WATOTO 350 WAKATISHA MASOMO YAO KWA SABABU MBALIMBALI

  Masama Blog      
Na Mwandishi Wetu, Tunduru

ZAIDI ya wanafunzi 350 kati ya 602 waliotakiwa kuwepo katika shule ya Sekondari Marumba kata ya Marumba Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, wameshindwa  kuendelea na masomo  yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba na utoro.

Wanafunzi hao waliokatisha ndoto zao ni wale waliochaguliwa kuanza masomo ya sekondari katika shule hiyo kuanzia  mwaka 2016  hadi  2019 ambapo waliobaki ni wanafunzi 250.

Hayo yamesemwa  jana na Mkuu wa shule hiyo Michael Kapinga, wakati akitoa taarifa ya shule katika mahafali ya kumi ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo.

Alisema,wanafunzi waliosajiliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 20
16 ambao walitakiwa kuhitimu masomo ya kidato cha nne mwaka 2019 walikuwa 144 wakiwemo wasichana 76, hata hivyo waliofanikiwa  kufika kidato cha nne ni 44 ambapo  wanafunzi  76 waliishia njiani huku idadi ya  wasichana nayo ikishuka kutoka kutoka 76 hadi  15.

Hata hivyo alisema, licha ya tatizo  kubwa la utoro kwa wanafunzi, shule imekuwa ikipiga hatua kitaaluma  japo mwaka 2018 matokeo hayakuwa ya kuridhisha sana kutokana na changamoto mbalimbali zilizotokea.

Kwa mujibu wa Kapinga,mwaka jana shule ilisajili wanafunzi 48,  kati ya hao waliofanikiwa kufanya mitihani ya kidato cha nne walikuwa 43  na  waliochaguliwa kuendelea na  masomo ya kidato cha tano ni wanafunzi 6.

Alisema, tatizo la utoro kwa wanafunzi limekuwa sugu na kuwaomba wazazi kushirikiana na serikali za vijiji na kata kukomesha tabia hiyo,  sambamba na kufuatilia maendeleo ya watoto wao na kuhakikisha wanawapa mahitaji muhimu ili kuwa kama chachu  kwa watoto kupenda shule.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo Mjumbe wa kamati ya utendaji wa Chama cha Walimu(CWT) Taifa Sabina Lipukila ameitaka jamii  ya Watu wa Tunduru kubadilika  kwa kuwekeza nguvu kubwa katika elimu, badala ya kuona ufahari wa kurithisha watoto mali ikiwemo mashamba ya  korosho.

Alisema,idadi ya watoto 350 ambao wamekatisha masomo  ni kubwa sana katika Historia ya wilaya hiyo na kusisitiza kuwa,lazima juhudi zifanyike kuhakikisha watoto hao wanarudishwa ili waendelea na masomo.

Lipukila alisema,  hata umaskini uliokithiri katika wilaya ya Tunduru umechangiwa  na kiwango kikubwa cha ukosefu wa elimu kwa wananchi wake, jambo ambalo ni lazima  jamii,wazazi na serikali za vijiji zikae pamoja ili kumaliza tatizo hilo  linaloonekana kuota mizizi.

Aidha,amewaagiza watendaji wa vijiji,kata na maafisa tarafa kuwasaka wanafunzi wanao katisha masomo ili warudi shule na kuwakamata wazazi wa wanafunzi watoro wanaowaficha watoto wao  nyumbani.

Alisema, ni aibu  kwa wilaya ya Tunduru kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaokatisha masomo hasa wakati huu ambapo Serikali ya awamu ya tano imeondoa gharama zote  kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne.

Lipukila ameiagiza Bodi ya shule, kuweka mikakati madhubuti itakayosaidia kuwarejesha watoto wote shule na wale wanaochaguliwa kuanza  kidato cha kwanza kuhakikisha hawakatishi masomo.

Sambamba na hilo ameitaka bodi ya shule,kuhakikisha inashirikiana na Serikali za vijiji kuweka utaratibu mzuri ambao utatoa nafasi ya kushirikisha wananchi wote  juu ya suala la ujenzi wa miundombinu ya shule  na sio  jukumu hilo kuachwa kwa wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule hiyo.

Naye Afisa elimu kata ya Marumba Issa Sinambe alisema, changamoto  ya wanafunzi kutomaliza elimu ya kidato cha nne inatokana na mwamko mdogo wa jamii,wazazi na wanafunzi wenyewe ambao baadhi yao wanalazimika kutembea umbali wa km 16 kwenda na kurudi shule.

Alisema, shule ya Sekondari Marumba inamilikiwa na wazazi wa kata mbili ya Marumba na Mbati, kwa hiyo kutokana na changamoto ya umbali wamejipanga kuanza ujenzi wa mabweli haraka iwezekanavyo kama hatua itakayowezesha wanafunzi hususani wa kike kuishi shuleni.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2qQo5k1
via
logoblog

Thanks for reading WATOTO 350 WAKATISHA MASOMO YAO KWA SABABU MBALIMBALI

Previous
« Prev Post