DKT KALEMANI ATANGAZA NEEMA NYAMAGANA

  Masama Blog      
Veronica Simba - Mwanza

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuwaunganishia umeme wananchi wa mitaa 14 ya Kata ya Lwanima na mitaa 9 ya Kata ya Buhongwa, wilayani Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, kwa gharama ya shilingi elfu 27 pekee sawa na miradi ya umeme vijijini.

Alitoa maagizo hayo Novemba 19 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo, ambapo aliwasha rasmi umeme katika Mtaa wa Mwang’haranga.

Akizungumza na wakazi wa eneo hilo, Waziri Kalemani alisema neema hiyo ya kuunganishiwa umeme wa elfu 27 imewafikia kutokana na mpango unaotekelezwa na serikali katika maeneo yaliyoko pembezoni mwa miji, yenye kushabihiana na vijiji, maarufu kama Peri-Urban.

“Kwakuwa maeneo haya yanashabihiana na vijiji, mtaunganishwa kwa bei ya vijiji. Mumshukuru sana Rais Magufuli kwa kuendelea kuwapigania wananchi wanyonge na kuhakikisha wanapelekewa huduma za maendeleo.”

Aidha, Waziri alimpongeza Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula, ambaye alimwelezea kuwa amepambana sana kuhakikisha wananchi wa maeneo husika wanapata nishati ya umeme kwa gharama hiyo nafuu.

Aliwataka TANESCO kukamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi ujao wa Desemba ili kuwawezesha wananchi hao kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka wakiwa na umeme.Kwa upande wake, Mbunge Mabula aliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa usikivu wa changamoto za wananchi na utatuzi wa haraka.

Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alifanya ziara wilayani Magu ambapo aliwasha umeme katika vijiji vya Mahaha na Nyasato huku akitilia mkazo taasisi za umma kuunganishwa na nishati hiyo kwa ajili ya uboreshaji wa huduma kwa wananchi.

Aliwataka viongozi wa Halmashauri za Wilaya na Vijiji kuhakikisha taasisi zote za umma zilizo katika maeneo yao, zinaunganishiwa umeme. “Hilo litatekelezeka ikiwa ninyi viongozi mtatenga fedha na kulipia gharama za kuunganishwa ambazo ni shilingi elfu 27 tu,” alisisitiza.

Akiwa katika Shule ya Msingi Nyasato (eneo ambalo waliishi babu na bibi yake), Dkt Kalemani alilipa kwa TANESCO shilingi elfu 27 ikiwa ni gharama za kuiunganishia umeme shule hiyo ambayo tayari ilikwishatandaza mfumo wa nyaya (wiring). Aliagiza umeme uunganishwe siku hiyohiyo.

Kwa nyakati tofauti, Waziri alipongeza jitihada zinazofanywa na Mbunge wa Magu, Desdery Kiswaga, katika kuhakikisha wananchi wake wanapata nishati ya umeme kwa ajili ya maendeleo yao.

Naye Mbunge huyo alipongeza uchapakazi wa Dkt Kalemani huku akimpambanua kuwa mmoja kati ya mawaziri wachapakazi, wenye weledi na kasi ya kazi katika Serikali inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli.

Alimwomba Waziri kufikisha salamu za shukrani za wana-Magu kwa Rais Magufuli kutokana na namna anavyowapigania katika masuala ya kimaendeleo.Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dkt Philemon Sengati, alimpongeza Waziri Kalemani kwa kutekeleza agizo la Rais Magufuli la kusitisha uagizaji nje wa vifaa mbalimbali vya umeme zikiwemo transfoma na kutumia vinavyozalishwa nchini.

Alisema kwa kutumia vifaa vya ndani, kumekuwa na mabadiliko chanya ya zoezi la uunganishaji umeme katika maeneo mbalimbali tofauti na ilivyokuwa awali.

Katika ziara hiyo, Waziri alifuatana na viongozi mbalimbali waandamizi kutoka wizarani, TANESCO na REA.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akiwasha umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Nyasato, wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, akiwa katika ziara ya kazi, Novemba 19, 2019.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyasato iliyopo wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza akiwa katika ziara ya kazi, Novemba 19, 2019. Waziri aliagiza shule hiyo iunganishiwe umeme siku hiyohiyo.
 Baadhi ya watoto wakazi wa Buhongwa mkoani Mwanza, wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza na wananchi wa eneo hilo akiwa katika ziara ya kazi, Novemba 19, 2019.

 Wananchi wa kijiji cha Mahaha, wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao kabla ya kuwasha rasmi umeme, Novemba 19, 2019.

 Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (wa pili-kulia), akimwonesha Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa tatu-kulia), baadhi ya mitaa ya Buhongwa, wilayani humo ambayo inashabihiana na vijiji na haijafikiwa na umeme. Waziri aliiagiza TANESCO kuipelekea mitaa hiyo umeme wa elfu 27 sawa na inavyotozwa vijijini. (Novemba 19, 2019)

 Mbunge wa Magu, Desdery Kiswaga, akizungumza wakati wa hafla ya kuwasha rasmi umeme kijiji cha Mahaha, wilayani humo. Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani aliwasha rasmi umeme katika kijiji hicho, Novemba 19, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dkt Philemon Sengati, akizungumza wakati wa hafla ya kuwasha rasmi umeme kijiji cha Mahaha, wilayani humo. Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani aliwasha rasmi umeme katika kijiji hicho, Novemba 19, 2019.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/333R8ha
via
logoblog

Thanks for reading DKT KALEMANI ATANGAZA NEEMA NYAMAGANA

Previous
« Prev Post