TAKUKURU YAKAMATA MAPAPA 99 WA AMCOS WANAODAIWA KUDHULUMU WAKULIMA LINDI, NI UTEKELEZAJI WA AGIZO LA RAIS DKT MAGUFULI ALOTOA OKTOBA15,2019

  Masama Blog      
Na Said Mwishehe, Michuzi blog
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema inawashikilia viongozi 99 wa vyama 10 vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) pamoja na kurejesha milioni 255,598,194.00 ikiwa ni utekelezaji wa agizo walilopewa na Rais Dkt. John Pombe Joseph alilolitoa akiwa katika ziara ya kikazi katika Mkutano wa Hadhara na Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa Mjini, mkoani Lindi.
Akiwa katika ziara hiyo ya kikazi Rais Dkt Magufuli aliiagiza TAKUKURU pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo na Ushiriki, Hussein Bashe, kuhakikisha kuwa Vyama 10 vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) vinavyodaiwa na Wakulima vinawalipa wakulima husika kabla ya msimu wa Korosho kuanza, vinginevyo wahusika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa Sheria.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari leo Oktoba 19, 2019, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo amesema ofisi yake imeshatekeleza agizo hilo la Rais kwa kuwakamata Viongozi 99 wa Vyama 31 vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) vilivyowadhulumu Wakulima wa Ufuta kiasi cha Sh. 1,236,364,075.00.
Amesema  kiwango hicho cha fedha wanachodaiwa kukidhulumu viongozi hao ni takribani mara tatu (3) ya kiwango kilichobainika awali ambapo baada ya Viongozi hao kuhojiwa wamekubali kulipa deni lote wanalodaiwa kabla ya kuisha kwa Mwaka 2019.
 Brigedia Mbungo amesema zoezi hilo litakuwa endelevu na halitokoma mpaka wahakikishe wakulima wote wamelipwa stahili zao kwa mujibu wa Sheria na kwamba fedha zote zilizorejeshwa kiasi cha Sh. 255,598,194.00 zimeshaanza kugawiwa kwa walengwa ambao ni wakulima wa Ufuta kupitia kwa Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Lindi, Robert Nsunza chini ya Usimamizi na uangalizi wa TAKUKURU.
Pia amesema katika zoezi la kurejesha fedha za wakulima, Takukuru imekuwa ikitambua mali za watuhumiwa, kuzipiga picha na kuzikamata mali za viongozi hao wa AMCOS ambazo zimekuwa zikidaiwa kama dhamana ya madeni wanayodaiwa kwa wakati kama walivyoahidi ili kuziuza endapo watashindwa kutimiza ahadi zao.
“Ili kuwathibitishia kuwa TAKUKURU haina utani katika zoezi hili tunaendelea na zoezi la kutambua, kuzipiga picha na kukamata mali za viongozi wa AMCOS zinazodaiwa kama dhamana ya madeni wanayodaiwa, na endapo viongozi hao watashindwa kukamilisha malipo ya madeni wanayodaiwa kwa wakati kama walivyoahidi kwa maandishi wao wenyewe kwa hiari yao basi mali husika zitataifishwa kwa mujibu wa Sheria ili wakulima wa Ufuta wapewe fedha zao.
Aidha Brigedia Mbogo amewataka Viongozi wote wa Vyama vya Ushirika nchini vinavyodaiwa na Wakulima viwalipe wakulima wao haraka iwezekanavyo kabla TAKUKURU haijawafikia na kwamba katika zoezi hilo hakuna chama cha ushirika kinachodaiwa ambacho kitabaki salama.
Amesema zoezi la ufuaitliaji wa malipo ya Wakulima kwa Vyama vya Ushirika ni endelevu na pindi litakapokamilika Takukuru itatoa taarifa kamili.

Amewataka wananchi wenye ushahidi wa dhuluma iliyofanywa kwa wakulima wa ufuta ama kwa yeye mwenyewe kudhulumiwa au kuhujumiwa kwa namna yoyote ile katika biashara ya Ufuta, wafike katika ofisi za TAKUKURU zinazopatika katika Mikoa na Wilaya zote nchi nzima.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2nZfhHl
via
logoblog

Thanks for reading TAKUKURU YAKAMATA MAPAPA 99 WA AMCOS WANAODAIWA KUDHULUMU WAKULIMA LINDI, NI UTEKELEZAJI WA AGIZO LA RAIS DKT MAGUFULI ALOTOA OKTOBA15,2019

Previous
« Prev Post