Ticker

10/recent/ticker-posts

Na: Moshy Kiyungi,Tabora.

Novemba, 2019.
Nchini Marekani yupo mwanamuziki Steve Wonder mwenye ulemavu wa macho aliye na ukwasi mkubwa unaomuweka katika nafasi ya kuwa miongoni wa wanamuziki matajiri duniani.

Miaka ya 1980 na 1990 alikuwepo mtunzi na mwimbaji katika bendi ya Juwata raia kutoka nchini Kenya, Niko Zengekala, aliyekuwa na ulemavu wa macho pia. Aliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi kwa tungo halikadharika uimbaji wake. Hii ni kudhihirisha kuwa ulemavu siyo sababu ya kubweteka.

Makala haya yanamzungumzia mwanamuziki Anania Ngoliga, mwenye talanta nyingi katika muziki. Amepitia vikwazo vingi vikiwamo vya kubezwa na kufuatia ulofa na ulemavu wake wa macho.

Wasifu wa Ngoliga aliwahi kuelezea kuwa pamoja na kuwa yeye ni mwanamuziki, hajui alikojifunza ala inayoitwa Kalimba, inayotumiwa na wasanii wa eneo lao la Mpawapwa mkoani Dodoma ila alijikuta tu analijuwa.

Ngolinga yaelezwa kuwa alipozaliwa baada ya kupata ufahamu, aliwaona baba pamoja na baba zake wadogo wote wakipiga ala hiyo.

Alisema kuwa hata dada zake watoto wa baba yake mdogo walikuwa mabingwa wa kupiga Kalimba. Kwa kawaida Anania nimcheshi kila wakati, anakumbuka wakati akiwa bado mdogo yeye na ndugu zake walikuwa wakishindana kupiga ala hiyo.

Anania alizaliwa akiwa na udhifu wa kuona vizuri, tatizo hilo liliendelea hadi alipofikisha umri wa miaka mitano, macho yake yakaanza kupoteza uwezo wa kuona kabisa.

Alipelekwa kwenda kuanza shule ya Wasioona ya Buigiri, lakini anakiri na kutoa shukurani nyingi kwa mwalimu wake Abel Mbata. Mwalimu Mbata alikuwa anafundisha hapo Buigiri ndiye aliyemshawishi babu yake ili aweze kujiunga na shule hiyo.

Baba yake Ngoliga baada ya ushawishi huo akafanya mipango yote ya yeye kujiunga na shuleni hapo rasmi.Katika shule ya Buigiri kulikuweko na magitaa na piano na vyombo vingine vya kisasa, hivyo Anania akajifunza pia kupiga vyombo hivyo.

Kufikia darasa la nne tayari alikuwa kiongozi wa kwaya ya shule yake hiyo ya Buigiri.Aliendelea na masomo shuleni hapo hadi alipomaliza darasa la saba mwaka 1976, mara baada ya kumaliza alirudi kwao Mpwapwa mkoani Dodoma.

Anania alipofika Mpwapwa akajiunga na kwaya ya Kanisa Kuu la Anglican la Mpwapwa, ambako hata huko baada ya muda mfupi akawa mwalimu wa Kwaya hiyo.

Mwaka 1987 aliamua kwenda katika jiji la Dar es Salaam akasindikizwa na rafiki yake kwa ajili ya kumsalimia dada yake aliyekuwa kaolewa huko, aliyekuwa akiishi maeneo ya Msasani. Kwa bahati nzuri jirani na alipofikia kukawa na jamaa aliyekuwa na gitaa.

Hivyo Anania Ngoliga akawa anaachiwa kupiga gitaa hilo mara kwa mara, jambo ambalo likamfanya shemeji yake amuulize kwanini asijiunge na mojawapo ya bendi.

Kwakuwa mmiliki wa hilo gitaa alikuwa anawafahamu baadhi ya wanamuziki wa bendi iliyojulikana kama Jambo Stars, iliyokuwa mali ya Dk. Vulata, ikiwa na makao makuu huko Komakoma maeneo ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Hivyo Anania akaenda kuonana na wanamuziki wa bendi hiyo na kujitambulisha kama yeye anauwezo wa kuimba, huku akilazimika kuficha kuwa anajua kupiga gitaa.Alifanya hivyo baada ya kuingiwa na hofu alipowasikia wapigaji wa magitaa waliokuweko katika bendi hiyo wakati ule, ambao walikuwa wazuri sana.

Ngoliga aliwakuta wanamuziki walikuwapo katika bendi hiyo ya Jambos Stars akina Kazembe wa Kazembe, Cobra wa Bilumba ambao wote walikuwa wapigaji wazuri wa magitaa.Alikuwapo Omari Gendaeka aliyekuwa akiliungurumisha gitaa la besi na mwingine aliyekuwa akijulikana kwa majina ya Cheo Ali.

Anania Ngoliga alifanyiwa usaili na akaonekana anafaa, hivyo akawa mmoja wa wanamuziki wa bendi hiyo ya Jambos Stars.Aliendelea kupiga katika bendi hiyo mpaka siku moja ambapo mwanamuziki aliyekuwa raia toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lovy Longomba, alipita kuangalia mazoezi yao.

