Ticker

10/recent/ticker-posts

WATU 145 WAAMBUKIZWA KIFUA KIKUU KWA MUDA WA MIEZI MIWILI

Mratibu wa kifua kikuu na Ukoma Hospitali ya wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole akiongea jana na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Lijombo kata ya Mbesa wakati wa Uhamasishaji wa kampeni ya uchunguzi wa kifua kikuu,kampeni inayofanyika katika vijiji vyote vya wilaya ya Tunduru. Picha na Muhidin Amri.


Na Mwandishi Wetu, Tunduru

JUMLA ya wahisiwa(watu) 754 wakiwemo wanaume 85 na wanawake 60 walifanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu,  kati ya hao 145 waligundulika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo.

Aidha, katika kampeni hiyo watoto walio na umri chini ya miaka kumi na tano waliofanyiwa uchunguzi wa kifua kikuu ni  25 na waliopima virusi vya ukimwi 145 ambapo watu 17 walikutwa  na maambukizi mapya ya VVU na  wameanzishiwa  dawa ya kufubaza makali ya ugonjwa huo na watu wanne wamefariki Dunia.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa kifua kikuu na Ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole wakati wa kampeni ya uhamasishaji na uchunguzi wa vimelea  vya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi wa kijiji cha Lijombo kata ya Mbesa  inayoendelea katika maeneo mbalimbali wilayani Tunduru.

Alisema,tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu katika wilaya ya Tunduru limekuwa kubwa  jambo lililochangia umaskini kwa baadhi ya watu wanaougua ugonjwa huo hasa ikizingatia kuwa mtu mwenye TB hasiyepata tiba sahihi hawezi kufanya kazi ya uzalishaji mali.

Alisema, kutokana na  ukubwa wa tatizo hilo ndiyo maana Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu imeanza kampeni ya kufika kila kijiji kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo kwa wananchi sambamba  na kuanzishiwa dawa kwa wale wanaobainika kuwa na TB.

Dkt Kihongole amewashauri wakazi wa kijiji  hicho kujenga nyumba bora ili kuruhusu mwanga na hewa nyingi kuingia ndani kwani vimelea vya kifua kikuu upendelea  kuishi maeneo yenye giza.

Kwa mujibu wa Kihongole,Serikali ya awamu ya tano imejidhatiti kukabiliana na adui maradhi ikiwemo ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma,na alitaja dalili za mtu mwenye  maambukizi ya TB ni kukohoa  zaidi ya wiki mbili,kupungua uzito,mtoto kulia lia,kuchelewa kukua.

Kihongole, ameitaka jamii kuacha kuwaficha watu wenye TB majumbani kwani ni sawa na kukaa na Bomu ndani, kwa sababu mgonjwa asiyepata tiba anaweza kuambukiza watu wengine kumi na tano kwa wakati mmoja na ameshauri mtu anapoona dalili hizo ni vema kwenda katika vituo vya kutolea huduma kupata ushauri na tiba.

Kwa upande wake,mtaalam wa maabara wa kutoka Hospitali ya wilaya ya Tunduru John Msami alisema,ugonjwa wa kifua kikuu ni tatizo kubwa katika wilaya ya Tunduru ambalo linahitaji nguvu ya pamoja kati ya jamii na Serikali ili kuweza kulimaliza.

Msami alisema, kati ya watu kumi wanaofika Hospitali ya wilaya na kufanyiwa vipimo kupitia makohozi,watu wawili hadi watatu wanakutwa na  vimelea vya  TB.

Hata hivyo,baadhi ya wakazi wa kijiji cha Lijombo mbali na kuishukuru Hospitali ya wilaya kuendesha  kampeni hiyo, wameomba wataalam wake wafike kila kijiji ili kufanya uchunguzi wa  ugonjwa wa kifua kikuu na magonjwa mengine ikiwemo ukimwi ambao unazidi kupoteza maisha ya watu wengi.

Mohamed Machedo na Mahamudu Yusuf walisema, kampeni ya upimaji  wa ugonjwa wa kifua kikuu imekuja wakati muafaka kwani itasaidia sana kuokoa maisha ya watu wengi ambao watapata fursa ya kushiriki ujenzi wa Taifa letu na  shughuli mbalimbali  za kujiletea kipato na hivyo kuondokana na umaskini katika familia zao.

Mahamudu Yusuf, amewaomba wataalam kuanza kutembelea vijijini  kwa ajili ya kutoa elimu juu ya ujenzi wa nyumba Bora  ambazo hazitakuwa rafiki wa wadudu wa kifua kikuu.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2BQhCHU
via

Post a Comment

0 Comments