Ticker

10/recent/ticker-posts

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU WALENGWA WA TASAF KULAZIMISHWA KUCHANGIA BIMA ZA AFYA NA MICHANGO YA KIJAMII

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb) akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Mhe. Omary Ahmed Badwel Bungeni leo jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililohusu  Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika vijiji vyote nchini. 

Na. Aaron Mrikaria-Dodoma

Serikali imewaagiza Viongozi wa Vijiji kutowalazimisha walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kukatwa ruzuku kwa ajili ya kuchangia bima za afya na michango mbalimbali ya kijamii kwani ruzuku hiyo hutolewa na Serikali kwa ajili ya kuziwezesha kaya maskini kujikwamua kiuchumi.

Agizo hilo limetolewa Bungeni leo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Mhe. Omary Ahmed Badwel aliyetaka kujua Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika vijiji vyote nchini.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, ruzuku inayotolewa na Serikali kwa walengwa ni kwa ajili ya kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi kama vile chakula, gharama za elimu na Afya na kuwekeza katika kuanzisha miradi itakayowaongezea kipato na hatimaye kujikwamua na umaskini, hivyo ni maamuzi ya kaya husika kupanga matumizi ya ruzuku wanayoipata.

“Katika baadhi ya maeneo, Viongozi wa Vijiji wamekuwa wakiwalazimisha walengwa kukatwa ruzuku ili kulipia bima za afya na michango mbalimbali jambo ambalo si sahihi na halikubaliki”, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameelekeza walengwa kutokatwa ruzuku moja kwa moja bila ridhaa yao bali wapewe stahiki zao na kama kuna michango ya shughuli za maendeleo ya kijiji inapaswa kutozwa kwa wananchi wote wa kijiji husika. 

Dkt. Mwanjelwa amewataka viongozi wote waliokuwa wanatoa amri ya kukatwa kwa ruzuku za walengwa wa TASAF moja kwa moja bila ridhaa yao, waache mara moja kwani ni kinyume cha utaratibu na iwapo wataendelea, Serikali itawachukulia hatua za kali za kinidhamu na kisheria. 

Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini tangu uanze kutekelezwa na Serikali mwaka 2013 umezinufaisha kaya maskini kwa asilimia 70, na hivi sasa Serikali inajiandaa kuanza utekelezaji wa Awamu ya Tatu sehemu ya pili mwishoni mwa mwaka huu baada ya Serikali kupata fedha lengo likiwa ni kuzifikia kaya zote maskini nchini. 



from MICHUZI BLOG https://ift.tt/32nD95y
via

Post a Comment

0 Comments