Ticker

10/recent/ticker-posts

WALIJUWA GWIJI LA TAARABU SITI BINTI SAAD?

Na Moshy Kiyungi,Tabora.

Histoiria ya muziki wa taarab haiwezi kukamilika iwapi hautalizungumzia jina la Siti binti Saad.

Mama huyo alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha kuimba, wakati alipokuwa akiimba, sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali maili nyingi.

Ilifikia kipindi cha sherehe yeyote ilishindwa kufana kama Siti binti Saadi hakuwepo jukwaani kutumbuiza.

Alikuwa Mzazibari aliyezaliwa katika kijiji cha Fumba huko Kisiwani Zanzibar mwaka 1880.

Siti mara baada ya kuzaliwa alipewa jina la 'Mtumwa'. Hiyo ilikuwa ni desturi ya kawaida kwa kuwa alizaliwa katika kipindi cha Utumwa wa Kiarabu, waliokuwa wakitala visiwa hivyo.

Siku zilivyokuwa zikiendelea, alitokea Kabaila mmoja wa Kiarabu wakati huo, akampa jina hilo la Siti.

Baba yake Bwana Saad, alikuwa ni wa kabila la Kinyamwezi kutoka mkoa wa Tabora, wakati mama yake alikuwa ni Mzigua toka mkoani Tanga.

Wazazi wote hao walizaliwa Zanzibar. Maisha ya familia yao ilikuwa ni duni sana, kwani walijishughulisha zaidi katika kilimo na ufinyanzi. Kazi hizo zote Siti aliweza kujifunza na kuzimudu vizuri mno.

Kama waswahili wasemavyo “kulala masikini, kuamka tajiri” Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha uimbaji.

Kupitia kipaji hicho kilimsaidia sana tangu siku za awali za maisha yake. Alitumia uimbaji wake wakati akiuza vyungu vya mama yake alivyokuwa akimsaidia kuvitembeza mitaani huku akiimba.

Yaelezwa kwamba Siti alipokuwa akiimba, sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali maili nyingi. Hiyo ndio ilikuwa ishara ya watu kujua kwamba vyungu vya kina Mtumwa vinapita leo.

Alifananishwa kuwa ana mapafu yenye nguvu kama ya Simba, kutokana na awezo wa kupaza sauti yake mbali bila kuachia pumzi.

Wakati huo elimu kwa watoto wa kike haikutiliwa mkazo, Siti hakuwahi kwenda shule wala kuhudhuria mafunzo ya Koraani.

Mnamo mwaka 1911, aliona ni bora ahamie mjini Unguja akitokea kijiji cha Fumba, ili kubooresha maisha yake zaidi.

Siti mara baada ya kuingia mjini humo, ilikuwa ni neema kwani alikutana na Bwana mmoja aliyeitwa Muhsin Ali wa kundi la muziki wa taarabu la ‘Nadi Ikhwani Safaa’.

Katika kipindi hicho kundi hilo ndilo lilikuwa pekee la muziki wa taarab, lililoanzishwa na Sultani wa wakati huo Seyyid Barghash Said, aliyekuwa akipenda starehe na anasa.

‘Nadi Ikhwani Safaa’ lilikuwa ni la wanaume peke yake, wanawake hawakuruhusiwa kujiunga na vikundi vya muziki kwa vile ilikuwa ikichukuliwa kama ni uhuni.

Lakini Bwana Muhsin alikiona kipaji cha pekee cha Bi. Siti, akajitolea kumfundisha kuimba kwa kufuata mirindimo ya vyombo vya muziki, akaanza kuimba kwa lugha ya Kiarabu.

Baada ya hapo alikwenda kumtambulisha kwa wanamuziki wenzie wa ‘Nadi Ikhwani Safaa’, ambao bila kusita wakaanza kufanya naye maonesho mbalimbali katika jamii.

Kundi hilo lilipata mialiko mingi kwenda kutumbuiza hususan kutoka kwa Sultan Seyyid Barghash Said na matajiri wengine wa Kiarabu, katika harusi na sherehe zingine mbalimbali Kisiwani humo.

Siti alikuwa mithiri ya ‘moto’ wa kuotea mbali, jina lake likavuma kwa haraka sana hadi nje ya mipaka ya nchi na Bara la Afrika.

Punde Siti alianza kufananishwa na mwimbaji mahiri wa kike aliyetamba wakati huo kutoka nchi ya Misri, Umm Kulthum.

‘Moto’ wa Siti haukuwa wa kuusogelea karibu, kwani 1928 Kampuni ya kurekodi muziki ya Columbia and His Master's Voice, yenye makazi yake huko Mumbai nchini India, ilisikia umaarufu wa Siti binti Saadi.

Hivyo ikaliaki kundi la Nadi Ikhwani Safaa, akiwemo yeye kwenda kurekodi nyimbo kwa lugha adhimu ya Kiswahili, kujaribu kama muziki wake utauzika.

Kampuni hiyo haikuweza kuamini jinsi muziki ule ulivyo pata soko kwa kasi kubwa. Wastani wa santuri 900, ziliweza kuuzika katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo. Hadi kufikia mwaka 1931, santuri 72,000 zilikuwa tayari zimeuzwa.

Kutokana na kusambaa kwa santuri hizo, umaarufu wa Siti ulizidi kuongezeka mara dufu. Watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia walikuwa wakienda Zanzibar kumshuhudia.

