Ticker

10/recent/ticker-posts

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUSIMAMIA MASLAHI YA WAFUGAJI NA KUWATAKA KUFUATA SHERIA ZA NCHI

Na. Edward Kondela

Serikali imewataka wafugaji katika Wilaya za Chunya na Mbarali Mkoani Mbeya kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi ikiwemo ya kutoingiza mifugo katika maeneo ya Hifadhi za Taifa ya Ruaha na Pori la Akiba la Ruangwa, hali ambayo imekuwa ikisababisha migogoro kati ya wafugaji na askari wa Hifadhi za Taifa (TANAPA), wanaolinda hifadhi hizo ambapo baadhi ya migogoro hiyo imesababisha vifo vya wafugaji, askari na mifugo.

Akizungumza Jumanne hii (19.11.2019) wakati wa kuhitimisha ziara ya siku mbili ya makatibu wakuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Sheria na Katiba, waliozuru baadhi ya maeneo yenye migogoro katika wilaya hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka wafugaji kuacha tabia ya kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi kwa ajili ya malisho kwa kuwa ni kinyume na taratibu za nchi.

“Serikali inawataka wafugaji wote kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na kutoingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi za taifa kwa kuwa ni kinyume cha sheria pia serikali itaendelea kuhakikisha wafugaji wanafanya shughuli zao kwa amani bila kubughudhiwa ili mradi wanafuata sheria na taratibu za nchi ikiwemo ya kutoingiza mifugo katika mashamba ya wakulima.” Amesema Prof. Gabriel

Akizungumza kwa niaba ya makatibu wakuu wa wizara hizo, Prof. Gabriel amefafanua kuwa kutokana na Tangazo la Serikali (GN) Na. 28 la Tarehe 14 mwezi Machi mwaka 2008, ambalo liliongeza eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kutoka Kilometa za Mraba 5,878 hadi kufikia Kilometa za Mraba 20,226 hali hiyo imesababisha eneo la malisho kupungua kutoka hekta 259,000 za awali hadi 154,000 katika Wilaya za Chunya na Mbarali ambapo amewataka wafugaji katika wilaya hizo kuheshimu tangazo hilo wakati serikali ikifanyia kazi maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kuainishwa kwa vijiji vilivyopo katika maeneo ya hifadhi ili maboresho yaweze kufanyika kwa maslahi ya vijiji hivyo.

Katika ziara hiyo ya makatibu wakuu kutoka wizara nne Mkoani Mbeya uongozi wa TANAPA umekubali kutengeneza barabara za kuainisha mipaka ya maeneo ya hifadhi na vijiji mara baada ya kuainishwa kwa mipaka mipya kufuatia agizo la Rais Dkt. John Magufuli la kutambuliwa kwa maeneo ya vijiji na hifadhi za taifa ambalo tayari linafanyiwa kazi.

Kufuatia matukio ya mauaji ya askari mmoja wa TANAPA na askari mgambo mmoja mwaka 2018 waliouawa na wafugaji wakati wakiswaga ng’ombe waliokamatwa katika Hifadhi ya Ruaha kuelekea Kambi ya Nyota ya TANAPA iliyopo Wilaya ya Mbarali na tukio la hivi karibuni la Tarehe 11 Mwezi Oktoba 2019 la kuvamiwa kwa kambi hiyo na baadhi ya wafugaji wakiwa na silaha za jadi kwa nia ya kukomboa mifugo iliyokamatwa katika Hifadhi ya Ruaha hali iliyosababisha kijana mmoja wa wafugaji (19) kupigwa risasi na askari wa TANAPA na ng’ombe 14 kuuawa, Katibu Mkuu Prof. Gabriel amewataka wafugaji kutumia njia zisizo halali kukomboa mifugo iliyokamatwa.

Akizungumza na baadhi ya wafugaji katika Kijiji cha Igunda, Kata ya Igava Wilayani Mbarali, katibu mkuu huyo amefafanua kwa wafugaji hao kuwa kutokana na sheria na haki za wanyama duniani ni makosa kuua mnyama bila kuwa na sababu za msingi hali iliyosababisha serikali kuchukua hatua kwa askari wa TANAPA waliohusika kupiga ng’ombe hao risasi na hivyo kuwataka wafugaji hao kuwa watulivu kwa kuwa suala hilo linashughulikiwa na vyombo vya dola.

