TBS Yaondoa Sokoni Vipodozi Vyenye Viambata Sumu

  Masama Blog      
Maofisa wa Shirika La Viwango Tanzania (TBS) wakichambua vipodozi vyenye viambata sumu wakati walipofanya ukaguzi wa kushtukiza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Vipodozi hivyo vimepigwa marufuku kutokana na kuwa na madhara kwa watumiaji.

Na Mwandishi Wetu 
AINA mbalimbali za vipodozi vilivyopigwa marufuku kwa matumizi ya binadamu vimeondolewa sokoni na maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza jijini Dar es Salaam.

Maofisa shirika hilo walifanya ukaguzi huo mwishoni mwa wiki kwenye maduka mbalimbali yaliyopo Kariakoo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ukaguzi huo,Mkaguzi Mwandamizi wa Shirika hilo,Mhandisi Donald Manyama, alisema wauzaji wa vipodozi hivyo wameonesha ushirikiano wa kutosha,kwani wamevitoa kwa kadri ambavyo walielekezwa.

Alipoulizwa kama kuingia nchini kwa vipodozi hivyo, kunachangiwa na kutokuwepo udhibiti wa kutosha mipakani,Mhandisi Manyama, alisema udhibiti upo wa kutosha,lakini vitu ambavyo vimepigwa marufuku nchini vinaingia kwa njia ambazo sio halali.

Alisema waingizaji wamekuwa wakitumia njia za panya kuingiza vipodozi hivyo. Alisema vipodozi walivyovikamata wamevichukua kwa ajili ya kwenda kuviharibu.

"Zoezi hili sio kwamba litaishia hapa (Dar es Salaam) baada ya kumaliza hapa tutaendelea na ratiba yetu mikoani kuondoa vipodozi hivi," alisema Mhandisi Manyama.

Alipoulizwa madhara ya vipodozi hivyo vyenye viambata sumu kwa matumizi ya binadamu,Manyama alisema vina madhara kwenye ngozi ya binadamu.

"Kwanza vinaichubua hiyo ngozi na kuifanya kuwa laini kiasi kwamba mtumiaji akifanyiwa operesheni ushonaji wake unakuwa ni mgumu," alisema na kuongeza;

"Vingine vinasababisha saratani ya ngozi, kupunguza kinga ya ngozi na kuathiri mfumo wa homoni za mwili. Hivyo tunawashauri hata watumiaji kuacha kutumia vipodozi hivyo. Wengine wanavitumia bila kufahamu, wakiona mwenzao amebadilika ngozi,wanadhani havina madhara.

Alisema wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waache kutumia vipodozi hivyo.Alitoa wito kwa wasambazaji wa vipodozi hivyo kuacha, kwani wakikamatwa watawasababishia mitaji yao kupotea na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kutozwa faini.

Lakini pia alitoa wito kwa watumiaji kuacha kuvitumia kwa sababu ni hatari kwa afya zao. Baadhi ya vipodozi vilivyokamatwa kwenye ukaguzi huo na kuondolewa sokoni ni Carolight,Movate,Coco Pulp, Diproson,Viva White, Carotone, Bronz na Eclair.

Vingine ni Citrolight, Tent Clear, Tender White, Clinic Clear, TCD, Baby Face,Light up,Dermotyl na Top Lemon. Mmoja wa wauzaji wa vipodozi hivyo, Rose Joseph, alishauri udhibiti uimarishwe zaidi mipakani,kwani kama vitaendelea kupatikana vitazidi kupata soko.

Aliipongeza TBS kwa kuendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye masoko, kwani hatua hiyo inawasaidia kujua aina ya vipodozi vilivyopigwa marufuku kutokana na kuwa na viambata sumu.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2J6yJJu
via
logoblog

Thanks for reading TBS Yaondoa Sokoni Vipodozi Vyenye Viambata Sumu

Previous
« Prev Post