WABUNGE WAELIMISHWA KUHUSU UWEKEZAJI NCHINI, WAELEZWA NAFASI YA TANZANIA DUNIANI

  Masama Blog      
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimepata fursa ya kutoa elimu ya uwekezaji kwa wabunge kupitia semina iliyotolewa kwa wajumbe wa Kamati mbili za Bunge ikiwa ni mkakati maalumu wa kuwajengea uwezo kufahamu masuala ya uwekezaji nchini.

Semina hiyo imefanyika Mjini Dodoma na ilifunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki .Kamati hizo ni Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma na Kamati ya Katiba na Sheria. 

Hivyo wabunge hao walielimishwa kwa undani kuhusu majukumu ya TIC, namna kituo kinavyovutia uwekezaji kwa kuzingatia hitaji la mwekezaji, sababu za kuwekeza Tanzania, vigezo vya mwekezaji kujisajili na TIC, vivutio vya uwekezaji na namna ambavyo vinachangia kuvutia uwekezaji mpya.

Pia wameelezwa kuhusu umuhimu wa uwepo wa dirisha la huduma za mahala pamoja TIC kwa wawekezaji na namna linavyofanikisha uwekezaji, faida za uwekezaji na nafasi ya Tanzania katika masuala ya uwekezaji, mgawanyo wa miradi ya uwekezaji kimkoa.

Mengine yaliyoelewa kwa wabunge hao ni namna miundombinu mizuri inavyochangia kuvutia uwekezaji, na namna ambavyo uharaka wa upatikanaji wa idhini(vibali,vyeti na leseni) mbalimbali za kufanikisha uwekezaji zinavyovutia uwekezaji. 

Akizungumza mbele ya wabunge hao Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Goefrey Mwambe ameweka bayana namna ambavyo mataifa yote duniani yanavyoshindana kuvutia uwekezaji, changamoto za uwekezaji na mapendekezo ya maboresho ya mazingira ya uwekezaji nchini ili kuvutia uwekezaji zaidi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji kwa Umma Dk. Chegeni amesema kupitia semina wamepata picha kubwa ya mwenendo na nafasi ya Tanzania kiuwekezaji duniani, Afrika na Afrika Mashariki. 

Amesema, tayari kuna mikakati na jitihada zinazochukuliwa na Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji lakini tuongeze kasi ili kufanikisha uwekezaji zaidi. Semina imechangia kuwaongezea elimu zaidi kuhusu uwekezaji na watakuwa katika nafasi nzuri ya kuchangia pale hoja za uwekezaji zitakapowasilishwa Bungeni. 

Dk.Chegeni amehimiza TIC iendelee kutoa elimu ya uwekezaji kwa wadau wote wakieleza TIC na majukumu yake, faida za uwekezaji kwa nchi na faida za mwekezaji akijisajili na TIC katika kufanikisha uwekezaji wake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki akitoa neno la ufunguzi kabla ya semina ya wabunge iliyoandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) kuanza. Semina hiyo imefanyika Mjini Dodoma
 Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geoffrey Mwambe akitoa mada wakati wa semina hiyo iliyofanyika Mjini  Dodoma


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/33vrLWF
via
logoblog

Thanks for reading WABUNGE WAELIMISHWA KUHUSU UWEKEZAJI NCHINI, WAELEZWA NAFASI YA TANZANIA DUNIANI

Previous
« Prev Post