Ticker

10/recent/ticker-posts

Benki ya Exim Yazidi kujitanua zaidi, Yaingia Ethiopia.

Benki ya Exim Tanzania imezidi kujitanua zaidi nje ya mipaka ya Tanzania kwa kufungua kituo cha huduma za benki hiyo (Commercial Representative Office ) katika jiji la Addis Ababa nchini Ethiopia.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Dk Bernard Kibesse wakati akifungua rasmi tawi jipya la benki ya Exim Tanzania lililopo katika mtaa wa Mkwepu jijini Dar es salaam ikiwa ni baada ya benki hiyo kukamilisha taratibu za umiliki wa iliyokuwa Benki ya UBL Tanzania. Katika uzinduzi huo, Dk Kibesse alimuwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.
Kufuatia hatua hiyo Benki hiyo inakuwa taasisi ya kwanza ya kifedha nchini Tanzania kuendesha shughuli zake kwenye mtandao wa mataifa matano  ikiwemo  Ethiopia ambayo inatajwa kuwa ndio nchi ya pili kwa ukubwa wa idadi  ya watu barani Afrika. Mataifa mengine ambayo benki hiyo inaendesha huduma zake ni pamoja Uganda, Comoros na Djibouti.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na benki hiyo jijini Dar es salaam mapema leo ilisema kwamba benki hiyo imepata leseni ya kufungua na kuwa na Ofisi ya Mwakilishi wake nchini Ethiopia kupitia tawi lake la nchini Djibouti na imepanga kuanza kazi kutoa huduma zake nchini humo hivi karibuni.
"Tunatarajia kwamba huduma zetu zitaanza  kutolewa kikamilifu mapema mwezi Disemba, 2019 kupitia Ofisi ya Mwakilishi wetu kibiashara  iliyopo katika Jengo la Zouleka LKG, ghorofa ya 2, Sub City Bole, 2160 / B. Addis Ababa. '' alisema Bw Jaffari Matundu, Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo kupitia taarifa hiyo.
Alisema upanuzi huo  wa Ethiopia unakuja kama sehemu ya mikakati wa upanuzi wa benki hiyo kwa ujumla katika kutimiza matarajio yake ya kuwa Benki ya Pan African. Aidha ufunguzi wa ofisi hiyo  ya uwakilishi utakuza mipango ya kimkakati katika kuongeza ushirikiano na nchi mbambali  za Afrika na inatoa jukwaa muhimu kwa Benki hiyo kuuza huduma zake za kipekee kwa biashara za nje.
"Hii ni hatua muhimu kwa Benki ya Exim ikiwa kama kikundi.'' Alisema Matundu  huku akibainisha kuwa ukuaji thabiti wa uchumi nchini Ethiopia ambao umechochewa na uwekezaji mkubwa wa umma na ongezeko la wateja ndio sababu nchi hiyo imekuwa kivutio kwa taasisi za kifedha kuwekeza katika taifa hilo.
Alisema kuwa Benki hiyo pia inakusudia kusaidia ufanyaji wa biashara baina ya Tanzania  na Ethiopia,  kusoma soko na fursa za uwekezaji zilizopo huku ikishiriki katika kuendesha ukuaji wa uchumi baina ya nchi hizo mbili.
Aliongeza kuwa Ethiopia imerekodi viwango vya juu zaidi vya ukuaji wa uchumi ulimwenguni kote katika miaka michache iliyopita na imeorodheshwa  miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi barani Afrika kulingana na takwimu za Shirika la Fedha Duniani (IMF).
"Tunatazamia fursa zaidi za ukuaji kupitia soko la Ethiopia, haswa kwa kuzingatia mageuzi yaliyofanyika hivi karibuni nchini humo. Tunaamini kwamba kuna fursa nyingi za ukuaji wa uchumi nchini Ethiopia, na Benki ya Exim kama kikundi tunataka kuwezesha hili. "Alisema.
Aidha ukuaji huo wa Benki ya Exim umeonesha kuivutia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambapo hivi karibuni, akifungua rasmi tawi jipya la benki hiyo lililopo katika mtaa wa Mkwepu jijini Dar es salaam ikiwa ni baada ya benki hiyo kukamilisha taratibu za umiliki wa iliyokuwa Benki ya UBL Tanzania, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Dk Bernard Kibesse aliipongeza benki hiyo huku akiahidi kuipa ushirikiano zaidi katika kufanikisha adhma yake ya kufungua matawi zaidi nje ya nchi.
“Ni fahari kwetu kuona benki ya kizalendo inafanya mambo makubwa kama haya. Mmekuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa mabenki hapa nchini jinsi inavyojizatiti kujiimarisha ndani na nje ya mipaka ya nchi.Hatua hii ni sawa na kuitikia kilio cha wadau wa huduma za kifedha hapa nchini  wanaohitaji huduma zinazokidhi mahitaji yao pia huduma zinazolingana na zile za kimataifa na kwenye mazingira yaliyobereshwa.’’ Alisema Kibesse.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2KOinpW
via

Post a Comment

0 Comments