Ticker

10/recent/ticker-posts

MSANII RAY C ALITUMBUKIA KWENYE DAWA ZA KULEVYA, AKAJINASUA.

Na Moshy Kiyungi,Tabora.

Oktoba, 2019.


“Kizuri hakikosi kasoro” msemo huu wa Kiswahili umejidhihirisha wazi kwa msanii Rehema Chalamila, ambaye ni mrembo mwenye sifa zote za kike, anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii la Ray C.

Aliwahi kujitumbukiza kwenye ‘janga’ la matumizi ya dawa za kulevya, lakini baadaye aliamua kujinasua kwa kuachana nayo.

Ray C ni msanii wa muziki wa Bongo Fleva, aliyejaaliwa kuwa na umbo la kupendeza, sauti nyororo, sura nzuri inayopambwa na macho yenye mvuto.

Uhodari wake wa kuzinyonga nyonga umemfanya kuwa maarufu ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.

Rahema alizaliwa mkoani Iringa, Mei 15, 1982, amejaaliwa kuwa uwezo mkubwa wa kuimba muziki wa R&B, dansi, Afro-Jazz, Taarab hata Bongo-Bhangra.

Kabla ya kujihusisha na muziki, aliwahi kufanya kazi ya utangazaji wa redio ya Clouds Fm ya jijini Dar es Salaam.Mwaka 2003 Ray C alitoka na albamu yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la ‘Mapenzi Yangu’.

Msanii huyu aliendelea kujulikana zaidi baada ya kuachia vibao vingine kadhaa kama vile, Sikuhitaji, Mapenzi Yangu, Nawewe Milele, Ulinikataa na nyingine nyingi zilizompa umaarufu zaidi.Juhudi zake katika muziki, hatimaye Ray C akatokea kuwa mwimbaji maarufu aliyeutingisha muziki wa Bongo Fleva kati ya miaka ya 2003 na 2009.

Sifa zake nzuri zikatambaa kila kona, lakini akaja kuzichafua baada ya kuingia matatani, kiafya alipoanza kutumia dawa za kulevya.

Dawa hizo zilimtesa kwa kipindi kirefu hadi mwaka 2012, ambapo Rais wa Tanzania wakati huo, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alimpa msaada wa fedha kwa ajili ya matibabu yake.

Alianza matibabu bila kuchelewa na mara baada ya kupona, msanii huyo Rehema Chalamila a.k.a Ray C, alikwenda kumtembelea Rais Dkt. Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kumshukuru kwa msaada wa matibabu aliompatia wakati alipokuwa mgonjwa.Katika ziara hiyo Ray C alifuatana na mama yake mzazi Margaret Mtweve na dada yake Sarah Mtweve.

Akiwa Ikulu, alimweleza Rais Kikwete kuwa afya yake imeimarika na kwamba muda si mrefu atarejea jukwaani kukonga nyoyo za washabiki wake waliokuwa wamemkosa kwa kipindi kirefu.

Kwa apande wake, mama mzazi wa Ray C, alimshukuru Rais kwa kuokoa maisha ya bintiye.Mama huyo akatoa wito kwa watu wanaokusanya michango kwa ajili ya matibabu ya Ray C, waache kufanya hivyo kwani yamegharamiwa na Rais Kikwete.

Kwa mujibu wa maelezo kutoka Ikulu, Rais alimpongeza Ray C kwa kuikubali hali yake ya kiafya, pia kukubali kupata matibabu ambayo alikuwa akiendelea nayo chini ya uangalizi maalum.

Lakini kama Waswahili wasemavyo kuwa “Sikio la kufa halisikii dawa”, katika hali ya kushangaza na kusikitisha, Ray C, alikumbwa na mikasa mingi ukiwemo wa mwaka wa 2016, ikaripotiwa kwamba amerudia tabia yake ya kutumia dawa za kulevya!

Taarifa hizo zilipomfikia Rais Kikwete, zilimsikitisha na kumkera sana.

Licha ya matatizo yake hayo, Ray C, alifanya kazi kwa kuachia albam za Mapenzi Yangu ya mwaka 2003, na Wewe Milele ya mwaka 2004, Sogea Sogea ya mwaka 2006 na Touch Me ya 2008.

Ray C, alikwisha twaa Tuzo kadhaa katika kazi zake, zikiwemo za msanii bora wa kike kwa mwaka 2004.Ray C alishiriki na kufanikiwa kupata tuzo za Msanii bora Afrika ya Mashariki mwaka 2005, shindano lililoandaliwa na Channel O Music Awards.

Mwaka 2006 kampuni ya Pearl of Africa Music Awards, ilimtunuku tuzo ya Msanii bora wa kike Tanzania.Aidha alitwaa tuzo ya msanii Bora wa kike kutoka Uganda na Tanzania na mwaka 2007.

Ray C alinyakua tuzo ya Msanii bora wa kike Tanzania mwaka 2007 na 2008, zilizotolewa na Pearl of Africa Music Awards.

Mwaka 2011 Tanzania Music Awards ilimpa tuzo kwa Video bora, Wimbo bora, Wimbo bora wa Afro Pop na Wimbo bora wa kushirikishwa wa 'Mama Ntilie', akishirikiana na Gelly wa Ryme & AT.

Ray C katika baadhi ya kazi zake aliwahi kuwashirikisha wasanii wengine kama Dknob, Chid Benz, Mheshimiwa Temba, Squeezer pamoja na Nako Nako.

Mapema Januari 02, 2018 msanii huyo wa muziki wa Bongo Fleva Rehema Chalamila (Ray C), alimuomba Rais John Pombe Joseph Magufuli kupitisha sheria kama aliyofanya Sultan Qaboos wa Oman.

Rayc C aliaandika ombi hilo kupitia ukurasa wake wa instagram 

“Mzee mi na shida Moja! hawa wanaume hapa nchini wanajifanya wajuaji Sana! Ombi langu la mwaka huu kwako ni hili! Naomba upitishe sheria kama ya Sultan Qaboos wa Oman! Hakuna mahusiano ya Kimapenzi kati ya mwanamke na mwanaume mpaka wafunge ndoa! 

“Na yeyote atakaekutwa na mwanamke iwe hotelini! Guest house bila Cheti cha ndoa wapelekwe wote segerea! Nadhani itasaidia sana wanawake wengi kuolewa badala ya kuwa manungaembe! Utakuwa umewanyoosha kisawasawa hawa Wanaume zetu. Tutaheshimiana! 

Msanii huyo mkongwe wa muziki wa Bongo fleva Rehema Chalamila maarufu kama Ray C, alimuanika kwenye mitandao ya kijamii mpenzi wake mpya.

Ameshawahi kuwa kwenye mahusiano na Rapa Lord Eyes, ametumia ukurasa wake wa Instagram kumtambulisha mpenzi wake huyo.

Kila la heri Rehema Chalamila aka Ray C, baadhi ya wadau wa muziki huo wanakusihi kuachana kabisa na dawa za kulevya.


Makala hii imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa mitandao ya kijamii.
Mwandaaji wa makala hii anapatikana kwa namba: 0713331200, 0736331200, 0767331200 na 0784331200.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/33Ymkji
via

Post a Comment

0 Comments