Ticker

10/recent/ticker-posts

WACHUNGAJI WATATU KANISA LA EAGT WAWASILISHA KUSUDIO LA KUKATA RUFAA MAHAKAMA KUU

Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii

WACHUNGAJI watatu wa Kanisa la EAGT (Tanzania) wamewasilisha kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu ili waweze kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Novemba 15, mwaka 2019 na Jaji Leila Mgonya.

Kusudio hilo la rufaa limewasilishwa mahakamani hapo na Wakili Edwin Swalle anayewawakilisha, wachungaji, Yared Lesilwa, Gilbert Weja na Petrol Kapama kwà niaba ya wenzao 543 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Wakili Swale amesema wanakata rufaa kwa sababu hawajaridhika na uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu wa kuwataka wateja wake kuandika barua kwanza ili kuona kama wanaweza kusuluhishwa nje ya Mahakama kupitia viongozi wa Kanisa ama la.

Amedai, wao wanaamini Mahakama ilijipotosha vibaya kwa kutoa uamuzi huo kwa sababu maombi yaliyokuwepo mbele yake ni kutoa kibali kwa wachungaji hao watatu waweze kuwawakilisha wenzao 543 na siyo kujadili undani wa tuhuma.

Ameongeza wateja wake walikwishajaribu kutafuta mwafaka bila mafanikio, hivyo chombo pekee cha kutatua mgogoro huo ambao ni tuhuma za ubadhirifu wa mali za Kanisa na ukwepaji wa kodi ni mahakama pekee.

Ameendelea kudai kuwa, kwa sababu hiyo hapakuwa na sababu ya kujadili ama kuzungumzia tena jambo lingine nje ya mahakama au kujadili hoja ambazo Mahakama ilishazitolea uamuzi tarehe 9 Agosti, 2019. 

Ambapo Jaji Mgonya baada ya kuangalia kama wadaiwa wanastahili kushtakiwa binafsi ama bodi ya wadhamini ya kanisa hilo,alisema wanastahili kushtakiwa mahakamani.

“Lengo la kwenda Mahakama ya Rufaa ni ili iruhusu wapewe kibali cha kuendelea kwa niaba ya wachungaji wenzao 543 kutoka maeneo mbali mbali nchini ambao ni ngumu kwao wote kufika Mahakamani na ni upotevu wa fedha na muda,"amesema Swalle.

Katika shauri hilo, Wachungaji hao ambao wanatetewa na Wakili Swalle walikuwa wakiomba kuruhusiwa kuwashtaki viongozi wa Kanisa la EAGT (Tanzania ) ambao ni wadaiwa katika kesi hiyo.

Wachungaji hao ni mchungaji Christomoo Ngowi ambaye ni mdhamini wa kanisa hilo, mchungaji Asumwisye Mwang'mbola ambaye naye alikuwa mdhamini wa kanisa hilo lakini kwa sasa ni marehemu.

Wengine ni mchungaji Brown Mwakipesile ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Mchungaji Leonard Mwizarubi Katibu Mkuu na mchungaji Praygod Mgonja ambaye ni muweka Hazina wa kanisa hilokwa tuhuma za ubadhilifu wa mali za kanisa, ukwepaji wa kodi kwa kuingiza magari kinyume cha taratibu.

Ambapo walipata msamaha wa kodi ya Serikali wakati magari hayo hayapo kwenye orodha ya mali za kanisa na uvunjifu wa katiba kwa kuwafukuza wachungaji bila ya kufuatia katiba ya kanisa na sheria za nchi.

Hata hivyo kwa upande wa wadaiwa walipinga maombi hayo wakidai kuwa wao hawapaswi kushtakiwa kwa mashtaka hayo ila bodi ya wadhamini ya kanisa hilo ndiyo ishtakiwe siyo wao kama viongozi kwa majina yao.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/37o5Zqr
via

Post a Comment

0 Comments