ZAIDI YA WANAFUNZI WA KIKE 150 WA SHULE ZA SEKONDARI TUNDURU WAKATISHA MASOMO KUTOKANA NA KUPATA MIMBA

  Masama Blog      

Na Mwandishi Wetu,Tunduru

ZAIDI ya wanafunzi wa kike 100 wa shule mbalimbali za Sekondari wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wamekatisha masomo  baada ya  kupata mimba kuanzia Mwezi Januari hadi Julai 2019.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amesema hayo jana, wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake mjini Tunduru kuhusiana na tatizo sugu la utoro kwa wanafunzi wa shule za  msingi na sekondari katika wilaya hiyo kongwe hapa nchini.

Alisema, suala  la mimba kwa wanafunzi wa kike katika wilaya hiyo lilikuwa kubwa,  na hali hiyo imetokana na mwamko mdogo wa jamii,wazazi kuhusu umuhimu wa elimu na hata uwajibikaji mdogo wa watu waliopewa dhamana ya kusimamia  maendeleo ya elimu katika wilaya  hiyo.

Aidha Mtatiro alisema, Mwezi Agosti wanafunzi waliopewa mimba walikuwa 25 ambapo vijana 19 wamekamatwa wakati Mwezi Septemba wanafunzi waliopata ujauzito walikuwa 19 na wanaume 16 wanashikiliwa kwa kosa  hilo.

Hata hivyo Mtatiro alisema,tatizo  hilo  sasa limeanza  kupungua  hasa baada ya kuwepo kwa mikakati na ufuatiliaji madhubuti  ambapo takwimu za vitendo vya wanafunzi wa kike kupata mimba zinaonesha mafanikio makubwa kwani  Mwezi Oktoba wasichana walioripotiwa kupata mimba ni 6 na tayari wanawashikilia vijana kadhaa ambao wametajwa na wasichana kuhusiana  na kadhia hiyo.

Alisema, baadhi ya wazazi  na vyombo vya Dola wamechangia sana kuongezeka kwa vitendo vya mimba kwa  kupoteza ushahidi  pindi watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani.

Mtatiro alitolea mfano kati ya wanaume mia moja waliowapa ujauzito wanafunzi ni kumi tu ndiyo waliofikishwa  polisi katika kipindi hicho,huku wanaume tisini hawajafikishwa katika vyombo vya sheria licha ya kutajwa kuwa ndiyo walihusika kuwapa mimba wanafunzi.

“hapa unaona ukubwa wa tatizo lilikuwepo wakati huo,wasichana  mia moja wamepewa ujauzito na kukatisha  masomo yao,lakini idadi ya wanaume waliohusika kuwapa ujauzito mabinti wetu ni kumi na tisini wako uraiani, ni jambo la kusikitisha sana kuona baadhi ya watu wanashindwa kuwajibika katika  usimamizi na utekelezaji wa majukumu yao” alisema, Mtatiro.

Alisema, ili kudhibiti vitendo vya mimba na utoro kwa wanafunzi,wilaya  imejipanga kuhakikisha vijana wote wanaomaliza shule za msingi kwa kila kijiji wanafahamika na mara  wanapochaguliwa kuanza masomo ya sekondari kutakuwa na utaratibu ambao utawezesha kufuatilia mahudhurio  ya kila  siku kwa mwanafunzi.

Kwa mujibu wake,  moja kati  mkakati  ya wilayani  kuhakikisha  watoto wote waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2019,mwaka 2020 wanakwenda sekondari na hakutakuwa na  mtoto atakayebaki nyumbani, sambamba na ujenzi wa Mabweni kwa kila shule ya sekondari.

Mkuu wa wilaya amevionya vyombo vya dola kutekeleza wajibu wake na kuwakamata wanaume wanaowapa mimba wanafunzi wa kike na kujiepusha  na tabia ya kuwa wasuluhishi wa matukio ya mimba kwa wanafunzi na watoto walio na umri chini ya miaka 18.

Pia Mkuu wa wilaya,amewaonya wazazi na walezi  atakayezuia mtoto kwenda shule atachukuliwa hatua na kusisitiza kuwa,suala la kupata elimu kwa kila mtoto ni lazima  na sio suala la hiari kama baadhi ya watu wanavyodhani.

Akizungumzia suala la wanafunzi zaidi ya 350 wa shule ya Sekondari Marumba kuacha masomo Mtatiro alisema,suala hilo ni la wilaya mzima kwani  kuna watoto wengi waliocha shule na hawajulikani waliko.

Alisema, tatizo la utoro katika wilaya hiyo linachangiwa sana na mila na desturi za wenyeji,hata hivyo ni lazima waanze kubadilika kwani elimu ndiyo jambo linalohitajika kupewa kipaumbe cha kwanza.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Marumba kata ya Marumba halmashauri ya wilaya ya Tunduru wakiimba wimbo wa shule wakati wa mahafali ya kumi ya kidato cha nne katika shule hiyo.hata hivyo zaidi ya wanafunzi 350 waliochaguliwa kuanza masomo kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 wameshindwa kuendelea na masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Mimba na utoro.from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2BVZ2hA
via
logoblog

Thanks for reading ZAIDI YA WANAFUNZI WA KIKE 150 WA SHULE ZA SEKONDARI TUNDURU WAKATISHA MASOMO KUTOKANA NA KUPATA MIMBA

Previous
« Prev Post