Mambo yalizidi kuwa mazuri kwa Siti hadi ikafikia hatua Kampuni ya kurekodi ya Columbia, ikaamua kujenga studio maalum ya kurekodi muziki kwa ajili ya Siti binti Saadi hapo hapo mjini Zanzibar.

Hatua hiyo ya kujengewa studio watu wenye wivu, waliwaumizwa mno, wakaanza kumtungia nyimbo za kumkejeri, ili kumpunguzia kasi hasa walitumia kigezo kwamba hakuwa na uzuri wa sura!

Siti bint Saadi alitunga na kuimba nyimbo sana, lakini wimbo, huu ndio uliovuma sana. Msomaji mpendwa wa makala haya, nakusihi usome maneno ya kajeri na majibu yaliyomo kwenye wimbo wa nguli huyu:

Kejeri

“Siti binti Saadi kawa mtu lini,

Kaja mjini na Kaniki chini,

Kama si sauti angekula nini?

Siti bint Saadi kwa kujua hila za wabaya wake, akaona isiwe taabu akajibu mashambulizi kwa namna hii:

Majibu

“Si hoja uzuri,

Na sura jamali,

Kuwa mtukufu,

Na jadi kebeli,

Hasara ya mtu,

Kukosa akili”.

Kwa kujibu shambulio hilo kwa namna yake aliweza kuwafunga midomo wale wote waliokuwa wakimfuatafuata.

Uanaharakati

Siti alikuwa ni mwanamke wa kwanza kuwa mwanaharakati katika kipindi chake, aliweza kuwatetea wanawake na wanyonge kwa ujumla.

Kipindi hicho, watu waliokuwa matajiri walikuwa wakiwaonea masikini, walipofikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Waliweza kutoa hongo ili kuachiwa huru, halafu yule aliyeshitaki ndiye akafungwa!



Kijiti

Utunzi wake wa wimbo wa ‘Kijiti’ ulimpatia sifa kubwa kwani ulikuwa ukielezea kisa cha kweli kilichomkuta mwanamke mmoja mgeni kutoka Bara.

Mwanamke huyo alipofika Zanzibar, alikutana na tajiri mmoja ambaye alijifanya amempenda. Hivyo akamchukua na kulala naye halafu baadaye akakatisha maisha yake kwa kumuua!

Tajiri yule alishitakiwa kwa bahati nzuri walikuwepo mashahidi wawili walioshuhudia tukio lile.

Kupitis utajiri wake, alitoa hongo kesi ikawageukia wale mashahidi na wakafungwa.

Kwa Weledi aliokuwa nao Siti, akaachia kibao hiki:

“Tazameni tazameni,

Eti alofanya Kijiti,

Kumchukua mgeni,

Kumcheza foliti,

Kenda naye maguguni,

Kamrejesha maiti”.

Siti aliendelea kumwambia tajiri yule kupitia nyimbo zake kwamba asijethubutu kwenda Dar er Salaam, kwa maana watu wenye hasira wanamsubiri na wameapa kwa ajili yake.

Nguli huyo Aliendelea kufanya shughuli zake za muziki hadi uzee ulipompata.

Shaaban Robert.

Muda mfupi kabla ya kifo chake, Siti alikutana na mwandishi maarufu na mwanamashairi Shaaban Robert, ambaye alimhoji na kuweza kuandika Wasifu wake katika kitabu alichokiita ‘Wasifu wa Siti binti Saadi’

Wasifu huo unaonekana kuwa ndio bora zaidi uliowahi kuandikwa katika fasihi ya Tanzania. Kitabu hicho kinatumika kufundishia shule za sekondari za Tanzania.

Ilipotimu Julai 08, 1950 Siti binti Saadi alifariki dunia na kuacha pengo kubwa katika tasnia ya taarab.

Hata baada ya kifo chake jina lake bado linatumika sana kama kielelezo cha ushujaa wake.

Hadi leo hii Siti hutumika kama kipimo cha kufundishia uimbaji wa taarab. Anakumbukwa katika historia yake ya kuwa mwanamke wa kwanza Afrika mashariki kurekodi muziki katika santuri.


Bi. Kidude

Japo pengo hilo halikuweza kuzibika, lakini kuna watu wengine waliibuka wakawa na umaarufu wa kutunga na kuimba taarab kupitia kwake, mfano hai ni marehemu Fatuma Binti Baraka a.k.a Bi. Kidude.

Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA), kimetumia jina lake kulipa jina gazeti la chama chao ‘Sauti ya Siti.

Siku zinavyokwenda taarabu nayo imebadilika kwa kiasi kikubwa. Ala za muziki na mirindimo ya zamani huwezi kuzipata miaka ya hivi karibuni.

Wasanii wa miaka hii ya karibuni, wamedai kuuboresha muziki huo kwa kubadili mirindimo huku waimbaji kulishambulia jukwaa wakicheza pamoja na wanenguaji . Wameuita ‘Tara dansi’. Lakini wasanii hao wamekwenda mbali kwa kubuni mtindo wa ‘Tara Singeli’.

Swali la kujiuliuza muziki wa taarab wa siku za hivi karibuni uliojaa mipasho, utaishi?

Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi, Amina.


Mwisho.

Mwandaaji wa makala haya anapatikana kwa namba: 0784331200, 0767331200, 0713331200 na 0736331200.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/37suLFW
via

Post a Comment

0 Comments