Aidha ameeleza kuwa kuwa pindi mifugo inapokamatwa na askari wa TANAPA inapobainika kuingia kwenye maeneo ya hifadhi, wamiliki wa mifugo hiyo wanapaswa kufuata taratibu za kisheria za kulipa faini na kukabidhiwa mifugo yao na kusisitiza kuwa ni muhimu kwa wafugaji kujiepusha kuingiza mifugo maeneo wasiyoruhusiwa yakiwemo ya Hifadhi za Taifa.

“Sisi viongozi wa Wizara za Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Mambo ya Ndani ya Nchi na Sheria na Katiba tunasikitishwa sana na matukio haya ya mauaji kijana mdogo amefariki dunia kwa sababu ambazo zingeweza kuepukika kwa kutaka kumdhuru askari kwa kutumia silaha za jadi akiwa na wenzake takriban 20 ili kukomboa ng’ombe waliokamatwa hifadhini, tunawaomba mjiepushe na matukio ya namna hii fuateni sheria na taratibu za nchi ili mfuge bila bughudha.” Amefafanua Prof. Gabriel

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwaongoza viongozi wenzake katika ziara hiyo akiwemo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ramadhan Kailima, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba Bw. Amon Mpanju na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Maurus Msuha akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda wamefika pia katika Kijiji cha Lualaje Kata ya Lualaje Wilayani Chunya na kuzungumza na baadhi ya wafugaji kufuatia matukio ya wafugaji hao kuingiza ng’ombe katika Hifadhi ya Ruaha.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ramadhan Kailima amewataka wafugaji hao kufuata sheria na taratibu za nchi na kwamba jeshi la polisi litazidi kutoa ushirikiano kwa wafugaji hao katika matukio mbalimbali yakiwemo ya kuwabaini baadhi ya wafugaji ambao wamekuwa wakiingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi pamoja na kujihusisha na uhalifu.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba Bw. Amon Mpanju amewataka wafugaji kuwa watulivu na walitambue Tangazo la Serikali Na. 20 la Tarehe 14 mwezi Machi mwaka 2008, ambalo liliongeza eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kupunguza eneo la malisho katika Wilaya za Chunya na Mbarali hali iliyosabisha baadhi ya maeneo waliyokuwa wakiyamiliki kubadilishwa matumizi na kuwa ya hifadhi, ambapo suala hilo tayari linafanyiwa kazi kwa maelekezo ya Rais Magufuli na kuwataka kutoingiza mifugo yao katika eneo la hifadhi hadi serikali itakapotangaza maamuzi mengine.

Kuhusu kuainishwa kwa mipaka kati ya vijiji na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na Pori la Akiba la Ruangwa, akizungumza kwa niaba ya katibu mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kutoka katika wizara hiyo Dkt. Maurus Msuha amesema serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itahakikisha inatuma timu ya wataamu katika maeneo hayo ili kuweka alama maeneo ambayo wananchi yanawatatiza kufahamu mipaka ya vijiji na maeneo ya hifadhi ili kuondoa migogoro kati ya maeneo ya wakulima na wafugaji na mipaka ya Hifadhi ya Ruaha na Pori la Akiba la Ruangwa.

Baadhi ya wananchi katika Wilaya za Chunya na Mbarali waliopata fursa ya kuzungumza wakati wa ziara ya makatibu wakuu kutoka Wizara za Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Mambo ya Ndani ya Nchi na Sheria na Katiba wamesema wamefurahishwa na ziara hiyo na kwamba watazingatia maelekezo waliyopatiwa ili kuhakikisha wanafuga kwa kufuata sheria na kwamba watashirikiana na serikali ili kuwabaini baadhi ya wafugaji wanaokiuka sheria na kuingiza mifugo katika maeneo ya Hifadhi ya Ruaha na Pori la Akiba la Ruangwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamefafanua kuwa wamefurahishwa kwa viongozi hao wa juu kutoka wizarani kufika hadi katika maeneo yao na kujionea changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ya maji na malisho pamoja na kupata taarifa za matukio ambayo yamejitokeza katika wilaya hizo kutoka mamlaka mbalimbali za serikali wakiwemo viongozi wa serikali, wafugaji pamoja jeshi la polisi.

