Ticker

10/recent/ticker-posts

DC NDEJEMBI AGAWA MICHE LAKI NNE YA KOROSHO KWA WAKULIMA


Charles James, Michuzi TV

MKUU wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Mhe Deo Ndejembi amegawa mbegu za Korosho kiasi cha tani tatu kwa wakulima ikiwa ni jitihada ya kukuza zao hilo wilayani humo.

DC Ndejembi amesema wamegawa mbegu hizo baada ya kukaa kikao kikubwa ambapo waliazimia kuanza kilimo cha korosho ndani ya Wilaya hiyo ikiwa ni mkakati wa kukuza uchumi wa wananchi na Serikali ndani ya Halmashauri yao.

Amesema mbegu hizo ziliagizwa na Mkurugenzi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Mhe Job Ndugai ambapo amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuondokana na kilimo cha mazoea na kujikita sasa katika kufanya kilimo chenye tija na maendeleo.

" Tunatambua Kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa letu, na sisi Kongww tumedhamiria kwa dhati kabisa kupiga hatua kubwa kupitia zao hili la korosho. Tumefanya utafiti na kugundua ardhi yetu ni rafiki kwa zao hili hivyo hatuna budi kuchangamkia fursa hii.

Lengo kubwa ni kuwainua wananchi wetu kiuchumi na kupitia kampeni yetu ya Ondoa Njaa Kongwa (ONJAKO) tumeamua sasa kuongeza zao la korosho na kila kaya itabidi ilime ekari mbili," Amesema DC Ndejembi.

Jumla ya miche za korosho zinazohitajika ni miche Milioni mbili na laki mbili lakini kiasi walichoamua kuanza nacho kwa kugawa ni miche Laki nne ambapo kila kaya itaanza kupanda ambapo baada ya wiki nne watagawa tena miche Laki nne.

DC Ndejembi amesema wao kama Wilaya wamedhamiria kuhama kutoka kufanya kilimo cha kujitegemea na kwenda kwenye kilimo cha biashara ili kumuunga mkono Rais Dk John Magufuli katika kunyanyua uchumi nchini na kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.

" Rais wetu anahimiza sana katika kukuza uchumi kupitia viwanda hivyo ni lazima sisi wasaidizi wake kuwahamasisha wananchi wetu kutoka kwenye kilimo cha kujikimu kwenda kwenye biashara maana viwanda hivi ambavyo Serikali ya Dk Magufuli inajenga vitahitaji malighafi ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na kilimo.

Hivyo sisi kama Kongwa tumeona njia pekee ya kufanikisha hilo ni kuwafanya wananchi wetu walime kwa wingi korosho kwa sababu licha ya wao kufaidika kiuchumi lakini pia watakuza mapato kwa serikali," Amesema DC Ndejembi.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi akigawa miche ya korosho kwa wananchi wa Wilaya hiyo. DC Ndejembi amesema lengo lao ni kufanya kilimo cha kibiashara.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2NrPxNP
via

Post a Comment

0 Comments