Ticker

10/recent/ticker-posts

Wakurugenzi wa Halmashauri Watakiwa kutenga Fedha za Kutokomeza Mazalia ya Mbu

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt Dorothy Gwajima akifungua Mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wanaohusika katika kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa Malaria nchini katika ukumbi wa Morena jijini Dodoma Meneja Mpango wa Kudhibiti Malaria nchini Dkt Ali Mohamed akizungumza kwenye mkutano huo Baadhi ya washiriki wa mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wanaojihusisha na udhibiti wa malaria nchini wakimsikiliza Dkt Gwajima leo jijini Dodoma



………………..

Na Mathew Kwembe

Wakurugenzi wa Halmashauri wametakiwa kutenga fedha katika mipango ya bajeti za halmashauri zao kwa ajili kununulia dawa ya kupulizia wadudu wanaosababisha magonjwa mbalimbali nchini ukiwemo ugonjwa wa malaria, kama mkakati mmojawapo wa kuhakikisha kuwa Tanzania inatokomeza ugonjwa huo nchini kutoka maambukizo ya asilimia 7.3 hivi sasa hadi asilimia 1 ifikapo mwaka 2030.

Sambamba na hilo, Wakurugenzi wa halmashauri wametakiwa kulipa madeni yao baada ya kuchukua dawa za kupulizia wadudu katika kiwanda cha kutengeneza dawa hizo kilichopo kibaha, mkoani Pwani.

Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt Dorothy Gwajima mara baada ya kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wanaohusika katika kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini.

Amesema hatarajii katika bajeti zijazo, kuona halmashauri hazitengi fedha kwa ajili ya kudhibiti na kutokomeza mazalia ya mbu katika halmashauri zao kwani hazitapita.

“Haitapita bajeti ya halmashauri kama haitaweka mikakati ya kudhibiti Malaria sambamba na maelekezo tuliyokuwa tukiyapeleka na mafunzo ambayo tumekuwa tukiyatoa,” amefafanua.

Dkt Gwajima ameongeza kuwa ni muhimu fedha hizo zitengwe ili zitumike katika kutokomeza mazalia ya mbu kwani wataalamu wa halmashauri wanajua ni maeneo gani ya halmashauri yenye mazalia mengi ya mbu wanaoambukiza ugonjwa wa malaria.

“Kwa hiyo lazima ionekane pale ni kiasi gani cha dawa kitaagizwa kutoka katika kiwanda chetu cha kibaha kinachozalisha dawa zinazotumika kupulizia kwenye mazalia ili kudhibiti ongezeko la wadudu hawa,” amesema na kuongeza:

“Wakurugenzi hawa walichukua hizi dawa kibaha hawajalipa, kwanza walipe deni, kisha wapange kwenye bajeti zao kuhakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika.”

Amesema kuwa ni jukumu la wataalamu kuainisha maeneo yenye mazalia mengi ya mbu ili dawa zitakazonunuliwa ziweze kutumika vizuri, badala ya kupuliza kila eneo.

Amesema kuna maeneo kwenye halmashauri ambayo yanajulikana kabisa ndiyo yenye mazalia ya mbu na kwamba dawa ikipulizwa kwenye maeneo hayo tatizo linakwenda chini.

Akizungumzia zaidi kuhusu hali ya maambukizo ya ugonjwa wa malaria nchini Dkt Gwajima amesema jitihada zinazofanyika kutokomeza ugonjwa huo nchini zinafanikiwa kwani maambukizo ya malaria nchini yamepungua hadi asilimia 7.3 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015/16.

Amesema kupungua kwa maambukizi ya malaria kumetokana na kuwepo kwa mikakati mbalimbali ya kinga pia uwepo wa dawa zinazotumika kupambana na ugonjwa huo ambapo kiwango cha matumizi yake kilifikia asilimia 98.4, huku matumizi ya kipimo cha haraka cha kupima vijidudu vya malaria (mRDTs) ikifikia asilimia 97.8, lakini pia kumekuwa na ongezeko la matumizi ya vyandarua vyenye dawa kwa asilimia 62.5 mwaka 2017 kulinganisha na asilimia 55.9 mwaka 2015/16.

Kwa upande wake Meneja Mpango wa kudhibiti Malaria nchini Dkt Ali Mohamed amesema kulingana na takwimu za mwaka 2017, mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita, Mara,Lindi, Ruvuma na Mtwara inaonekana kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria.

Amesema kutokana na takwimu hizo, maeneo hayo yanayoonekana kuwa na kiasi kikubwa cha maambukizi ipo haja ya kupelekwa mikakati ya ziada mbali na mikakati ya kawaida ya kuzuia mbu, kuhakikisha kuna vitendanishi vya kupima malaria na dawa za kutosha zina ubora unaotakiwa.

Ameitaja mikakati ya ziada ni jinsi ya kutumia dawa kinga (SP) kwa ajili ya wanafunzi shuleni, pia kutoa dawa katika maeneo ambayo malaria inapatikana kwa kipindi kichache, na mikakati mingine ambayo hufanywa na Mpango wa kudhibiti Malaria nchini.

Juhudi za kuutokomeza ugonjwa wa malaria nchini, barani Afrika na duniani kwa ujumla bado una safari ndefu kwani kwa mujibu wa taarifa ya dunia ya malaria ya mwaka 2018 inaonyesha kuwa zimeripotiwa kesi milioni 219 za malaria duniani na kusababisha vifo 435,000.

Kadhalika barani Afrika, kati ya kesi zilizoripotiwa asilimia 70 zinatoka Afrika na idadi ya vifo asilimia 71 pia inatoka barani Afrika hasa katika nchi kumi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania. Nchi nyinginezo ni Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ghana, Mali, Msumbiji, Niger, Nigeria na Uganda.



from MICHUZI BLOG https://ift.tt/32Kdu8f
via

Post a Comment

0 Comments