kwenye mambo ambayo yatawapotezea muda, na mnapopata changamoto mbalimbali basi viongozi wa Chuo tupo na hata Serikali ya Wanafunzi ipo kwa ajili ya kusikiliza na kupatia ufumbuzi changamoto hizoo,"amesema Prof. Mwakalila.

Mkuu huyo wa Chuo  amesema  Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kina historia iliyotukuka, kina jina kubwa, vijana wengi wanamsoma tu Baba wa Taifa kwenye vitabu lakini ni mtu muhimu sana kwa Taifa letu.

Amesema muasisi wa Chuo Cha Mwalimu Nyerere  ni Rais wa Kwanza wa Taifa hili ambaye ni hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo  mawazo  ya kujenga Chuo kwa ajili ya wazalendo yalianza mwaka 1958 ambapo Chuo kilifunguliwa rasmi Julai 29, mwaka 1961, hivyo Chuo hiki ni kikongwe.

Prof. Mwakalila ameongeza lengo la Chuo wakati kinaanzishwa ilikuwa ni  kwa ajili ya  kuandaa viongozi wazalendo ambao lazima waandaliwe, ili kwenda kuongoza nchi, hivyo amewahakikishia wanafunzi kuwa wapo kwenye Chuo ambacho kitawajenga kimaadili na kizalendo kwa ajili ya kuwa viongozi wazuri wa baadae.
 Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalim Nyerere jijini Dar es Salaam Profesa Shadrack Mwakalila akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo hicho ambapo amesisitiza nidhamu na kusimamia elimu ambayo imepeleka hapo

Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere wakifuatilia hotuba ya mkuu wa Chuo hicho Profesa Shadrack Mwakalila hayupo pichani wakati anazungumzia nao chuoni hapo


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2WY2pya
via

Post a Comment

0 Comments