Baada ya kumshuhudia Ngoliga na kubaini uwezo wake, Lovy muda uleule akatamani kumchukuwa awe katika bendi yake ya Afriso Ngoma.Lovi Longomba akaenda kwa shemeji yake Anania, kumuomba amshawishi Anania ajiunge na Afriso Ngoma. Bendi hiyo ilikuwa ni mali ya mzee Mwendapole na Lovy akiwa kiongozi wa bendi.

Anania alitamka kuwa kitendo hicho aliona kama ni ndoto, kwakuwa hakikupita kipindi kirefu tangu afike katika jiji hilo akitokea Mpwapwa. Aidha alikuwa hajawahi kupigia bendi yoyote, ikaona maajabu pale alipoombwa na mwanamuziki kama Lovy Longomba kwenda kujiunga na bendi yake ilikuwa kama ndoto.

Anania Ngoliga hakufanya ajizi alienda kuripoti katika bendi hiyo ya Afriso Ngoma. Lakini kwa bahati mbaya siku alipofika huko, ilikuwa ndio siku Lovy alikuwa anasafiri. Hata hivyo Lovy aliacha maagizo kwa wanamuziki wenzake kuwa wampokee Anania, kwa uhakika zaidi wamfanyie mahojiano.

Kama Waswahili wasemavyo kuwa “Hakika asiyekujuwa hakuthamini…” hakuna mwanamuziki yeyote miongoni mwao aliyeshughulika naye.

Fikra tele zikamjaa Anania akidhani kuwa yawezekana wenzake hao walimdharau kufuatia udhalili aliokuwa nao,hakuwa hana hata viatu, alikuwa amevaa viatu vya matairi alivyotoka navyo Mpwapwa.

Alienda mbali zaidi akijihisi kuwa labda ulemavu wake wa macho umewafanya wasimtilie maanani.

Baada ya wiki mbili Lovy alirejea akakuta mahojiano hajafanyiwa. Akamuomba aimbe, nae akaimba vizuri baadhi ya nyimbo za Afriso, nakujikuta yuko katika neema kubwa kwani baada ya jaribio hilo akapata ajira mara moja.Wakati huo huo waimbaji wawili wa bendi hiyo Kasavubu na Anderson Supa wakaachishwa kazi.

Bendi ya Afriso Ngoma ilikuwa na imesheheni wanamuziki waliokuwa na uwezo mkubwa katika muziki. Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja na John Maida, Robert Tumaini Mabrish, Mjusi Shemboza, Kasongo Kalembwe, Peter Kazadi wote hao walikuwa wakishika ala za muziki.

Kwa upande wa waimbaji walikuwa Lovi Longomba, Ramadhani Kinguti ‘Systeme’, Tofi Mvambe na mwenyewe Anania Ngoliga.Bendi hiyo iliweza kurekodi nyimbo nyingi ikiwemo ya ‘Elly wangu’ vilevile ilipata fulsa ya kusafiri karibu wilaya zote hapa nchini.

Ngoliga baadaye aliamua ‘kuitosa’ Afriso Ngoma, akahamia katika bendi ya Legho Stars iliyokuwa imeanzishwa.Kwa mara ya kwanza bendi ya Legho Stars ilipoanzishwa waimbaji walikuwa yeye Anania Ngoliga, Tshibanda Sonny, Marcelino Vitalis na Lucy Emea. Kwa upande wa wapiga vyombo walikuwapo akina Stamili Uvuruge, Chris Chiwaligo, George Mtully na Hemed Mganga.

Bendi ya Legho Stars nayo ilionja hamahama ya wanamuziki wake. Kama ilivyo kawaida ya wanamuziki kuhamahama, Legho Stars iliondokewa na wanamuziki wake akina Stamili Uvuruge pamoja na Tshibanda Sonny.

Ili kuiamarisha bendi hiyo, iliwasajiri wanamuziki wengine akiwemo mtunzi na mwimbaji Tshimanga Kalala Assosa, Jemsia Msuya, John Maeda na Shaaban Manyanya kwa pamoja wakaianza Legho Stars ya awamu ya pili.

Ngoliga bado safari yake ya kutafuta ilikuwa haijakamilika. Hakukaa sana katika bendi hiyo ya Legho Stars akaenda kujiunga na kundi la Ram Choc Stars liliyokuwa linaongozwa na mwanamama Rukia Mtama.

Katika bendi hiyo ilikutana na waimbaji wengine ‘wakali’ akina Banza Tax, Salim Shaaban, Adiel Makula, Chris Chiwaligo, Ado Mpoloto , Geofrey Charahani na kwenye upigaji wa gitaa la rhythm, alikuwa ni Yahaya Mkango.

Ram Choc Stars ilipata mkataba katika Iringa hotel,iliyopo mjini Iringa.
Wanamuziki takribani wote walitimka wote kwa pamoja siku ya mwaka mpya 1991, wakaiacha bendi hiyo wakilalamika kutolipwa mishahara.

