Ticker

10/recent/ticker-posts

HIFADHI MBILI ZA TAIFA ZAZINDULIWA MKOANI KAGERA

Abdullatif  Yunus wa Michuzi TV.

Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe ni Hifadhi mbili nyingine zilizozinduliwa rasmi mnamo Novemba 28, Mwaka huu, na hivyo kufanya  idadi ya Hifadhi za Taifa  kufikia 22 mpaka sasa.

Tukio hilo kubwa na la kihistoria katika sekta ya Utalii, limefanyika katika Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera Chini ya Waziri mwenye dhamana Dkt. Hamisi Kigwangala (MB), huku likihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo  wajumbe Wa kamati ya Bunge ya Uwekezaji, Maafisa wa Shirika la TANAPA, Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Adoloph Mkenda, Viongozi wengine wa Chama, Dini na Serikali pamoja na wananchi.
Katika kuhakikisha Utalii unazidi kuimarishwa Mkoani Kagera hususani katika Wilaya za Karagwe na Kyerwa,

Waziri  wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala amesema suala la kulinda Hifadhi pamoja na wanyama wake ni jukumu la kila mwanchi anaepatikana katika eneo husika, hivyo wananchi pamoja na Taasisi husika hawana budi kuendelea kuweka miundo mbinu wezeshi pamoja na kuweka vivutio vingine kwa watalii ili kuwanfanya waendelee kufika katika Hifadhi hizo.

Aidha Waziri Kigwangala ameelekeza kujengwa kwa kituo cha utamaduni chenye vyumba walau kumi kwa kuanzia, kituo ambacho amewaelekeza TANAPA kukijenga kati ya Omugakorongo hadi Murongo, ili kusaidia kurahisisha safari ya Watalii kujifunza na kujionea mambo mengine ya kiutamaduni, wanapokuwa safarini kuelekea katika Hifadhi za Ibanda na Rumanyika, na kwa kufanya hivyo Itamsaidia pia mwananchi mmoja mmoja kunufaika na uwepo wa Hifadhi katika maeneo yao.

Kwa upande wake Msimamizi wa Hifadhi hizo Bwana Allen Kijazi amesema pamoja na changamoto baadhi wanazokabiliana nazo kama TANAPA, pia wapo na mpango wa kukarabati uwanja wa Ndege uliokuwa zamani ukitumiwa na Wakimbizi, na kusema kuwa baada ya kukamilika kwa Uwanja huo unaopatika Wilayani Kyerwa, utarahisisha huduma ya Usafiri wa anga kwa watalii na wawekezaji, licha ya kuwa tayari wameanza pia uchongaji wa barabara zinazoingia na kutoka hifadhini.

Mwenyeji katika Shughuli hiyo ya uzinduzi wa Hifadhi za Taifa, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Ndg. Rashid Mwaimu amesisitiza zaidi juu ya kuendelea kutunza kulinda na kuhifadhi rasilimali zote za Wilayani Kyerwa, Hifadhi ya Ibanda ikiwa ni mojawapo na huku akitangaza vita dhidi ya majangili wanaofikiria kuhujumu Hifadhi na rasilimali nyinginezo kwa namna yoyote
Pichani ni Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala (MB), akiwa amesimama katika jukwaa maalumu kabla kupokea heshima, kabla ya ukaguzi wa gwaride katika onesho lilifonywa na Jeshi USU, katika Uzinduzi wa Hifadhi za Taifa za Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe.
 Pichani Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Ndg. Rashid Mwaimu akitoa salaam zake kwa Wananchi na Viongozi (hawapo pichani) wakati wa Uzinduzi wa Hifadhi za Taifa za Ibanda na Rumanyika..
 
 Pichani ni Gwaride kutoka Jeshi USU likiendelea kunogesha Uzinduzi wa Hifadhi za Ibanda na Rumanyika katika Shughuli ya Uzinduzi rasmi wa Hifadhi hizo uliofanyika Wilayani Kyerwa.
 Pichani ni Picha ya pamoja ya Mgeni rasmi, Viongozi, pamoja na baadhi ya  Watumishi wa TANAPA wakati wa Uzinduzi wa Hifadhi za Taifa za Ibanda na Rumanyika.
Pichani ni sehemu ya Burudani kutoka TANAPA BAND ikiendelea kuburudisha katika uzinduzi wa Hifadhi za Taifa za Ibanda na Rumanyika.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2Y2ATQL
via

Post a Comment

0 Comments