CCM YAPITA BILA KUPINGWA KWENYE VIJIJI 6,248 NA MITAA 1,169, WALIOENGULIWA SASA KUSHIRIKI UCHAGUZI HUO

  Masama Blog      

Charles James, Michuzi TV

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kupita bila kupingwa kwenye maeneo mbalimbali nchini katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kutokana na kukosekana kwa wagombea wa upinzani kwenye maeneo hayo.

CCM imepita bila kupingwa katika vijiji 6,248 kati ya vijiji 12,319 sawa na asilimia 51 ambapo kwa upande wa mitaa wamepita bila kupingwa katika mitaa 1,169  kati ya mitaa 4,262 sawa na asilimia 27 huku kwenye vitongoji wakipita kwa asilimia 58.

Akizungumza jijini Dodoma leo wakati akitoa taarifa ya zoezi la uchukuaji fomu, urudishaji, uteuzi, pingamizi na rufaa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amewataka pia wagombea ambao walichukua fomu na kuzirejesha basi washiriki uchaguzi huo ifikapo Novemba 24 ambapo pia amefuta  maamuzi ya kuwaengua wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo.

Waziri Jafo amesema licha ya vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo kutangaza kujiondoa kwenye uchaguzi huo bado wagombea wao waliendelea kurudisha fomu ba kufuatilia rufaa zao jambo ambalo linaonesha jinsi gani wanavyohitaji kushiriki uchaguzi huo lakini wananyimwa haki yao na vyama vyao.

" Hata kabla ya zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu halijafungwa bado kuna wanachama walikua wanarudisha fomu na kuendelea na mchakato, hii inaonesha jinsi gani ambavyo watu wanahitaji kushiriki uchaguzi huu wa kidemokrasia lakini wananyimwa fursa hiyo na vyama vyao.

Sasa safari hii hakuna kurudisha Mpira kwa kipa, hivyo kupitia kanuni no 52 ninatoa muongozo kwamba wagombea wote ambao waliteuliwa na kudhaminiwa na vyama vyao na kufanikiwa kurejesha fomu zao za uteuzi kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi wana sifa ya kupigiwa kura na wananchi katika uchaguzi huu kulingana na maeneo wanayogombea," Amesema Mhe Jafo.

Amesema kwa kuwa imeonekana wazi wananchi kutoka vyama mbalimbali wamekua na nia kubwa ya kushiriki uchaguzi huo licha ya vyama vyao kutokueka umuhimu katika kuwaelekeza wanachama wao mambo muhimi, Mamlaka ya uchaguzi imeona ni vema kutoa nafasi kwao kushiriki kwani imejiridhisha licha ya vyama hivyo kujitoa bado wanachama wao waliendelea na mchakato wa zoezi la urejeshaji wa fomu.

Waziri Jafo amesema mambo pekee ambayo yanaweza kumuengua mtu kwenye uchaguzi huo ni kutokua Raia wa Tanzania, Kutojiandikisha katika Kijiji, Mtaa au Kitongoji husika, Kujiandikisha mara mbili, Kutodhaminiwa na Chama chake cha Siasa, Wagombea zaidi ya mmoja kutoka Chama kimoja kurejesha fomu katika nafasi moja.

Amesema katika zoezi hilo la uchukuaji na urejeshaji wa fomu kulikua na changamoto kubwa kwa wagombea wengi kufanya makosa ya kikanuni yaliyopelekea kutoteuliwa.

" Ndugu zangu kulikua na makosa mengi katika zoezi hili la urejeshaji fomu, baadhi ya makosa hayo ni pamoja na kujidhamini wenyewe, kutojaza fomu namba IV, kutofautiana kwa majina, kutojaza fomu kwa ukamilifu, kukosea umri ambapo makosa hayo yalitokana na vyama kushindwa kuwajibika katika kuwaelekeza wanachama wao jambo ambalo limesababisha zaidi ya mapingamizi 15, 380 kuwasilishwa," Amesema Jafo.

Amesema msimamizi wa uchaguzi ataanza kupokea ratiba za kampeni kutoka vyama vyao Siasa kuanzia Novemba 10 hadi 11 kwa ajili ya kuziunganisha.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake Dodoma leo kuhusiana na zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa litakalofanyika Novemba 24 mwaka huu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akitoa taarifa ya zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu, uteuzi, pingamizi na rufaa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/36NFday
via
logoblog

Thanks for reading CCM YAPITA BILA KUPINGWA KWENYE VIJIJI 6,248 NA MITAA 1,169, WALIOENGULIWA SASA KUSHIRIKI UCHAGUZI HUO

Previous
« Prev Post