Nimeikumbuka Sanaa ya zamani, natamani kurudia utoto tena

  Masama Blog      

Charles James

MALKIA wa Bongo Fleva na Dada mwenye nyota tano, Lady Jay Dee, Komando alipata kuimba 'natamani kuwa malaika, natamani nirudi kama mtoto.

Mimi naondoka na huo mstari wa ninatamani kurudi kuwa kama mtoto. 

Ndio. Kuna vitu sivioni hivi sasa kutokana na utandawazi wa Dunia basi natamani muda urudi nyuma nirudie utoto wangu nivione.

Vijana ambao wameikuta sanaa yetu katika nyakati hizi za Instagram ni ngumu kuelewa ninachozungumza.

Kuna mambo ya zamani kila nikiyakumbuka naona utamu wa muziki na maigizo yetu. Naona tasnia ya Burudani kuna vitu inamiss aisee.

Hebu tukumbuke namna ambavyo kwenye Taarab kulikua kunawaka moto siyo masihara? Hivi bado muziki huu wa mwambao upo maana hautambi tena.

Battle ya Bi Khadija Kopa na Chama lake la Tanzania One Theatre (TOT) dhidi ya mhasimu na mpinzani wake Marehemu Aunt Nasma Khamis Kidogo akiwa na Bendi yake ya Muungano Culture Group haikua na mfano wake.

Wapenzi wa Taarab waligawanyika. Watu waligawana upande. Hawa wangetamba na mipasho ya Bi Khadija, wengine wangewehuka na vijembe kutoka kwa Aunt Nasma. 

Upinzani na ushindani ulikuepo wa kutosha na bado haikuwahi kujulikana nani bora zaidi ya mwingine. Kila upande uliamini mtu wao ndiye bora.

Ushindani wa Nasma na Khadija ulikua ni wao peke yao haukuyahusu makundi. Ulikua ni upinzani binafsi ambao TOT wala Muungano haukuwahusu.

Ni kusema kwamba Nasma na Khadija walikua wakubwa kuliko Muungano Culture na TOT. Wakubwa kuzidi waajiri wao. Wanastahili nyota za kutosha hawa Mama zetu.

Baadaye kuliibuka ushindani wa makundi mawili ya Zanzibar Modern Taarab na East African Melody. Vita ilikua kubwa. 

Burudani ilitolewa. Siasa za Muziki zikayavunja makundi haya. Toka hapo Taarab imegeuka kuwa Bongo Fleva.

Vipi kuhusu Michezo ya kuigiza kila Jumamosi, Jumapili kwenye Runinga ya Mzee wetu Hayati Reginald Mengi? Ebwana Kaole walijua kututeka haswa.

Maisha, Jahazi enzi za kina Mr Bomba, Swebe Santana, Sinta na Mtunis katika ubora wao ilikua siyo masihara.

Kipindi hicho ikifika wikiendi unaoga mapema unasubiri taarifa ya habari iishe ngoma ianze. 

Hakukua na suala la kununua kifurushi cha King'amuzi ulikua ni mwendo wa kuzungusha Antenna kutegesha chaneli vizuri.

Maigizo yalikiki mjini. Hakukua na kusimuliana Tamthiliya za akina Sultana. 

Tungepeana stori za Maisha ya akina Mashaka au namna Joti na Mpoki walivyokua wakimdhulumu mlugaluga Masanja Mkandamizaji kwenye Maigizo ya Mambo Hayo.

Kipindi Fulani hata Maigizo ya Kenya yalitukamata kisawa-sawa. Ulikuepo mchezo wa Tausi. Uliojaa wakali akina Mzee Kasry, Kalumanzira, Sitti, Baraza na Mjuba. 

Walitisha kinoma noma. Siyo leo wamebaki na Komedi ya akina Omondi na Churchill Show. Hata wao wenyewe wanajua wamezingua.

Bado sijakushawish kumiss mambo ya zamani? Tusogee kwenye Bongo Fleva kidogo. Hivi ilishawahi kutokea battle kama ya wahuni wa TMK Wanaume Family na watoto wa kishua East Coast Team ya Upanga?

Ebwana hii ilikua ni zaidi ya vita. King Crazy Gk angepiga autro kwenye Leo Tena akisema, "TMK mwisho Rap kuwakilisha".

Kisha Juma Nature akajibu kwenye autro ya Kamua ngoma ya KR Mulla, " Najua umesikia TMK siyo mwisho Rap kuwakilisha". Ushindani ulikua mkubwa na ulisisimua.

