Ticker

10/recent/ticker-posts

Wambura aandika barua kwa DPP kuomba msamaha

Na Karama Kenyunko, Blogu ya Jamii.
ALIYEKUWA  Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Michael Wambura ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri makosa  yanayomkabili mahakamani hapo.

Wambura ambaye alifikishwa  kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Februari 11, mwaka huu, akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka 17 yakiwemo ya kutakatisha zaidi ya Sh. Milioni 100.

Wambura amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kelvin Mhina kuwa, ameandika barua hiyo kufuatia agizo la msamaha uliotolewa na rais hivyo ameuomba upande wa mashtaka  wafuatilie barua hiyo ili apate majibu kwa haraka.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon amedai watafuatilia suala hilo ili wapate majibu mapema.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 16,2019

Mapema, kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa kwani upelelezi wake bado haujakamilika.

Katika mashtaka hayo 17; shtaka moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004, sehemu isiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Siku hiyo, Wambura kwa nia ya kutapeli alitengeneza barua ya kughushi ambayo haina kumbu kumbu namba akionyesha imeandikwa na E Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Jeck system anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka la kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, mshtakiwa alitoa barua iliyokuwa haina kumbu kumbu namba ya Julai 6, 2004, akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, kuanzia shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia kiasi cha zaidi Sh 95 milioni, kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbali mbali na riba kutoka kwa kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa siyo kweli.

Pia katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadiawa kutenda kosa hilo, Juni 17, 2015 huko katika ofisi za TFF, ambapo kwa njia ya udanganyifu, mshtakiwa alijipayia Sh 10milioni kutoka TFF kwa kuonesha kuwa ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ha Jeck jambo ambalo siyo kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadai, kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, makao makuu ya Shirikisho hilo, alijipatia Sh 25milioni kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia, shtaka jingine utakatishaji fedha haramu, Mshtakiwa anadaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21 2015, alijipatia Sh 75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali na zimetokana na shtaka la kughushi.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2nIF1rq
via

Post a Comment

0 Comments