Awali kabla ya makatibu wakuu hao kutembelea wafugaji katika Wilaya za Chunya na Mbarali, wamefika katika Ofisi ya Mkuu wa Mbeya na kuwa na mazungumzo na mkuu wa mkoa huo Mhe. Albert Chalamila pamoja Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya, ambapo Mhe. Chalamila amewaambia serikali ya mkoa huo itaendelea kufanya kazi kwa kusimamia sheria na kuwaasa viongozi wenzake wanapofika mkoani hapo kupata taarifa sahihi ya mkoa kabla ya kufika katika maeneo mbalimbali kuzungumza na wananchi.

Aidha Mhe. Chalamila amebainisha kuwa migogoro ya wafugaji katika Wilaya za Chunya na Mbarali ambao wamekuwa wakiingiza mifugo kwenye maeneo ya Hifadhi ya Ruaha na Pori la Akiba la Ruangwa katika Mkoa wa Mbeya unatokana na wafugaji kuwa na mifugo mingi tofauti na maeneo ya malisho, hali ambayo imekuwa ikiulazimu uongozi wa mkoa kutoa elimu kwa wafugaji juu ya ufugaji wa kisasa na wenye tija kwa wafugaji kuwa na ng’ombe wachache wanaoweza kuwapatia matokeo mazuri.

Ameongeza kuwa uongozi wa Mkoa wa Mbeya utazidi kusimamia na kutoruhusu mifugo kuingizwa katika maeneo ya hifadhi pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha mkoa huo unakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Katika ziara hiyo ya makatibu wakuu wanne Mkoani Mbeya, ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ramadhan Kailima, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba Bw. Amon Mpanju na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Maurus Msuha akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda, ilikuwa na lengo la kupata taarifa sahihi ya hali ya wafugaji katika Wilaya za Chunya na Mbarali pamoja na kupata hadidu za rejea ambazo wataalam watatumia katika kufanya mapitio na maboresho ya Tangazo la Serikali (GN) Na. 28 la Mwaka 2008 ili iwe shirikishi na kupata suluhu ya migogoro ya wakulima na wafugaji.
 Picha ya pamoja ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila akiwa na makatibu wakuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Maliasili na Utalii akiwakilishwa na mkurugenzi wa idara ya wanyamapori na Wizara ya Sheria na Katiba, mara baada ya mazungumzo kuhusu hali ya ufugaji katika Wilaya za Chunya na Mbarali mkoani humo, wakiwa tayari kutembelea maeneo ambayo yamekumbwa na migogoro ili kupata hadidu za rejea zitakazotumiwa na wataalam ili kutatua migogoro hiyo katika ziara ya siku mbili kuanzia tarehe 18-19 mwezi Novemba 2019.
 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiangalia moja ya vielelezo pamoja na kuoneshwa ramani ya mipaka iliyowekwa kutenganisha maeneo ya vijiji na Hifadhi ya Ruaha na Pori la Akiba la Ruangwa, katika ziara ya siku mbili Mkoani Mbeya kuanzia tarehe 18-19 mwezi Novemba 2019 akiwa na viongozi wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Sheria na Katiba na Wizara ya Maliasili na Utalii.
 Kutoka kushoto picha ya kwanza: Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba Bw. Amon Mpanju, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ramadhan Kailima, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Maurus Msuha akimwakilisha katibu mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii wakizungumza na wananchi katika Kijiji cha Igunda, wilayani Mbarali na kuwasisitiza serikali itaendelea kusimamia maslahi ya wafugaji na kuwataka wafuate sheria na kuheshimu mipaka ya hifadhi za taifa na maeneo ya vijiji, wakati viongozi hao walipokuwa wakihitimisha ziara ya siku mbili Mkoani Mbeya katika Wilaya za Chunya na Mbarali kuanzia tarehe 18-19 mwezi Novemba 2019.




from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2Ov4BJL
via

Post a Comment

0 Comments