Ticker

10/recent/ticker-posts

CHUO CHA CBE CHAPATA HATI SAFI KUTOKA KWA CAG

 Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Injinia Stela Manyanya akizungumza kwenye mahafali ya 54 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Kampasi ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Naibu Waziri aipongeza CBE kwa kupata hati safi

 Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara, Profesa Emanuel Mjema akizungumza kwenye mahafali ya 54 ya chuo hicho mwishoni mwa wiki ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stela Manyanya ambapo wahitimu walikuwa 2,439 katika fani mbalimbali kwa kiwango cha Astashahada, Stashahada, Shahada na Shahada za Uzamili.
Wahitimu wa fani mbalimbali katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Dar es Salaam wakimsikiliza Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Injinia Stela Manyanya kwenye mahafali ya 54 ya chuo hicho mwishoni mwa wiki.


Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imepongeza mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Chuo cha Biashara cha CBE katika maendeleo ya taaluma na miundombinu tangu kuanzishwa kwake miaka 54 iliyopita.

Pia imepongezwa kwa kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu zake kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).

Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya kwenye mahafali ya 54 ya chuo hicho yaliyofanyika Kampasi ya Dar es Salaam.

Kwenye mahafali hayo wahitimu walikuwa 2,439 katika fani mbalimbali kwa kiwango cha Astashahada, Stashahada, Shahada na Shahada za Uzamili.

Manyanya aliwapongeza kwa kukarabati jengo la utawala katika kampasi ya Dar es salaam na kuanzisha ukarabati mwingine wa jengo la Cafeteria ambalo baada ya kukamilika litakuwa na maktaba kubwa ya kisasa na kumbi za mihadhara kwa kutumia fedha za ndani.

“Nimeelezwa na pia nilipata fursa ya kutembelea na kujionea eneo hilo kubwa lenye Majengo ya kutosha yanayohitaji kufanyiwa ukarabati katika kampasi ya Mwanza,”

“Pia nawapongeza kwa maendeleo mazuri ya mradi mkubwa wa ujenzi wa hostel katika Kampasi za Dar es Salaam na Dodoma ambao mchakato wake unaendeshwa na Benki ya Dunia kwa ajili “Public Private Partnership” (PPP) umefikia mahali pazuri,” alisema.

Waziri aliwapongeza pia kwa kusimamia Mapato na Matumizi ya fedha za Chuo na kupata hati safi za Mkaguzi Mkuu wa fedha za Serikali (CAG), pamoja na hati safi katika manunuzi ya umma kutoka Public Procurement Regulatory Authority (PPRA), ambapo mwaka huu CBE imeshika nafasi ya pili na kupata hati safi katika manunuzi ya umma.

Alisema CBE imepanda kwenye ubora wa vyuo vikuu, yaani “University ranking”, kutoka nafasi ya 53 hadi ya 15 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mkuu wa chuo cha CBE, Profesa Emanuel Mjema chuo kinaendelea kuwasomesha wanataaluma wake kufikia kiwango cha shahada ya uzamili na uzamivu PhD kwa kutumia fedha za ndani.

Alisema pamoja na jitihada za chuo kuwasomesha wahadhiri wake hivi sasa kinawanataaluma 16 tu wenye shahada za uzamivu na kati ya wahadhiri 178 na kwamba mpaka sasa wanasomesha wahadhiri 44 kwa ngazi ya uzamivu na sita uzamili.

Profesa Mjema aliipongeza serikali kwa kutoa vibali vya kuajiri wahadhiri mara kwa mara ingawa idadi ya wanachuo waliopo chuo kinahitaji kuwa na wahadhiri 240 wakati waliopo ni 178 tu.

Alisema hali hiyo inasababisha kuwepo kwa changamoto katika kutoa taaluma na kufanya tafiti mbalimbali nan chi inapoelekea kwenye uchumi wa viwanda tafiti mbalimbali zinahitajika kwenye sekta ya biashara.

Pia Profesa Mjema aliipongeza serikali kwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wote wa CBE hali inayosababisha chuo hicho kujiendesha vizuri kwani kazi kubwa ya vyuo ni kufundisha, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Alisema chuo kimetuia fedha za ndani kimefanikiwa kukarabati majengo yake katika kampasi zake Dar es Salaam na Dodoma na kuanzisha ujenzi mwingine wa maktaba ya kisasa ambalo litakuwa na kumbi za mihadhara.

Profesa Mjema aliishukuru serikali kwa kufanikisha mchakato wa mradi mkubwa wa ujenzi wa hosteli katika kampasi ya Dar es Salaam na Dodoma ambao umefikia pazuri.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2KsWpIQ
via

Post a Comment

0 Comments