CWT KUJENGA OFISI ZA WILAYA 40

  Masama Blog      
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kinatarajia kukamilisha ujenzi wa ofisi za CWT za wilaya 40 ili kuboresha utendaji kazi wa walimu wa sehemu mbalimbali hapa nchini. 

Katibu mkuu wa CWT, Deus Seif aliyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya mwalimu wilayani Simanjiro mkoani Manyara. 

Seif alisema hadi mwezi Aprili mwakani, ofisi 40 ikiwemo ya CWT Simanjiro zitakuwa zimejengwa ili kuondokana na adha ya kupanga ofisi wakati uwezo wa kujenga ofisi wanao.

"CWT ni taasisi kubwa ya tatu nchini ukiondoa Kanisa Katoliki na CCM, hivyo lazima tujenge ofisi ili yasitupate mambo ya majengo tunayopanga yakiuzwa na sisi tunauzwa huko huko," alisema. 

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula alisema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kimepanda wilayani humo kupitia walimu. 

Mhandisi Chaula alisema kiwango cha ufaulu wilayani Simanjiro kwa shule za msingi mwaka 2017 kilikuwa asilimia 49.96 na mwaka jana ilikuwa asilimia 69.01.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi alisema wana miaka mitatu kwenye wilaya hiyo na wamefanikisha uanzishwaji wa shule mbili za sekondari za kidato cha tano na sita. 

"Tunatarajia kuanzia shule nyingine ya tatu ya kidato cha tano kwenye tarafa ya Moipo pia tumeanzisha chuo cha Veta kilichopo Emboreet kupitia ufadhili wa mdau wa maendeleo Peter Toima," alisema Myenzi. 

Mwanachama wa heshima wa CWT, Peter Toima alisema kupitia shirika lake lisilo la kiserikali la ECLAT Foundation, anajitolea matofali 3,000 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya CWT Simanjiro. 

Toima ambaye kitaaluma ni mwalimu alisema yeye ni mdau wa elimu ndiyo sababu huwa anashirikiana na serikali kuunga mkono maendeleo mbalimbali ikiwemo kujenga madarasa ya shule. 

Katibu wa CWT wilaya ya Simanjiro, mwalimu Nazama Tarimo alisema Simanjiro ina walimu 892 wakiwemo 622 wa shule za msingi na 270 wa shule za sekondari. Tarimo alisema katika awamu ya tano ya serikali ya Rais John Magufuli, walimu 249 wamepandishwa madaraja kati ya walimu 355 waliokasimiwa kupandishwa. 

Hata hivyo alisema tayari walimu 222 wamebadilishiwa mishahara yao hadi mwezi Oktoba, bado walimu 106.
Katibu Mkuu wa CWT, mwalimu Deus Seif (katikati) akikagua eneo litakalojengwa ofisi ya chama hicho Wilayani Simanjiro.
Katibu Mkuu wa CWT, mwalimu Deus Seif akipokewa na walimu wa Mkoa wa Manyara, alipofanya ziara ya siku moja wilayani Simanjiro.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2KaK6AE
via
logoblog

Thanks for reading CWT KUJENGA OFISI ZA WILAYA 40

Previous
« Prev Post