Ticker

10/recent/ticker-posts

Abel&Fernandes, AAR waungana kutokomeza kisukari nchini

KAMPUNI ya Mawasiliano ya Abel & Fernandes imeungana na Kampuni ya Afya ya AAR na wadau wengine kwa lengo la kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kisukari ambao kwa kiasi kikubwa umeelezwa kusababishwa na mtindo wa maisha.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Abel & Fernandes, Fatma Fernandes alisema kampeni hiyo dhidi ya kisukari imelenga kuboresha huduma za afya na maisha ya watu wanaoishi na ugonjwa huo.

Alisema kampeni hiyo iliyopewa kaulimbiu ya ‘Tenda Leo, Mabadiliko ya Kesho ...tuungane kutokomeza kisukari’ imelenga kuwaunganisha wadau mbalimbali kuboresha huduma za kinga, tiba ili kudhibiti ugonjwa wa kisukari.

Alisema watatoa huduma kwa mamia ya jamii iliyokumbwa na kisukari, kutoa taarifa muhimu kuhusu kisukari na kupaza sauti kwa wale waliokosa haki zao dhidi ya ugonjwa wa sukari.

“Ugonjwa wa kisukari nchini unakua, kwa sababu hadi sasa watu zaidi ya milioni 4.2 wamebainika kuwa na ugonjwa huo. Abel & Fernandes tunaelewa tatizo hili, ndio maana tumeamua kuungana kuelimisha watu juu ya ugonjwa huo ili waweze kupata matibabu sahihi na kujua namna ya kujitunza,” alisema.

Alisema ili kufikia malengo hayo ya uhamasishaji, Abel & Fernandes inakusudia kufanya kazi na madaktari na wataalam ili kuhakikisha kuwa huduma sahihi zinatolewa katika hospitali mbalimbali kwa walioathirika na ugonjwa huo.

"Tunapaswa kuanza kwa vitendo sasa, ambapo hatua ya kwanza ni kuunga juhudi ya serikali kuboresha huduma zinazotolewa dhidi ya waathirika wa ugonjwa huo kwa kuanzisha mikakati ya kitaifa ya kuudhibiti na kuwa na ufuatiliaji wa mara kwa mara. Hii itaruhusu matumizi bora ya rasilimali, ambayo ni muhimu ikiwa mkoa utaandaa mikakati dhabhiti ya kudhibiti janga hilo,”alisema.

Aidha, naye Dk. Akil Msei kutoka AAR alisema kwa mujibu wa ripoti za Shirika la Afya Duniani (WHO) takwimu zinaonyesha kila sekunde 10 mtu mmoja mwenye kisukari hufariki duniani na zaidi ya watu 40,000 wenye kisukari Tanzania hukatwa miguu.

Alisema pia zaidi ya watu milioni 422 wana kisukari duniani hivyo kupelekea ugonjwa huu kushika nafasi ya 5 kama kisababishi cha vifo duniani.

"Ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa sugu na unaathiri watu wengi. Kuna aina mbili za ugonjwa wa kisukari; Aina ya 1 na Aina ya 2. Aina ya 2 inazuilika na hii ndio tunajaribu kushughulikia ili tuweze kuzuia kuongezeka kwa visa kama hivyo. "

Alisema kampeni hii iliyoandaliwa kwa nia ya kuboresha maisha ya watu wenye ugonjwa wa kisukari itaanza kwa muda wa mwezi mmoja kwa kushirikisha watu wa kada mbalimbali katika utoaji wa elimu dhidi ya ugonjwa huo.

“Tutakuwa na kampeni za barabara ambazo zitatembelea maeneo ya Tegeta na Kariakoo kwa kutoa huduma katika magariu maalumu ya kidijitali.

“Kampeni inaenda sambamba na Siku ya wagonjwa wakisukari Novemba 14, 2019 ambapo tutakuwa na zahanati zinazotembea pamoja na kifungua kinywa kwa wagonjwa na wadau wote.

Ungana nasi tunapopambana na Ugonjwa huu wa Kisukari. Kwa habari zaidi tembelea tovuti ya kisukari www.diabetesestanzania.com.
Mkurugenzi Mtendaji wa Abel & Fernandes, Fatma Fernandes akizungumza katika uzinduzi wa kampeni dhidi ya ugonjwa wa kisukari ambayo imelenga kuboresha na kutoa huduma bure kwa watu wanaoishi na kisukari huo nchini.
Mmoja wa wahuduma wa afya walioandaliwa na kampuni ya Abel&Fernandes pamoja na AAR akitoa huduma kwa wananchi waliojitokeza kupata huduma na elimu ya kisukari kwa kutumia vituo vinavyotembea katika barabara maeneo ya Tegeta na Kariakoo jijini Dar es Salaam.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2QrJaw1
via

Post a Comment

0 Comments