Ule msemo wa Waswahili kwamba “Usiache mbachao kwa msala upitao” Ngoliga baada ya ‘mtiti’ wa wanamuziki wa bendi nzima kuhama Ram Choc Stars, aliamua kurejea tena Legho Stars wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Joseph Mulenga ‘King Spoiler’ aliyekuwa akilicharaza gitaa la solo.

Wanamuziki wengine waliokuwepo ni John Maida, alikuwa akipiga gitaa la rhythm na Christopher Chiwaligo na gitaa la besi lilikuwa likiungurumishwa na Adolf Mpoloto.

Waimbaji walikuwa Ana Mwaole, Banza Tax, Salim Shaban na yeye Anania Ngoliga.

Lakini kama nilivyokujuza msomaji wa makala haya kwamba Anania alikuwa mtafutaji. Kwa mara nyingine tena akaiacha bendi hiyo na kuhamia kwenye bendi iliyokuwa mbioni kuanzishwa ya Ngoza Makayota.Juhudi za kuanzisha bendi hiyo ziligonga ukuta baada ya danadana za ahadi zikawa nyingi bila kununuliwa vyombo vya muziki.

Wanamuziki hao wakawa wanafanya mazoezi bila kupiga dansi. Hali hiyo ilipelekea yeye na wanamuziki wenzake wakaondoka tena kundi zima na kwenda Iringa. Huko wakajiunga na bendi iliyokuwa inaendeshwa na kanisa Katoliki la Mshindo iliyokuwa inaitwa VICO Stars (Vijana Catholic Stars). Hata huko hawakukaa muda mrefu katika bendi hiyo kufuatia masharti magumu na pia haikuwa na fedha za kuwalipa, maonyesho yake yalikuwa machache sana ambayo karibu yote yalifanywa vijijini.

Wanamuziki hao watano wakakimbilia kwenda mji mkuu wa Tanzania Dodoma. Wakati walipokuwa safarini kwenda Dodoma na kujiunga na bendi ya Materu Stars, kwa bahati mbaya hawakupata nafasi ya kufanya onyesho lolote kutokana na tatizo la kukosekana kwa vyombo.

Wakati wakihangaika siku moja wakatembelewa na mwanamuziki Kasaloo Kyanga wakiwa mazoezini. Kasaloo aliwaambia kuwa wanahitajika tena mjini Iringa ambako kulikuwa na bendi ikitarajiwa kuazishwa.

“Mtafuta hachoki akichoka kaisha pata” mseomo huu ulijionesha wazi baada ya Ngolika na wenzake wakaamua karudi Iringa, wakaanzisha bendi ya Living Light mwaka 1993 mwishoni.Bendi ihiyo ilianza kupiga katika hoteli ya Living Light, iliyokuwepo eneo la Wilolesi mjini humo.

Bendi yao hatimaye ikapata mkataba wa kupiga muziki Dodoma Hoteli, tatizo lilikawa kwa mmiliki wa bendi aliyetoa amri kuwa wanamuziki wapige muziki bila kulipwa chochote hadi pale atakaporudisha fedha alizonunulia vyombo.

Amri hiyo ililikuwa gumu wakikumbuka kuwa hakukuweko na makubaliano yoyote kati ya wanamuziki na mwenye mali katika mkakati wa kununua vyombo.Kafuatia haIi hiyo ikalazimu wanamuziki waondoke kwenye bendi hiyo baada ya kufanyaka ‘Varangati’ kubwa.

Wakapata taarifa kuwa kuna shirika lilioitwaTACOSODE lilikuwa na vyombo vya muziki, hivyo kundi hilo lilijiunga na na kutengeneza bendi ya TACOSODE mwaka 1995.

Anania aliweza kuendeleza bendi hiyo hadi mwaka 2002, vyombo vyao vilipo chakaa kufika hali ya kutoweza kutumika tena.Tahfif katika maisha yalianza kuonekana baada ya kujiunga katika bendi ya Tango Stars, ambapo walikuwa wakilipwa mishahara. Lakini ghafla mwenye bendi akaamua kushusha mishahara yao.

Wanamuziki hao wakawa hawana jinsi ila kuiacha bendi hiyo ambapo Anania akahamia katika bendi ya Karafuu huko Zanzibar.Anania Ngolika aliamua kwenda kujiunga katika bendi ya Kalunde inayoongozwa na Deo Mwanambilimbi ambako ndiko yuko mpaka sasa.

Kwa makala haya natumani mpendwa msomaji utakuwa umemfahamu Anania Ngolinga, jinsi alivyofanya kila aina ya jitihada kutimiza malengo yake ya kuwa mwanamuziki pasipo kukata tamaa. “Penye nia pana njia”

Hili ni fundisho tosha kwa wanamuziki wanaochipukia kuto bweteka baada ya kutoa single moja!


Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba 0784331200 na 0713331200.



from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2q9OA3J
via

Post a Comment

0 Comments