WADAU WA NISHATI JADIDIFU WAWEKA MIKAKATI KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI JADIDIFU KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

  Masama Blog      
 Na Said Mwishehe, Michuzi Blogu
MASHIRIKA sita ambayo yamejikita katika eneo la mabadiliko ya tabianchi yamekutana katika Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujadiliana  na kuandaa jumbe mbalimbali ambazo zinatoa elimu ya pamoja kwa jamii na Serikali namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa nishati jadidifu.

Baadhi ya washiriki ambayo wamekutana kujadili nishati jadidifu kama njia sahihi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni Jukwaa la Mabadiliko Tabianchi (FORUMCC), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Kampuni ya Habari na Teknolojia (NUKTA), Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), Climate Action Tanzania na Tangise. Ambapo mashirika hayo wamekutana chini ya ufadhili wa Shirika la Hivos ambalo linafadhili mradi wa nishati jadidifu kupitia FORUMCC.

Mratibu wa Mradi wa nishati jadidifu  kutoka FORUMCC Euphrasia Shayo amesema kutokana na tafiti zilizofanywa na taasisi hizo zinatakiwa kutengeneza jumbe kuu tatu mpaka tano ambazo zitatumiwa na mashirika hayo sita kutoa elimu kwa jamii .

Ameongeza mbali na hiyo jumbe hizo  amazo zitapelekwa bungeni na kuwaeleza wabunge vitu ambavyo serikali inapaswa kuvifanya kuhakikisha  masuala ya nishati jadidifu yanapewa kipaumbele.

Shayo amesema licha ya  kuhakikisha masuala ya nishati jadidifu yanapewa kupaumbele, Serikali ifahamu kuwa mpaka sasa  bado hali si nzuri kwa jamii kuhusu umuhimu ya nishati  hiyo,  wameamua kujipanga kwa kwenda kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari na wabunge .

"Uelewa na umuhimu wa nishati jadidifu hapa nchini bado upo chini, tunataka kwenda huko bungeni kutoa elimu ili waweze kujua na wakati tunapeleka meseji zetu na hoja iwe rahisi kwao kuzitetea, hata hivyo hawa wadau sita ambao ni mashirika yasiyo ya kiserikali yanafadhiliwa na Shirika la Hivos ambalo linatoa fedha zao kwa mashirika haya ili waweze kufanya kazi kwa pamoja na weledi," amesema.

Amefafanua katika mradi huo kila shirika lina kazi yake ya kufanya lakini zipo nyingine ambazo zitafanywa kwa pamoja, mfano za kutengeneza jumbe hizo maalum za pamoja ambazo zinatokana na tafiti mbalimbali zilizofanya  na mashirika hayo.

Ametumia nafasi hiyo kueleza kwa upande wa FORUMCC wanaangalia hali ikoje nchini kuhusu masuala ya nishati jadidifu na je Serikali inaona kuwa uwiano uliopo ni mzuri kwenye utoa wa fedha masuala ya nishati hiyo.

Wakati huo huo Mratibu wa Mradi wa kushawishi Benki ya Maendeleo ya Afrika kuelekeza uwekezaji katika sekta ya nishati Jadidifu unaotekelezwa katika nchi sita chini ya ufadhili wa Christiani Aid kupitia African Climate Justice Alliance (PACJA,) Msololo Onditi ameeleza changamoto iliyopo  sasa ni ukosefu wa  sera au  mkakati wa pamoja unaowaongoza kwenye matumizi ya nishati jadidifu.

"Ukiangalia sekta ya nishati watendaji wapo juu, mfumo wa kitaasisi wa kiserikali bado ni changamoto lakini hatuna Sera iliyosimama kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi, " amesisitiza.

Mmoja wa wadau kutoka Mtandao wa Nishati na Jinsia Tanzania(Tangesen)Thabiti Mkidadi kwa upande wake ameshauri kuwa kuna kila sababu kwa halmashauri zianze kuweka mikakati yake katika kusaidia serikali Kuu kwenye suala la nishati jadidifu.

"Utakuta halmashauri zinauwezo wa kupanga na kuweka mikakati ya kuwepo kwa nishati jadidifu lakini zinawaachia Serikali Kuu kuwawekea mipango hiyo," amesema Mkidadi.

Ameongeza kuwa wakati Serikali Kuu inaendelea  na mikakati yake katika sekta ya nishati, ni vema halmshauri nazo kuweka mkakati utakaohakikisha nishati jadidifu inatumika katika kuleta maendeleo ambapo ametoa mfano kinyesi cha binadamu inaweza kutumika kutengeneza nishati jadidifu." 
Tunaweza kupata umeme wa nishati jadidifu ya.kinyesi cha binadamu.Kuna moja ya shule ya sekondari wanatumia nishati hiyo,"amesema.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2NkLwJU
via
logoblog

Thanks for reading WADAU WA NISHATI JADIDIFU WAWEKA MIKAKATI KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI JADIDIFU KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Previous
« Prev Post