Ticker

10/recent/ticker-posts

ONYO KALI LATOLEWA KWA WATU WENYE KUTAKA KUVURUGA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA , KUVUNJA AMANI ILIYOPO

Waziri wa Mambo ya Ndani,Mhe. Kangi Lugola akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo suala la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Uhalifu na matumizi mabaya ya mitandano ya kijamii.

WIZARA ya Mambo ya Ndani pamoja na Jeshi la Polisi wametoa onyo kali kwa watu ambao watabainika kutaka kuvuruga mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 24 mwaka huu kwa kutoa lugha za kuchonganisha au kupotosha.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani imesema Jeshi la Polisi limejipanga kukabiliana na wote ambao wanatarajia kufanya matukio ya uvunjifu wa amani na kwamba mbali ya kutiwa nguvuni wajiandae kudumbukizwa kwenye maji ya washawasha na si kumwagiwa maji hayo kama ilivyozoeleka.

Akizungumza  leo Novemba 2,mwaka 2019 jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola amesema kuwa ole wao wenye mipango ya kuvuruga uchaguzi kwani watashughulikiwa na kwamba vyombo vya ulinzi vimejipanga vizuri.

"Kuna watu wamekuwa na tabia ya kutoa lugha za kuchonganisha wananchi kwa kisingizo cha kufanya kampeni wakati wa mikutano ya kampeni. Wale wenye tabia ya kupotosha au kuvunja amani safari hii hawana nafasi,anayebisha ajaribu hata sasa aone .Washawasha watamwagiwa na sio tu kumwagiwa bali tutawatumbukiza katika maji yenyewe,"amesema Waziri Lugola.

Ameongeza kuwa Polisi wameandaa mpango kazi kuhakikisha UCHAGUZI wa Serikali za Mtaa unakwenda vizuri ,hivyo atakayethubutu kujaribu kuuvuruga atakiona cha moto chini ya yeye(Waziri) , IGP Sirro na Rais Dk.John Magufuli wamedhamiria kuhakikisha amani iliyopo nchini inaendelea kuwepo na hakuna anaeweza kuivuruga kwa kigezo cha uchaguzi.

Wakati huo huo Waziri Lugola amesema Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kushughulikia matatizo ya wananchi na kwamba ametoa maagizo kwa IGP Sirro kuhakikisha makamanda wa Polisi katika Mikoa yote na Makamanda wa Polisi wa Wilaya wanapanga ratiba ya kwenda kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi.

Amesema katika ziara za viongozi wakuu wa nchi, wamekuwa wakipokea malalamiko na hivyo wamekubaliana makamanda hao watoke na ameahidi kufuatilia utendaji wao na wale ambao watafanya kazi kwa kusuasua wajiangalie kwani hatawavumilia .


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/34mRhxn
via

Post a Comment

0 Comments