Matamasha ya muziki yangejaa sana kutokana na battle za namna hii. ECT ya akina GK, AY na FA walikua watoto wa kishua kweli.

Video zao mavazi yao na mikogo yao ilijawa u-Marekani. TMK waliwateka watoto wa Kiswazi kwa Swaga zao. Staili ya Mapanga haijawahi kumuacha yeyote salama.

Hapo hapo Temeke wakati TMK wakipepetuana na ECT, Supastaa wa Bongo Fleva wakati huo na Kinara wa TMK, Juma Nature nae alikuwa na 'bifu' yake na Mkali wa Staili, Inspector Haroun Babu.

Kama kuna bifu ilichangamsha Bongo Fleva basi hii nayo ni mojawapo. Kosa kubwa lilifanywa walipokubali kurekodi remix ya Mzee wa Busara. 

Ghafla nimeukumbuka ubabe wa Kalapina na wajuba wake wa Kikosi Cha Mizinga. Hawa washikaji walikua watemi sana. 

Wangeweza kumkalisha yeyote ambaye wangemuona anaenda kinyume nao. Siwezi kusahau varangati lao na watoto wa Arusha Nako 2 Nako.

Memba wa N2N, Bou Nako aliingia kwenye rada za Kikosi, basi mkono ukapigwa siyo kitoto. Tokea hapo bifu likazidi. 

Washikaji wa Arusha wakaapa siku Kalapina na Kikosi wakienda Arusha hawatoki salama. Hivi Pina ushawahi kwenda Chuga tena?

Ila makundi ya muziki hayapo siku hizi, wako wapi Unique Sisters wale watoto wa Mzee Kipozi! HBC, Kwanza Unit na Mabaga Fresh? Hakika siwezi kusahau Banjo ya Mandojo na Domokaya.

Bado nakumbuka namna ambavyo Ray C alitumaliza na kiuno chake bila mfupa.Kama unadhani wakina Diamond ndio wasanii wa kwanza kurekodi video zao nje basi unajidanganya. 

Ray C mkwaju wake wa Uko wapi, alishuti video yake nchini Japan. Hiyo nazungumzia miaka 15 iliyopita. Rehema alikua mwanadada wa aina yake katika wakati wake.

Alituvuruga. Tulifurahia kusoma matukio na skendo zake kwenye magazeti kila wiki. Katika zama ambazo bado tuna ushamba wa ustaa, Ray C tayari alikua na Tattoo, vipini kwenye ulimi, kitovuni. 

Mavazi yake hayakumtofautisha na Beyonce wala Mary J Blige. Kweli nyakati hupita. Leo hatumzungumzi tena.

Stori za Wema na Diamond zimewahi kukuchanganya? Wazee wa Old School tulidatishwa na mahusiano ya mhuni Juma Nature na Sista Duu wa Maigizo Sista.

Shukrani kwa magazeti pendwa maana bila wao tusingejua namna Nature alivyokua amedatishwa na Sinta. Labda tungekuja kujua baada ya kupigana chini Kwa kuwa Juma alimtungia wimbo Sista.

Magazeti pendwa ndio yalikua Instagram kwetu. Ubuyu wote tungeupata kwenye Ijumaa au Amani. Hakukua na kununua bando. Ni mwendo wa Hard Copy tu.

Hivi unaona Miss Tanzania pako sawa pale? Nasikia Miss Mbeya wa mwaka huu alipewa Bodaboda kama mshindi.

Enzi ya Miss Tanzania ya Anko Lundega aisee msisimko ulikuepo. Kuanzia ngazi za chini mpaka Taifa.

Nani amesahau mchuano mkali wa mwaka 2001 kati ya Happiness Millen Magese na Miriam Odemba? Mzuka wa Miss Tanzania ulikua mkubwa sana. Lilikua ni shindano kubwa na maarufu zaidi Bongo. Leo ladha haipo tena.

Bado naendelea kukumbuka namna ambavyo shindano la Mkali wa Rhymes lilivyoiteka Nchi. Wapo watu mpaka kesho hawataki kukubali ushindi wa Afande Sale.

Sijui leo Braza Shigongo akiandaa tena nani atashinda. Wacha nimkumbuke mshikaji wetu Cool James Dandu ninapoona tuzo zake za Kilimanjaro Music Awards zikiwa zimefunikwa na hazipo tena. Mwamba hatumtendei haki.

0683 015145
from MICHUZI BLOG https://ift.tt/33mIURI
via
logoblog

Thanks for reading Nimeikumbuka Sanaa ya zamani, natamani kurudia utoto tena

Previous
« Prev Post