Ticker

10/recent/ticker-posts

WAGENI 250 KUANZA MKUTANO WA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UBUNIFU LEO JIJINI DAR

 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. Amos Nungu katikati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na mkutano wa kubadilishana uzoefu wa  Masuala ya Sayansi Techinolojia  na Uzoefu unaoanza leo hapa nchini kulia ni Ofisa Mtafiti wa Costech, Neema Tindamanyire na kushoto ni Meneja Sayansi Hai kutoka Costech, Hulda Gideon.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimzikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. Amos Nungu.

WAGENI 250 kutoka nchi mbalimbali duniani wamewasili hapa nchini kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Baraza la Sayansi Kanda ya Afrika kwa lengo la kubadilishana uzoefu pamoja kujifunza kuhusu masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. Amos Nungu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu mkutano huo ambao unaoanza leo.

Alisema mada inayotawala mkutano huo ni sayansi wazi na shirikishi katika utafiti na ubunifu wa maendeleo, hivyo Costech kama mratibu wa masuala hayo ya utafiti, teknolojia na ubunifu imepewa dhamana ya kuandaa mkutano huo.

“Kupitia mkutano huu tutabadilishana uzoefu pamoja na kujifunza kutoka kwa kila mmoja, pia kujenga mahusiano pale inapowezekana,” alisema Dk. Nungu.

Dk. Nungu alisema, Tanzania ipo kwenye sera ya uchumi wa viwanda hivyo katika mkutano huo watajifunza mambo mengi kutoka kwa wengine kwa kuwa nchi 16 za Afrika zinashiriki pamoja na mataifa makubwa karibu kila bara.

Katika mkutano huo, Dk. Nungu alisema Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Dk. Joyce Ndalichako atafungua.

Kwa upande wa Meneja Sayansi Hai kutoka Costech, Hulda Gideon alisema mkutano huo utazungumzia sayansi wazi kwa maana kuwa mawazo yote yanayotolewa yawe shirikishi, andiko pamoja na utafiti unaofanyika kuwa wazi na mwishoni taarifa ziwe wazi kwa ajili yaw engine kuzitumia.

Alisema sayansi wazi haiangali maandiko tu ya utafiti bali hata vifaa vinavyotumika ambavyo vinaweza kusaidia wengine ambao hawana vifaa hivyo.

Alisema Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazokuza sayansi nayo imeshiriki kwenye utafiti na data katika sekta ya afya na maliasili ambavyo kwa Tanzania inaongelewa kuwa ina viumbe hai wengi.

“Inabidi sayansi ilivyofanyika ikatumika kuwaambia watu kuwa kuna utafiti huo umefanyika. Hata kwa upande wa dawa unakuta mimea mingi ipo kwa nchi za Afrika ambazo ni maskini utafiti ukifanyika huku kama hakuna uwazi, yale maandiko yatabakia nchi zilizoendelea wataingia kwenye viwanda vyao na kuzalisha dawa halafu sisi tunasubiri kununua dawa kutoka kwao.

“Lakini kama tukiwa ile sayansi wazi watajua kuwa dawa zile pamoja na kuwa zimetengenezwa kwenye viwanda vya nje lakini zilitokea Afrika ni rahisi kushare ile keki iliyotokana na dawa hizo,” alisema.

Alisema hiyo ndiyo maana halisi ya kuhamasisha Tanzania kuingia kwenye michakato yote ya kuwa na sayansi hai inayokuwa na uwazi zaidi.

“Lengo kubwa la kuwa na sayansi hai ni kukuza sayansi yenyewe, kama Afrika au nchi zinazoendelea hatujafika kule lakini tukiifanya ile sayansi ikawa wazi ina maana wale wenzetu kule nje wanachokifanya na sisi tutakijua, tukikijua hatuna haja ya kuanza kitu upya tutatumia vile ambavyo wamevifanya na kuvileta huku kwetu kwa ajili ya kuviendeleza,” alisema.

 Sayansi wazi pia inasaidia kupunguza gharama hivyo mtu anayefanya utafiti wa aina hiyo nchini hatakuwa na haja ya kununua kifaa kinachohitajika ikiwa ni pamoja na kukuza ushirikiano baada ya kujua mwingine ana nini au anafanya nini.

Hata hivyo Ofisa Mtafiti wa Costech, Neema Tindamanyire alisema hadi kufikia jana nusu ya wageni walioalikwa walikuwa wameshafika.

Katika mkutano huo takribani sh. milioni 500 zitatumiwa na wageni hao kama gharama za kwenye hoteli, vyakula na huduma mbalimbali watakazozipata nchini ikiwa ni pamoja na kutembelea vivutio mbalimbali


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2NyIwe0
via

Post a Comment

0 Comments